Mambo manne waliyojadili Kapteni Traoré, Putin Russia

Ouagadougou. Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré, amehitimisha ziara yake nchini Russia alipohudhuria sherehe za Siku ya Ushindi wa Russia (Victory Day) dhidi ya utawala wa Kinazi wa Adolf Hitler.

Traoré, aliyesafiri kwenda Russia kwa kutumia ndege aliyotumiwa na rafiki yake, Rais Vladimir Putin, kisha kurejea nchini mwake, alishiriki kikamilifu katika sherehe hizo, ikiwemo kushuhudia gwaride la jeshi la nchi hiyo.

Katika sherehe hizo zilizofanyika Jumamosi, Mei 9, 2025, Traoré aliungana na marais wengine wa mataifa washirika wa Russia, akiwemo Rais Reccep Tayyip Erdoğan (Uturuki), Aleksandar Vučić (Serbia), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe), na Rais Xi Jinping wa China.

Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, Abdel Fattah el-Sisi (Misri), Nicolás Maduro (Venezuela), Mahmoud Abbas (Palestina), Ilham Aliyev (Azerbaijan), Thongloun Sisoulith (Laos), na Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico.

Walichozungumza Putin, Traoré

Baada ya gwaride la maadhimisho ya siku hiyo (Victory Day), Rais Putin alifanya mazungumzo na wawakilishi wa mataifa mbalimbali yaliyoshiriki, akiwemo Traoré, ambapo miongoni mwa mambo yaliyozungumziwa ni diplomasia ya kimataifa.

Katika hotuba yake mbele ya Rais Putin, Kapteni Traoré alifichua siri ya migogoro, umaskini na makundi ya kigaidi yanayoyatesa mataifa ya Afrika, ikiwemo Burkina Faso, kuwa ni matokeo ya ukoloni.

Traoré alisema Burkina Faso, ambayo ni mwathirika wa ukoloni, inapambana kujinasua dhidi ya matendo hayo, huku akiishukuru Russia kwa kusaidia kupeleka wataalamu wake wa kijeshi nchini mwake kujenga uwezo wa vikosi vya Burkina Faso.

“Tunatambua mbali na eneo la kiusalama na afya, kuna eneo lingine la sayansi na elimu na tungependa kuona Russia ikitusaidia kutoa mafunzo na kuwasomesha vijana wetu ili kutusaidia kuendeleza viwanda vyetu wenyewe,” alisema Traoré.

Mbali na eneo la usalama, Traoré alimuomba Rais Putin kuyasaidia mataifa ya Afrika, hususan Burkina Faso, katika sekta ya elimu, afya, sayansi na teknolojia, na viwanda.

“Tunaamini kuwa ugaidi tunauona sasa ni matokeo ya ukoloni ambao ndiyo kitu tunachopambana nacho nchini kwetu. Kama tukiwa na jeshi imara, tunaweza kupambana na ukoloni na kuendeleza taifa letu, ndiyo maana unaona hatukati tamaa na tunaendelea kupambana na makundi ya kigaidi nchini kwetu,” alisema.

Katika hatua nyingine, Traoré alisema kwa ushirikiano na Russia, Taifa hilo halitatoa mwanya wa vitendo vya uhalifu na ugaidi vinavyochochewa na mataifa yasiyolitakia mema, ikiwemo kuwatumia wataalamu wa Russia walioko Burkina Faso kukabiliana na vitendo hivyo.

“Nimeangalia gwaride na wanajeshi wa Russia waliopita mbele yetu (viongozi), tumeona vifaa vilivyotumika tangu Vita ya Kwanza ya Dunia na ya Pili na vifaa vya kisasa. Tungependa kuona ushirikiano kati ya mataifa yetu ukizidi kukua kwa kasi na kwa kina. Tunakushukuru kwa mtazamo wako ambao umekuwa nao juu ya Burkina Faso,” alisema.

“Tunatamani kuona Burkina Faso ikikua kwa kasi, watu wakijifunza kutoka Russia masuala ya sayansi. Kuna tafiti mbalimbali tunajua zimefanyika huku Russia, tungependa kuona ushirikiano wa kijeshi ukizidi kuimarika kati ya Russia na Burkina Faso, na kuimarisha ulinzi nchini kwetu,” alisema kiongozi huyo.

Awali, Rais Vladimir Putin wa Russia, mbali na kuwashukuru viongozi wa mataifa yaliyohudhuria sherehe hizo za miaka 80 tangu kukomeshwa utawala wa Kinazi chini ya Hitler, alisema Russia itaendelea kuiunga mkono Burkina Faso.

Alisema hadi kufikia 2024, Russia ilikuwa imepokea raia zaidi ya 350 wa Burkina Faso walioingia nchini humo kwa lengo la kupata elimu katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu, huku akidokeza mwaka huu Russia itakuwa tayari kupokea raia 27 wa Burkina Faso.

“Burkina Faso ilipambana vilivyo na vikosi vya Adolph Hitler, na sasa tunashirikiana kwenye mapambano ya kutokomeza ugaidi. Tutaendelea kuiunga mkono katika kupambana na ugaidi na kuhakikisha tunaisaidia kuweza kupambana na vikwazo visivyozingatia sheria,” alisema Putin.

Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traoré (kulia) akisalimiana na Rais wa Russia, Vladimir Putin. Picha na Mtandao

Rais Putin alisema tayari mataifa hayo yameanza mchakato wa kuunda Serikali ya pamoja itakayokuwa ikishirikiana kikamilifu kupambana na changamoto zikiwemo za kiusalama, kiuchumi, hususan vikwazo kutoka mataifa ya Ulaya, na ugaidi.

“Tunapaswa kuendeleza ushirikiano huu, hususan wa kibiashara kati ya Russia na Burkina Faso. Na tutaendelea kufanya ushirikiano kuendesha ukuaji wa kiuchumi na kuongeza mawanda kwenye uhusiano wa kiuchumi,” alisema Putin.

Alisema mataifa hayo yataendeleza ushirikiano wa kiutamaduni na huduma za kibinadamu, ambapo Ubalozi wa Russia uliopo Ouagadougou umekuwa kiungo muhimu kuimarisha miundombinu ya afya kwa raia wa Burkina Faso.

“Mwaka jana (2024) tulipeleka tani 25,000 za chakula, na mwezi huu uma tena msaada wa chakula. Tunashukuru na kutambua mchango wa Burkina Faso katika majukwaa ya kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) na mengine. Tutaendelea kuimarisha ushirikiano huu,” alisema Rais huyo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *