
Kuanzia mwaka 2016, nchi yetu inapitia katika kipindi chenye wimbo la makundi ya wahalifu wenye silaha, tena zingine za kivita, wakiteka raia, kuwatesa, kuwapoteza na wengine kuuawa kikatili. Hivyo kuibua hofu kwa jamii yetu.
Kutokana na wimbi hili, hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kusimama kwa ujasiri na kusema yupo salama kwani matukio haya yamewakumba wanasiasa, wanaharakati, wakosoaji mitandaoni, viongozi wa dini na raia.
Lakini kwa mtazamo wangu, yapo makundi 10 ambayo kama yataunganisha nguvu na kusimama kidete, nina uhakika wimbi hili la utekaji ambalo linachochea chuki kubwa kati ya raia na Serikali yao na vyombo vyake, litakuwa historia.
Kabla sijayataja makundi hayo, ningependa kurejea Ibara ya 13(6)(e) ya Katiba ya Tanzania inayosema ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha, ili kuuliza nani wanafanya haya?
Lakini kwa Katiba hiyohiyo, Ibara ya 14 inasema kila mtu anayo haki ya kuishi na kwa maneno sahihi inasema “Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii, hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria”, sasa nani wanaoua wenzetu?
Hakuna utetezi wowote unaokubalika kuhalalisha mauaji na matendo haya.
Usiku wa kuamkia Mei 2,2025, Taifa letu lilishtushwa na taarifa za kutekwa kwa mwanaharakati na mwanachama wa Chadema Jijini Mbeya, Nyagali Mdude kulikoambatana na umwagaji mwingi wa damu na hadi leo hajulikani alipo.
Septemba 7, 2024, mzee Ally Mohamed Kibao, aliyekuwa mjumbe wa Sekretarieti taifa ya Chadema, akiwa katika basi la Tashrif, alishushwa na watu wenye silaha za kivita, kumfunga pingu na kuondoka naye na kwenda kumuua kikatili.
Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna alivyoonyesha kusikitishwa na tukio hili na akaagiza vyombo vya uchunguzi, kumpelekea taarifa ya kina ya tukio hilo baya na mengine ya aina hiyo, akisema ni matukio yasiyovumilika.
Bahati mbaya sana, hadi ninapoandika makala hii hakuna taarifa rasmi iliyotolewa na vyombo vya uchunguzi juu ya tukio hili na matukio mengine ya kupotea kwa watu kama Deusdedith Soka, Immanuel Mbise na Jacob Mlay waliotekwa pamoja.
Wengine waliotekwa katika wimbi hilo ni Deonis Kipanya aliyekuwa kiongozi wa Baraza la Vijana (Bavicha), Sumbawanga, Shedrack Chaula aliyedaiwa kuchoma picha ya Rais na kupigwa faini, na kada wa CCM Mwanza, Daniel Chonchorio. Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana. Pia, Machi 15, 2025 Katibu wa CCM kata ya Chitete wilayani Ileje aliuawa na watu wasiojulikana. Kimsingi matukio ni mengi na yanatishia usalama wa wananchi.
Orodha ni ndefu, lakini kwa minajili ya makala hii, matukio hayo machache niliyoyaeleza yanatosha kabisa kuonyesha hofu iliyonayo jamii ya Watanzania, kiasi kwamba mtu ana uhakika tu wa kutoka nyumbani, ila siyo wa kurudi.
Nimetangulia kusema kuna makundi 10 ambayo kama yakisimama kidete yanaweza kutokomeza uhalifu huu na kundi la kwanza ni la viongozi wetu wa dini, kuanzia maaskofu, mufti, masheikh, mapadre, wainjilisti na maimamu wetu.
Askofu mkuu Desmond Tutu alipata kusema if you are neutral in situations of injustice, you have chosen the side of the oppressors”, akimaanisha: “Ikiwa hauegemei upande wowote katika dhuluma, umechagua upande wa wadhalimu”.
Kwa upande wa Waislamu, Mtume Mohamed (SAW), anawataka Waislamu kuwa kujihadhari na dhulma kwani itakuwa giza siku ya Kiyama, kwa hiyo dini zote iwe Uislamu au Ukristo, unapinga vitendo vya dhuluma na ukandamizaji haki.
Viongozi wetu hawa, wakiungana na kupaza sauti ya kinabii pamoja kukemea haya yanayoendelea nchini kwetu nina hakika haya maovu yatatoweka kama si kupungua, kwa kuwa wanaoyafanya nina hakika baadhi ni waumini wao.
Lakini, kukaa kimya kwa baadhi ya viongozi wetu wa dini na kujitizama wao kwa vile hayajawakuta wao au ndugu zao, watoto wao au familia yao, nina hakika ni jambo ambalo halimpendezi Mwenyezi Mungu.
Kama alivyosema Askofu Mkuu Tutu, kiongozi yeyote wa dini ambaye amechagua kuunga mkono wadhalimu kama hao watekaji basi naye hana tofauti na mtekaji, lakini wakipaza sauti za kinabii kwa umoja wao, hata watekaji watasalimu amri.
Kundi la pili ni la waandishi wa habari ambao wanatambulika kama mhimili wa nne usio rasmi, kwani siku zote wanasema kalamu ni kama silaha, wangeitumia vizuri kalamu yao kukemea na kufichua matendo haya nina hakika yangetoweka.
