
Wanadiplomasia wakuu kutoka Kenya na Jamhuri ya Dominika wamekutana mjini Santo Domingo siku ya Jumatatu na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuheshimu na kuongeza ufadhili ulioahidiwa kwa ujumbe wa usalama unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika nchi jirani ya Haiti.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Dominika, Roberto Alvarez na mwenzake wa Kenya, Musalia Mudavadi, wameonya kwamba Ujumbe wa Kimataifa wa Kuimarisha Usalama (MSS) nchini Haiti unajitahidi kukabiliana vilivyo na ghasia za magenge nchini kutokana na ukosefu wa fedha na usaidizi wa vifaa.
Kenya ilipeleka maafisa kwa MSS mnamo mwezi Juni 2024. Ujumbe huo unajumuisha takriban wafanyakazi 1,000, takriban 75% kati yao wanatoka Kenya.
Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2025 pekee, zaidi ya watu 1,600 waliuawa nchini Haiti na zaidi ya milioni 1 walikimbia makazi yao, kulingana na makadirio ya Umoja wa Mataifa.
Mawaziri hao wawili “wametambua kuwa Ujumbe haungeweza kuwa na ufanisi zaidi kutokana na ukosefu wa rasilimali za kifedha na vifaa muhimu kwa ajili ya kutumwa kikamilifu na kwa ufanisi kwa askari wanaopiga kambi nchini Haiti,” kulingana na taarifa rasmi.
Wameiomba jumuiya ya kimataifa “kutekeleza michango iliyopendekezwa, na hata kuiongeza, ili ujumbe huo ufanye kazi kikamilifu.”
Magenge yenye silaha kali yameongeza udhibiti wao nchini Haiti mwaka huu huku MSS na polisi wa eneo hilo wakipambana kuzuia ghasia zinazozidi kuongezeka.
Ujumbe huo, unaoongozwa na Kenya na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka wa 2023, bado umetumwa kwa sehemu kutokana na ahadi za ufadhili ambazo hazijatekelezwa.