
Shirika la ulinzi wa raia la Palestina limeripoti siku ya Jumatatu, Mei 12, kwamba “angalau” watu kumi wameuawa, ikiwa ni pamoja na wanawake kadhaa na watoto, katika shambulio la usiku la Israeli dhidi ya shule wanakopewa hifadhi watu waliokimbia makazi huko Jabalia, kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
“Watu wasiopungua kumi (waliouawa), wakiwemo wanawake na watoto kadhaa, pamoja na makumi ya majeruhi, wamesafirishwa kufuatia shambulio la anga la Israeli kwenye shule ya Fatima Bint Assad, wanakopewa hifadhi zaidi ya watu 2,000 waliokimbia makazi yao katika mji wa Jabalia,” amesema msemaji wa shirika la ulinzi wa raia Mahmoud Bassal huko Gaza.
Orodha ya wahasiriwa inaendelea kuongezeka. Siku ya Jumamosi, Mei 10 shirika la ulinzi wa wa raia la Palestina lilitangaza vifo vya watu watano katika shambulio la anga la Israeli dhidi ya nyumba iliyoezekwa kwa hema ambapo walikuwa wakiishi watu waliokimbia makazi yao katika Jiji la Gaza. Kulingana na ndugu wa marehemu, waathiriwa walikuwa wanandoa na watoto wao watatu, waliouawa wakiwa wamelala.
Jeshi la Israeli, ambalo lilianza tena mashambulizi yake dhidi ya vuguvugu la Kiislamu la Palestina la Hamas katika Ukanda wa Gaza mnamo Machi 18 baada ya kusitishwa kwa mapigano kwa miezi miwili, halijazungumza lolote katika hatua hii. Picha za shirika la habari la AFP kutoka eneo la tukio zinaonyesha watu wakitoa heshima zao mbele ya sanda tano nyeupe za ukubwa tofauti. “Watoto watatu, mama yao na mume wake walikuwa wamelala ndani ya hema na walishambuliwa na ndege [ya Israeli] bila ya onyo na bila ya wao kuwa na hatia” ya chochote, Omar Abu al-Kass, ambaye anajitambulisha kama babu wa uzazi wa watoto kwa upande wa mwanamke, ameliambia shirika la habari la AFP.