Buchosa. Uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umesisitiza kuendelea kampeni ya ‘No reforms, no election’ kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi bila kujali vitisho vya kukamatwa, kuswekwa mahabusu wala gerezani.
Msimamo huo umetolewa leo Mei 12, 2025 na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika Kijiji cha Bukokwa katika Halmashauri ya Buchosa na uwanja wa Stendi ya zamani mjini Sengerema ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kampeni ya ‘No reforms, no election’, inayoendelea mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema amepata taarifa kutoka kwa watu na vyanzo vya kuaminika kuwa kuna mpango wa kumkamata yeye pamoja na viongozi kadhaa wa kitaifa wa chama hicho kwa lengo la kudhoofisha kampeni yao, inayolenga kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi utakaorejesha mamlaka ya wananchi wa kuchagua na kuwajibisha viongozi wao.
“Hakuna kesi, vitisho, mahabusu ya polisi wala gereza itazuia kiu ya mabadiliko mioyoni mwa Watanzania,” amesema Heche.
Huku akitumia mfano wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere, Heche amesema tangu enzi za ukoloni, harakati zote za kudai mabadiliko zimekutana na vikwazo na vitisho vya jela kwa sababu wenye madaraka hawako tayari kuruhusu haki na usawa kwa wote.

“Mwalimu Nyerere angeogopa vitisho vya polisi, kesi za kutunga na kufungwa magereza leo hii Tanzania bado tungekuwa tunatawaliwa na wakoloni; hata sisi tunajua tutakumbana na vikwazo vya kukamatwa na polisi, kufunguliwa kesi na hata kufungwa jela, lakini hatutarudi nyuma,” amesema Heche.
Akitumia mifano ya wapigania uhuru wengine barani Afrika akiwemo Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Samora Machel wa Msumbiji na Sam Nujoma wa Namibia, Heche amesema mapambano ya kudai haki hayajawahi na kamwe hayatakuwa mepesi kwa sababu wanaokiuka haki hizo hawatakubali kirahisi kuacha matendo yao maovu hadi washinikizwe na nguvu ya umma.
“Sisi Chadema tumejitolea kulipa gharama za mapambano ya kudai haki na usawa kwa wote; hatutarudi nyuma hata wakiwakamata viongozi wetu wote,” amesema Heche.
Huku akionyesha msisitizo, Heche amesema; “Serikali ilitarajia tutarudi nyuma baada ya kumkamata na kumfungulia kesi Lissu. Sasa wameingiwa hofu baada ya kuona kampeni ya ‘No reforms, no election’ inachanja mbuga ndio maana wanafikiria kunikamata. Nawaapia wanajidanganya kwa sababu hakuna vitisho, kesi wala magereza itazima moto huu.”

Amerejea kauli yake kuwa Chadema haina ugomvi binafsi na viongozi wa Serikali na CCM, bali inatofautiana nao katika sera na mfumo wa uongozi na matumizi ya fedha na rasilimali za Taifa.
Akizungumzia taarifa za mpango wa kumkamata Heche, Katibu Mkuu wa zamani wa Chadema, Dk Wilbdroad Slaa amesema; “Hatua hiyo itaongeza moyo, ari na kasi ya Watanzania kudai mabadiliko; tena wafanye haraka kumkamata waone jinsi kampeni ya ‘No reforms, no election’ inavyoshika kasi.”
Kauli hiyo imeungwa mkono na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila akisema; “Wanaodhani kumkamata Heche kutapunguza kasi ya kudai mabadiliko wanajidanganya; wafanye haraka kumkamata waone jinsi mimi na viongozi wengine tutakavyoendelea kukiwasha kila kona ya nchi kudai mabadiliko.”
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, Brenda Ruphia amewaomba Watanzania kila mtu kwa nafasi na eneo lake kuunga mkono kampeni za kudai mabadiliko yatakayoleta maisha bora kwa kila mtu.