Ushahidi mama alivyomuua mwanawe, asiende kutoa ushahidi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeelezwa jinsi Sophia Mwenda (64) alivyoshirikiana na mwanawe wa kiume, Alphonce Magombola (36), kutekeleza mauaji dhidi ya binti yake wa kumzaa, Beatrice Magombola.

Imeelezwa kuwa baada ya kumuua, walichukua mwili wa marehemu kutoka nyumbani kwa marehemu eneo la Kijichi, wilayani Temeke, Dar es Salaam na kuutupa katika eneo la Zinga, Bagamoyo, mkoani Pwani.

Ushahidi huo umeeleza katika maelezo ya onyo aliyoyatoa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Sophia alikiri kuhusika na mauaji hayo, akifafanua kuwa aliamua kumuua binti yake ili kumzuia kutoa ushahidi katika kesi ya madai iliyofunguliwa na baba wa marehemu.

Kesi hiyo ilihusiana na uuzwaji wa nyumba ya familia iliyopo Mbeya, ambayo inadaiwa kuuzwa na Sophia kwa kushirikiana na mwanawe Alphonce, bila kushirikisha wala kupata ridhaa ya familia nzima.

Nyumba hiyo ya familia inadaiwa kuuzwa kwa Sh45 milioni na Sophia kwa kushirikiana na mwanawe, Alphonce bila kumjulisha mume wake, Dogras Mwagombola.

Kitendo hicho kilisababisha Dogras kufungua kesi mahakamani akipinga uuzwaji huo.

Kati ya fedha hizo, Sophia alipewa Sh12 milioni, ambapo alitoa Sh1 milioni na kumpatia binti yake mwingine, Rachel, aliyekuwa akiendelea na masomo, huku kiasi kilichosalia kikichukuliwa na Alphonce.

Maelezo hayo yalitolewa mahakamani Mei 9, 2025, na askari Polisi namba F 8858, DC Koplo Nicholaus kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay, wakati akiendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Mahakama.

Mshtakiwa Sophia Mwenda (64) akiwa na mwanae, Alphonce Mwagombola, wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, chini ulinzi wa askari magereza kusikiliza kesi yao ya mauaji ya mwanafamilia inayowakabili.

Koplo Nicolaus alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, aliyepewa mamlaka ya ziada kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.

Alieleza kuwa ndiye aliyefanya mahojiano na kurekodi maelezo ya onyo ya mshtakiwa, Sophia Mwenda, Machi 18, 2022, ambayo ameyasoma mahakamani.

Akiwa anaongozwa na mawakili watatu wa Serikali,  Daisy Makakala, Cathbert Mbiling’i na Violeth Davis, shahidi huyo alieleza kuwa siku hiyo ya Machi 18, aliitwa na kiongozi wake ofisini, ambapo alikabidhiwa jalada la uchunguzi la kesi inayomkabili Sophia na kupewa maelekezo ya kuchukua maelezo binafsi ya onyo kutoka kwa mshtakiwa huyo.

Akiwasilisha maelezo hayo, shahidi huyo alieleza kuwa Sophia aliyewahi kuwa mtumishi katika taasisi mbalimbali, zikiwemo idara za Ustawi wa Jamii, alifunga ndoa na Dogras Mwagombola na walijaliwa watoto wanne, wakiwemo Beatrice, Alphonce na Rachel.

Baadaye ndoa hiyo ilivunjika baada ya mumewe kuoa mke mwingine. Kufuatia hali hiyo, Sophia aliendelea na maisha yake akiwa anaishi nyumbani kwa Beatrice.

Desemba 1, 2020, alimpigia simu mwanawe Alphonce na kumwita nyumbani kwa Beatrice, eneo la Kijichi, shahidi alieleza.

“Sophia alinieleza kuwa alimpigia simu mwanawe, Alphonce na kumweleza wamepata taarifa kuwa Beatrice anatarajiwa kuwa mmoja wa mashahidi katika kesi iliyofunguliwa na Dogras huko Mbeya.

“Kwa hofu ya ushahidi huo, walikubaliana kumpiga Beatrice hadi apoteze uwezo wa kusafiri kwenda kutoa ushahidi,” alieleza shahidi huyo wakati akisoma maelezo ya Sophia.

Aliendelea kueleza kuwa Alphonce alielekea Kijichi, na alipofika nyumbani kwa Beatrice,

Dada yake huyo alishtuka kuona Alphonce akiwa amewasili usiku bila taarifa yoyote.

“Beatrice hakujua lolote kuhusu kilichokuwa kinaendelea. Alimuuliza mama yake kwa mshangao, ‘kwa nini Alphonce amekuja usiku nyumbani? Naomba aondoke, simtaki hapa,’” aliendelea kusimulia shahidi.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, “wakiwa ndani, wakati mtoto wa Beatrice akiwa amelala kwenye kochi, Alphonce alijaribu kumshambulia Beatrice.

“Hata hivyo, Beatrice alionyesha upinzani mkali na walizozana kwa muda. Baadaye, Alphonce alifanikiwa kumshika mikono Beatrice kutoka nyuma, lakini bado aliendelea kumpinga.

“Sophia, alipobaini Beatrice alikuwa karibu kumzidi nguvu Alphonce, alichukua kisu kilichokuwa mezani na kumchoma Beatrice kwenye titi la kushoto,” alidai shahidi huyo alipokuwa akisoma maelezo ya Sophia.”

Shahidi alieleza kuwa baada ya kuchomwa kisu, Beatrice alianguka chini, akaishiwa nguvu, na baadaye alianza kukoroma huku damu nyingi zikitoka mwilini mwake, hadi alipopoteza maisha akiwa ndani ya nyumba hiyo.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Sophia na Alphonce walipohojiwa walikiri kwamba lengo lao halikuwa kumuua, bali kumpiga tu, ili kumzuia kwenda kutoa ushahidi mahakamani.

Hata hivyo, baada ya kifo cha Beatrice, walibaki wakitafakari namna ya kuondoa mwili wake.

Kwa mujibu wa shahidi, walianza kwa kusafisha nyumba, ambayo ilijaa damu, kisha Alphonce alimfunga marehemu kwa shuka na kumviringisha katika mkeka wa kisasa.

Alidai kuwa baadaye walikubaliana kupeleka mwili huo Bagamoyo, ambapo Sophia alimuonyesha Alphonce mahali funguo za gari ya Beatrice zilipokuwa zimehifadhiwa.

Kwa mujibu wa shahidi, Alphonce alichukua funguo hizo na kwenda kwenye gari la dada yake, aina ya Toyota Vanguard, lililokuwa limeegeshwa nje ya nyumba.

Aliliendesha hadi mlangoni na hapo ndipo walipoupakia mwili wa Beatrice ndani ya gari hilo.

Shahidi huyo, ambaye alitoa ushahidi wake kwa zaidi ya saa tatu, aliendelea kusoma maelezo ya onyo ya Sophia, kuwa wakati wa tukio hilo Beatrice alikuwa na mtoto mdogo wa kike aitwaye Megan mwenye umri wa miaka mitatu.

Sophia alichukua mtoto huyo na kumlaza kitandani, kisha akafunga mlango wa nyumba na geti, kabla ya kuanza safari ya kuelekea Bagamoyo, Alphonce akiendesha gari.

“Tulianza safari na kufika Bagamoyo, lakini kwa kuwa ilikuwa usiku wa giza totoro, sikufahamu vizuri eneo hilo.

“Tuligeuka kushoto kutoka barabara kuu iendayo Bagamoyo na kuingia mtaa wa vichochoroni. Alphonce alisimamisha gari, tukashusha mwili wa Beatrice na kuuacha kando ya barabara. Pia, tulitupa shuka zenye damu pamoja na ndoo ndogo iliyokuwa kwenye gari ya marehemu,” alieleza shahidi huyo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kutekeleza tukio hilo, Sophia alirudi Kijichi ambapo alikuta mjukuu wake bado amelala.

Alphonce alielekea nyumbani kwake Bunju, lakini asubuhi alirudi Kijichi kumchukua mtoto wa Beatrice. Ili kuficha ukweli kuhusu kilichotokea, waliamua kuwaambia ndugu na jamaa kuwa Beatrice alikuwa ameenda Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Shahidi alidai Sophia aliendelea kuishi nyumbani kwa Beatrice kwa muda, na baadaye, kwa kushawishiwa na Alphonce, aliuza baadhi ya samani na vifaa vya ndani ya marehemu na fedha zilizopatikana, Alphonce alizichukua kwa madai kuwa alikuwa anamtafutia mama yake chumba cha kupanga.

“Januari 2021, nikiwa bado ninaishi nyumbani kwa Beatrice, mimi na Alphonce tuliuza nyumba nyingine ya marehemu iliyoko Morogoro kwa Sh34 milioni. Hata hivyo, Alphonce alichukua fedha zote kwa madai kuwa atanunua nyumba mpya Dar es Salaam, jambo ambalo halijawahi kutimia hadi leo,” alieleza shahidi huyo akiendelea kusoma maelezo ya Sophia.

Katika maelezo hayo pia, Sophia alikiri kuwa mwanawe Alphonce amewahi kufungwa gerezani mara kadhaa kwa makosa ya utapeli, na kwamba tabia hiyo ilikuwa ikimkera sana dada yake Beatrice. Baadaye, Alphonce alimtafutia mama yake chumba cha kupanga eneo la Mbagala, huku yeye akiendelea kuishi na mtoto wa marehemu.

Alipoulizwa sababu ya kuchukua uamuzi huo wa kikatili, Sophia alikiri kuwa alimuua mwanawe kwa lengo la kumzuia asifike kutoa ushahidi dhidi yake katika kesi ya madai iliyofunguliwa na baba wa Beatrice.

“Kwa nilichokifanya, namuomba Mungu anisamehe, najuta sana,” alisema Sophia kwa mujibu wa ushahidi uliosomwa mahakamani na Koplo Nicholaus.

Kesi hiyo imepangwa kuendelea kusikilizwa Jumatatu, Mei 12, 2025, ambapo washtakiwa wamerejeshwa rumande.

Awali, shauri hilo liliitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi kufuatia kuwepo kwa kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi.

Uamuzi huo ulitokana na pingamizi lililotolewa na upande wa utetezi, wakitaka Mahakama isipokee maelezo ya onyo ya Sophia wakidai kuwa yalichukuliwa kinyume cha sheria na kwamba mshtakiwa aliteswa wakati wa kuhojiwa na Polisi.

Hata hivyo, Mahakama ilitupilia mbali pingamizi hilo na kupokea maelezo hayo kama kielelezo rasmi cha upande wa mashtaka (kielelezo namba tatu), ndipo shahidi huyo alipoyasoma mbele ya Mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *