Wizara, jumuiya za utalii wabuni mpango kuongeza watalii Zanzibar

Unguja. Ili kufikia lengo la Serikali kuingiza watalii 829,00 mwaka huu, Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wengine wameingia makubaliano na taasisi tano kufanikisha azma hiyo.

Miongoni mwa taasisi zilizoingia makubaliano ni Jumuiya ya Waandaa Misafara (Zato), Jumuiya ya Wawekezaji wa utalii Zanzibar (Zati), Jumuiya ya Watembeza Watalii Zanzibar (Zatoga), Jumuiya ya mahoteli Zanzibar (Haz), Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) pamoja na kamisheni ua utalii.

Katika ushirikiano huo wa kukuza utalii kisiwani hapo, pia utafanyika mkutano wa utalii na uwekezaji Mei 20 na 21 mwaka huu kisiwani hapa na kuwakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali.

Akizungumza wakati wa kusaini makubaliano hayo leo  Mei 12, 2025, Waziri mwenye dhamana, Mudrick Ramadhan Soraga amesema taasisi hizo ni mhimu katika sekta ya utalii na ushirikiano ambao umelenga kukuza utalii kisiwani hapo.

“Wizara inaangalia njia za kubuni jinsi ya kuboresha zaidi maonyesho ya utalii na uwekezaji lakini kutanua wigo wa ushirikiano, ambao tunaamini tukishirikiana tunaweza kupata matokeo chanya, makubwa na utalii ukakua zaidi,” amesema.

Amesema maonyesho ya utalii na uwekezaji yanachukua nafasi ya kwanza kwa visiwa vya Zanzibar na yanayoleta wadau kutoka Tanzania bara na visiwani na  yatakayoendelea kukuza sekta ya utalii nchini.

Aidha amesema wizara inachukua hatua mbalimbali kuboresha, kusimamia na kuiratibu sekta hiyo vizuri ili iendelee kukuza uchumi wa nchi ambapo  inachangia asilimia 20 ya pato la Taifa.

Naye Mtendaji Mkuu wa maonyesho hayo, Javed Jafferji amesema ili kuyafanikisha ushirikiano wa pamoja unahitajika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukuza pato la Taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZNCC, Hamad Hamad amesema jumuiya yao imeunga mkono jitihada hizo ambazo zina umuhimu mkubwa kwa Zanzibar kuendelea kuvutia watalii kutoka nje na ndani ya nchi.

Amesema wadau wote kwa pamoja wanaunga mkono jitihada za kamisheni ya utalii na wizara katika masuala yote yanayohusu utalii kushirikiana pamoja, ili kuendelea kuimarisha sekta hiyo visiwani Zanzibar.

Kwa upande Aziz Ramadhan kutoka Zatoga, ushirikiano huo ni  muhimu kwa wadau kuwa na sauti moja katika kuendeleza sekta hiyo nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Zati, Fatma Ali Mohammed, aliipongeza wizara kwa kukubali ushirikiano huo ambao utasaidia kuifanya Zanzibar kuendelea kutambulika duniani kupitia sekta utalii na kukuza uchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *