Sh131.3 bilioni kutekeleza vipaumbele tisa, Katiba na Sheria

Unguja. Wizara ya Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora, imepanga kutekeleza vipaumbele tisa huku ikiliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh131.337 bilioni.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni kuendeleza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika utumishi wa umma, kukamilisha na kuendeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu ya Mahakama.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka 2025/26 ya wizara hiyo, barazani leo Mei 12, 2025, Waziri mwenye dhamana, Haroun Ali Suleiman amesema wizara imepanga kuendelea kuimarisha utendaji katika taasisi za sheria na kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali.

Pia  wataanza utekelezaji wa mikataba ya uwajibikaji kwa viongozi na kuanzisha programu za mafunzo ya kujenga umahiri wa watumishi wa umma na kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi.

“Kusimamia misingi ya utawala bora, maadili na kuongeza mapambano dhidi ya rushwa pamoja na ukaguzi na udhibiti wa rasilimali za umma,” amesema.

Ili kufanikisha vipaumbele hivyo ofisi imepanga kutekeleza malengo makuu ikiwa ni pamoja na kuimarisha upatikanaji wa haki na utawala wa sheria. 

Ofisi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kupambana na kupunguza kesi za udhalilishaji kutoka kesi 348 kwa mwaka 2023/24 hadi kesi 292 kwa mwaka 2024/25. 

Amesema idadi ya wananchi waliopatiwa msaada wa kisheria imeongezeka kutoka 122,149 kati ya hao wanawake ni 65,498 na wanaume 56,651 mwaka 2020 hadi kufikia wananchi 419,401 kati ya hao wanawake 226,172 na wanaume 193,229 mwaka 2023.

Aidha, idadi ya watoaji msaada wa kisheria imeongezeka kutoka 117 mwaka 2020 hadi 278 mwaka 2024. 

Waziri Haroun amesema juhudi pia zimechukuliwa za kuwawezesha watoaji wa msaada wa kisheria ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi kwa kupatiwa vitendea kazi ikiwemo usafiri, vishikwambi, printa na kompyuta mpakato.  

Katika bajeti hiyo, Kamati ya kudumu ya kusimamia ofisi za viongozi wakuu, imeitaka Serikali kwenye umaliziaji wa ujenzi wa mahakama, kujiandaa na upatikanaji wa vitendea kazi vya ofisi ikiwa ni pamoja na kutafuta namna bora ya uhifadhi majalada ambayo yamefungwa katika mahakama hizo, vikiwamo vielelezo hatarishi vya uhalifu ikiwemo dawa za kulevya.

Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), imesema imebaini kuna baadhi ya taasisi zinatozwa ada ndogo ikilinganishwa na mapato halisi ya taasisi hizo.

“Kwa msingi huo kamati yetu imeiagiza Ofisi ya Rais fedha na mipango kufanya tathmini itakayowezesha kutambua uwezo halisi wa makusanyo kwa taasisi zinazotozwa ada ya ukaguzi na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili ije na viwango vipya,” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo Juma Khatib wakati akisoma maoni ya kamati

Amesema pia kamati imebaini kwamba uwezo wa ofisi ya CAG kufikia malengo ya kukusanya Sh500 milioni iliyopangiwa ni mdogo kutokana na uhalisia kwamba hata taasisi zote zikilipa ada ya ukaguzi hawataweza kufikia hata nusu ya fedha za makadirio, ukizingatia hadi kufika Machi mwaka huu ofisi hiyo imekusanya asilimia 33.73 ya makadirio ya mapato ya mwaka 2024/25.

Katika makusanyo hayo ofisi hiyo imeongezewa makusanyo ya Sh177.6 milioni ikilinganishwa na bajeti iliyopita.

Wakichangia bajeti hiyo, mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih amesema licha ya Serikali kueleza kwamba msaada wa kisheria umeongezeka kwa kiasi kikubwa lakini wanaofaidika na msaada huo sio walengwa.

“Inawezekana watu wanafanya kazi kubwa, lakini walengwa hawafikiwi, lengo la programu hii ni kuwasaidia wenye mahitaji ambao kimsingi hawana uwezo lakini ukiangalia mtaani wapo wananchi wengi hawajafikiwa,” amesema.

Naye Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Suleiman amesema taasisi zote ambazo ofisi ya CAG inatoza ada makusanyo yake hazikufikia asilimia 50.

Amesema tatizo lipo kwenye taasisi zenyewe na iwapo zikiona hazina uwezo wa kukusanya ni vyema wakuu wa taasisi wakae na wizara ya fedha wajadiliane na kupunguziwa malengo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *