Askofu Mndolwa: Katiba ifuatwe uchaguzi mkuu ni muhimu, usiahirishwe

Mbeya. Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana nchini, Dk Maimbo Mndolwa amesema uchaguzi mkuu usiahirishwe kama baadhi ya watu wanavyosemasema, badala yake changamoto zilizopo zifanyiwe kazi ili kuliepusha Taifa kuingia kwenye mgogoro wa kikatiba.

Pia, amewaasa wanasiasa kutotenganishwa na uchaguzi badala yake watumie nafasi hiyo kuunganishwa akieleza kuwa yapo maisha baada ya kazi hiyo kukamilika.

Askofu Mndolwa ameyasema hayo leo Jumapili Mei 11, 2025 katika ibada ya kumuweka wakfu na kitini, Canon Jacob Kahemele kuwa Askofu Mkuu wa tatu wa Dayosisi ya Southern Highlands iliyofanyika Kanisa Kuu la Kristo Mbeya.

Amesema nchi inaweza kuingia katika mgogoro mbaya wa kikatiba kama watasikiliza watu wanaotaka kuahirisha uchaguzi mkuu.

“Kwa kuwa Naibu Waziri Mkuu (Dk Doto Biteko) uko hapa, Spika wa Bunge (Dk Tulia Ackson) upo hapa, tuiombe jamii na Serikali kwa ujumla kupitia ninyi, tusiahirishe uchaguzi, mwisho tutaingia kwenye mtanziko mkubwa na mgogoro wa kikatiba tusipate pa kwenda,” amesema askofu huyo na kuongeza;

“Nchi tuliyopewa ya edeni na Mungu ni hii, kama zipo changamoto kaeni mzifanyie kazi, hata sisi uchaguzi wetu wa Dayosisi wapo waliosema tuahirishe lakini tumeweza kufanya kwa sababu ya mazungumzo.”

Ametoa rai kwa wanasiasa kutotumia siasa kama ndiyo mwisho wa maisha badala yake watumie nafasi hiyo kuwaunganisha, huku akikemea maneno ya kejeli, matusi akisema  kuna maisha baada ya uchaguzi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko akiwa katika picha ya pamoja na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Dk Maimbo Mndolwa na Askofu mteule wa Kanisa Kuu la Kristo Mbeya Dayosisi ya Southern Highlands, Jacob Kahemele

Akizungumza baada ya ibada hiyo, Dk  Biteko amesema milango ya Serikali iko wazi na amewasihi wenye hoja kujongea kwa mazungumzo.

“Ninachoweza kusema kuhusu uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, utakuwa huru na wa haki huku nchi ikiendelea kuwa na amani kama Katiba inavyotaka,” amesema Biteko.

Amesema Serikali ilipowasikia waliotaka marekebisho ya sheria zinazosimamia uchaguzi, ilipitia na kufanya marekebisho.

“Lakini bado milango ya Rais Dk Samia ipo wazi kwa yeyote mwenye kutoa malalamiko yake ili nchi iende mbele,” amesema Biteko.

Amewaasa Watanzania kuendelea kuiombea nchi ili amani iendelee kuwepo kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Amesema Serikali inathamini mchango wa madhehebu yote ya dini ikiwamo Kanisa la Anglikana. 

“Katika nyanja za elimu, afya, maji na maendeleo ya jamii, Serikali inashirikiana kwa karibu na taasisi za dini kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wananchi, hivyo ninyi ni muhimu sana,” amesema.

Akitoa salamu za Mkoa wa Mbeya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk Juma Homera, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewashukuru viongozi wa dini kwa namna wanavyoshirikiana na serikali akiomba kuwapo mwendelezo.

“Kanisa hili limekuwa mfano kwenye sehemu ya huduma kama elimu, niwahakikishie viongozi wa dini zote kwamba tutaendelea kushirikiana nao ili jamii izidi kupata huduma zote za msingi” amesema Malisa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *