YANGA inajiandaa kushuka uwanjani leo jioni kuvaana na Namungo ya Lindi, ikiwa ni mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara iliyoingia raundi ya 27, lakini ndani ya ofisi za mabosi wa klabu hiyo kuna mchakato wa maana unaendelea juu ya kusaka kocha mpya ajaye wakirusha kesho kwa kocha Mswisi.
Yanga imefanya mazungumzo ya awali na wasimamzi wa aliyekuwa kocha mkuu wa Al Ahly ya Misri, kocha Marcel Koller, raia wa Uswisi ili aje kuifundisha timu hiyo msimu ujao, ikielezwa timu hiyo ya Jangwani inajiandaa kuachana na kocha wa sasa, Miloud Hamdi.
Koller alilazimika kuingia makubaliano maalum na Ahly kufuatia kikosi hicho kutolewa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mshtuko na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kulitema taji ililokuwa inalishikilia.
Koller ameipa Al Ahly ubingwa wa Afrika mara mbili mfululizo kabla ya kuishia nusu fainali msimu huu, lakini mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria walimrushia makopo kocha huyo mara baada ya kutolewa na Mamelodi.

Licha ya Koller kuwa alikuwa akilipwa fedha nyingi na Ahly, hatua hiyo haijaikatisha tamaa Yanga na imeamua kumfuata ikijua kwamba kocha huyo bado anaweza kufanya uamuzi kulingana na utofauti wa klabu hizo mbili.
“Inajulikana kwamba Koller alikuwa analipwa fedha nyingi, lakini ile ni Ahly na hii ni Yanga, tumewapa mradi wetu wataupima na kufanya uamuzi, tunasubiri majibu yao,” alisema bosi huyo wa juu wa Yanga aliyeongeza;
“Unajua huwezi kuishi bila malengo, tunataka kuwa na makocha ambao wamefanya vizuri Afrika iwe kufika nusu fainali, fainali au hata kuchukua makombe ya Afrika kwa kuwa hayo ndio malengo yetu kwa sasa.”
Mbali na Koller, Yanga pia imefanya mazungumzo na kocha Jose Riveiro raia wa Ureno aliyemalizia msimu na klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini kisha atatimka.
Riveiro amekuwa na msimu bora akiwa wa Pirates akiishia nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika akitolewa na Pyramids ya Misri ambapo mapema alishawaaga mabosi wake kuwa mwisho wa msimu huu atatimka.

Kesho jioni Orlando itashuka uwanjani kupambana na Golden Arrows ambao huo utakuwa mchezo wa mwisho kwa Riveiro ndani ya klabu hiyo lakini pia inaelezwa kuwa Al Ahly nayo inamvizia akiwa mmoja kati ya makocha inaowataka ambaye anafundisha barani Afrika.
Waarabu hao hesabu zao za kwanza ni kupata kocha mkubwa anayefundisha klabu za Ulaya wakiwa tayari wameshatoswa na Rafa Benitez waliyempa ofa kubwa ingawa raia huyo wa Hispania amechomoa.

Yanga jioni ya leo inavaana na Namungo katika mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, ikiwa ni moja ya mechi nne zinazopigwa kwenye viwanja tofauti ikiwamo ile wa mapema saa 8 mchana ambapo JKT Tanzania itavaana na Fountain Gate, huku KenGold na Pamba Jiji zikiumana kwenye Uwanja wa Sokoine kuanzia saa 10:00 jioni na usiku Azam itakuwa vitani dhidi ya Dodoma Jiji.