Kigogo wa CUF atimkia ACT Wazalendo

Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo leo Jumapili Mei 11, 2025 kimempokea, aliyekuwa Katibu Mtendaji Jumuiya ya Vijana, Ofisa Mwandamizi ofisi ya Katibu Mkuu, Msaidizi wa Katibu Mkuu, Mjumbe wa Mkutano Mkuu na baraza kuu, Mjumbe wa Sekretarieti ya Chama cha Wananchi (CUF) taifa, Iddy Mkanza.

Hayo yanajiri wakati katika uga wa siasa nchini kukumbwa na wimbi la baadhi ya wanachama wa vyama wakitangaza kuachia ngazi katika vyama vyako ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), huku wengine wakiweka usiri wa wapi waendapo. 

Ingawa kwa upande wa kiongozi huyo aliyejiengua CUF, imekuwa tofauti kwa kuwa ametangaza wazi kujiunga na chama hicho kilichoanza mwaka 2014. 

Akizungumza baada ya kupokelewa makao makuu ya ACT Wazalendo Magomeni jijini Dar, Mkanza amesema kilichomtoa CUF ni kukosekana kwa uongozi, ajenda pamoja na malengo kama chama cha siasa. 

“Mimi uamuzi wangu unatokana na tafakuri ya kina nilioufanya kwa muda mrefu, sababu zilizonitoa CUF miongoni ni kupoteza misingi yake ya kutetea walala hoi. Migogoro isiyokwisha inayotawala CUF baina ya watendaji wakuu wa chama na waandamizi. 

“Chama hakiendeshwi kitaasisi bali matamko na maamuzi yote yanayoamuliwa na mtu mmoja. Maamuzi hayafanywi na vikao bali na Mwenyekiti wa chama,” amebainisha. 

Akieleza zaidi amesema chama kimepoteza malengo, uongozi, hata yeye ilifikia wakati akiikosoa Serikali anashushwa jukwaani. 
“CUF haina lengo la taifa, lengo la chama na lengo binafsi. Pia Chama hakina ajenda,” amedai. 

Amesema uwepo wa mazingira hayo ndani ya chama ndipo akaamua kukihama na kutimkia ACT Wazalendo.
Kilichompeleka ACT

Akitaja sababu kwa nini ametimkia ACT Wazalendo Mkanza amesema ni chama chenye mshikamano wa malengo, kinaweza kutatua matatizo ya ndani. 

“ACT ndiyo inatekeleza wajibu wa mapambano kudai haki za Watanzania masikini kwa sababu imejipambanua kwenye ajenda na mapambano yake,” ameeleza. 

Amesema chama hicho kimejikita kwenye hoja hata uchambuzi wa viongozi unaleta suluhisho la matatizo ya Watanzania.
Awali, akizungumzia ujio huo, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Chama cha ACT Wazalendo Abdul Nondo, amewaita watu wote wenye nia ya kupigania wananchi na kuondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani. 

“Tunapigania haki, demokrasia na ustawi wa wananchi wa Tanzania. Chama kinapoaminiwa na viongozi wa vyama vingine kwetu sisi ni faraja kubwa,” ameeleza Nondo. 

Amesema ujio wa Mkanza kwenye chama chao ni maamuzi sahihi kwakuwa ndilo jukwaa sahihi la kuing’oa CCM madarakani.
Mwananchi imemtafuta Katibu Mkuu wa CUF kwa njia ya simu pamoja na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mohamed Ngulangwa bila mafanikio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *