Mbeya. Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), imekabidhiwa rasmi mradi wa kuunganisha umeme katika vitongoji 105 mkoani Mbeya.
Mradi huo wenye thamani ya Sh10.9 bilioni umetekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), utanufaisha wateja takriban 3,465.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya mradi huo iliyofanyika leo Kata ya Igawilo jijini Mbeya, Spika wa Bunge na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Akson, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi kupitia miradi ya mbalimbali ya maendeleo.
Amesema tangu mradi wa REA uanze mwaka 2021/ 2022, Serikali imetenga Sh71 bilioni kwa Mkoa wa Mbeya kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini.
Hivyo, amemtaka Mkandarasi wa mradi ETDCO, kuhakikisha anaukamilisha kwa wakati ili wananchi wa mkoa huo waweze kunufaika na nishati hiyo ya umeme.
“Nchi yetu ina umeme wa kutosha kutokana na Mradi mkubwa wa Bwala la Mwalimu Julius Nyerere, hivyo mradi huu wa usambazaji wa umeme kwenye vitongoji 105 unatakiwa kutelezwa kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na Nishati hii ya Umeme”, amesema Dk Tulia.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka ETDCO, Mhandisi Dismas Massawe amesema kampuni yao iko tayari kutekeleza mradi huo kwa weledi na kwa wakati kama ilivyo anishwa kwenye mkataba.
Amesema lengo ni kuhakikisha wananchi hao wanapata nishati ya umeme kwa wakati uliopagwa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Meja Jenerali mstaafu, Jacob Kingu amewataka wananchi wa Mbeya kujitayarisha kwa kuweka miundombinu ya kupokea huduma ya umeme katika makazi yao ili waweze kunufaika ipasavyo na mradi huo.

Akizungumza na Mwananchi, Christina Mwampashi mkazi wa Igawilo, amesema mradi huo utawaongezea fursa za kufanya biashara mbalimbali.
“Unajua ukiwa na umeme nyumbani kwako, utafanya kila aina ya biashara kama utajiongeza, hii kwetu ni fursa,” amesema Mwampashi.
Naye George Sijaona, amesema ni wakati sasa wa kila familia kujitahidi kuweka umeme kwenye nyumba.
“Ukiwa na umeme, utawasaidia hata watoto wetu kusoma vizuri sasa, hawatawasha tena chemli au kibatari, tunaishukuru sana Serikali kwa hatua hii,” amesema Sijaona.
Naye Neema Mwakyanjala amesema mradi huo ni mkombozi kwao kwa sababu utaongeza fursa za kiuchumi kupitia shughuli zinazohitaji umeme zikiwamo za kilimo cha kisasa na usindikaji wa mazao.