Ninawapa mtihani kidogo, fuatilieni vyombo vyetu vya habari mje mniambie ni vyombo gani ambavyo vinaandika sana kuhusu utekaji na kupotea kwa watu? Kuna vyombo vya habari (sio vyote), vimeamua kusimama upande wa watekaji.
Ni kwa nini? Ni kama mwandishi wa vitabu kupitia kitabu chake cha Ham on Rye alivyosema “I guess the only time most people think about injustice is when it happens to them,” kwamba hawafanyi hivyo kwa kuwa tu hayajawakuta.
Lakini vyombo vya habari vya Tanzania kwa umoja wao, vingetumia nadharia ya kupanda ajenda au “agenda setting”, kukabiliana na wimbi hili la utekaji kama Vicky Ntetema wa BBC alivyofanya kuhusu mauaji ya albino.
Nadharia hii ambayo ilianzishwa na Maxwell McCombs na Donald Shaw mwaka 1972, inapendekeza vyombo vya habari kuunda mtazamo wa umma kwa kuangazia mada fulani kuliko zingine na kuzifanya zionekane muhimu zaidi.
Lakini ninachokiona ni kuwa vyombo vyetu vingi vya habari vinaona kama ni dhambi vile kuandika wimbi la watu kutekwa na kupotea na kuviachia vichache kama Mwananchi, The Citizen, Jamhuri, Pambazuko na Online Tv.
Ni vyombo vya habari pekee, bila kuangalia uhusiano wao na baadhi ya taasisi za Serikali au uanachama wao katika vyama vya siasa, ungeiamisha nchi kuona tatizo hili linahitaji mjadala wa kitaifa kwa sababu linachochea chuki na Serikali.
Kundi lingine ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba kama lingetumia vyema mamlaka liliyonayo kupitia Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Tanzania, nina uhakika matendo haya mabaya na ya kikatili yangetoweka nchini kwetu.
Katiba inasema Bunge ndicho chombo kikuu hapa Tanzania ambacho kitakuwa na madaraka, kwa niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.
Pamoja na mamlaka haya, lakini sijaona Bunge likijadili matukio haya kwa niaba ya wananchi, na badala yake mara kadhaa mbunge alipoibua hoja ya kutaka suala hili lijadiliwe kwa dharura, hugonga mwamba kwa kigezo cha kanuni.
Nina uhakika, kama Bunge lingeiwajibisha Serikali kwa matukio haya, leo hii tusingekuwa na hali iliyopo sasa ambapo raia wanatekwa na kupotezwa na genge la wahalifu linaloonekana kuwa na nguvu kubwa na silaha za kisasa.
Mhimili wa Mahakama nao ni kundi moja muhimu ambalo linapaswa kuhakikisha utawala wa sheria unatamalaki katika nchi yetu, kwa kuwabana wale walio madarakani ili wasitumie vibaya madaraka waliyopewa kisheria.
Sheria zinazotoa madaraka lazima zitafsiriwe na Mahakama kwa ukali mkubwa dhidi ya wale walio madarakani ili wasidhulumu au kukandamiza raia, lakini pia watawala wasikubaliwe kutenda chochote ambacho hakiko katika sheria.
Yanapofunguliwa maombi ya Habeas Corpus kuwa mtu fulani alichukuliwa na Polisi lakini hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24 wala hajulikani alipo, isikubali kuyumbishwa na ufundi wa kisheria, kusimama upande wa wanaolia.
Kundi lingine ni la wananchi, wangetumia nguvu ya umma kukabiliana na watekaji haya mambo yangekomeshwa nchini, kwamba mtu akija kumkamata raia mtaani kwetu au barabarani, utaratibu ambao umewekwa kikatiba ufuatwe.
Kwa sababu matukio karibu yote, ambao wametekwa, kupotezwa au kuuawa, waliowachukua na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi, kiasi kwamba kwa sasa ni vigumu kutofautisha kati ya watekaji na polisi wa kweli wanaotekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria.
Katikati ya mazingira kama haya, nguvu ya umma inahitajika watu kukamatwa kiholela pasipo kufuata sheria na ni muhimu, kila raia awe tayari kuchukua picha za mnato au video za wakamataji na magari wanayoyatumia.
Mitandao ya kijamii itumike kusambaza picha na video hizo pale ambapo raia mwenzao aliyekamatwa na watu waliojitambulisha ni polisi anakuwa haonekani, lakini wanaposikia yowe la kuomba msaada, wajitokeze kwa wingi kutoa msaada.
Kundi lingine ni Idara ya Usalama wa Taifa, hawa ni mabingwa wa kukusanya taarifa za kiintelijensia kwa usalama wa nchi, hivyo wanaweza kuvisaidia vyombo vingine kama Polisi kwa kuwapa taarifa za Kiintelijensia za magenge haya.
Lakini kuna makundi kama ya wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na wanasheria kupitia Tanganyika Law Society (TLS) na wanasiasa wana wajibu wa kuamsha vuguvugu la kukataa yanayoendelea na kusimika utawala wa sheria.
Makundi hayo yakitimiza wajibu wao ipasavyo nina uhakika matukio haya yatakoma kama si kupungua katika jamii yetu na tutaokoa maisha ya wengi.
0656600900