
Wakati idadi ya laini za simu nchini ikifikia milioni 90.1 katika mwaka ulioishia Machi 2025, asilimia 24 pekee ya watu ndio wanaotumia simu janja.
Kuwapo kwa matumizi madogo ya simu janja yasiyoendana na kasi ya ukuaji wa matumizi ya mtandao kunatajwa kuacha watu wengi nyuma, jambo ambalo linapaswa kufanyiwa kazi.
Katika hilo wananchi wanataja kupunguzwa kwa bei ya simu za mkononi ndiyo njia pekee ambayo haitawaacha watu nyuma na kuwafanya waende sambamba na mabadiliko ya kasi ya teknolojia.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la usajili wa laini mfululizo katika vipindi tofauti vya robo mwaka ambapo kabla ya kufikia sasa zilikuwa milioni 76.66 katika mwaka ulioishia Juni 2024.
Baadaye laini hizo ziliongezeka hadi kufikia milioni 80.66 Septemba 2024 na milioni 86.84 katika robo ya mwaka iliyoishia Desemba 2024.
Hata hivyo, ukuaji huu wa usajili wa laini za simu katika kipindi cha miaka mitano umekua kutoka laini milioni 51.29 zilizokuwapo mwaka 2020.
Mpaka Machi, 2025 kampuni ya Vodacom ilikuwa ikiongoza kwa kutawala soko kwa asilimia 31.9, ikifuatiwa na Yas asilimia 28.5, Airtel asilimia 23, Halotel asilimia 14.7 na TTCL asilimia 1.9.
Wakati hili likishuhudiwa, kumeonekana kuwapo kwa kupungua kwa idadi ya dakika za huduma za sauti ndani ya nchi kwa asilimia 4.5 katika robo ya mwaka iliyoishia Machi 2025, ikilinganishwa na robo iliyoishia Desemba 2024.
Katika robo ya mwaka iliyoishia Desemba 2024, idadi ya dakika za huduma za sauti ilikuwa bilioni 42.5, ambazo zilishuka hadi kufikia dakika bilioni 40.6 kipindi kilichofuata.
Vivyo hivyo, idadi ya jumbe fupi za maandishi zilizotumwa zilipungua kwa asilimia 5 katika robo ya mwaka inayoishia Machi 2025 hadi kufikia bilioni 50 kutoka ujumbe bilioni 52.9 katika robo iliyoishia Desemba mwaka jana.
Akizungumzia suala hilo, Mtaalamu wa uchumi na biashara, Dk Donath Olomi anasema ukuaji huu huenda umechangiwa na tabia ya mtu kumiliki laini zaidi ya moja.
Au baadhi ya watu wanapopoteza simu wamekuwa na tabia ya kusajili laini mpya kabla ya kufuta usajili wa ile iliyokuwepo awali, jambo ambalo linazifanya kampuni za simu kushindwa kuifuta.
Hata hivyo, anasema kuwapo kwa ongezeko hili kutakuwa hakuna maana ikiwa watu wengi watakuwa wanatumia visimu vidogo, kwani wanakosa fursa ambazo wangeweza kuzipata.
“Watu wakiwa na simu kubwa wanapata taarifa zaidi, wakiwa na simu ndogo wanapoteza fursa ya kutumia uwezo wa teknolojia uliopo katika kufanya biashara na hata kufanya maamuzi mbalimbali, kwani mengi, ikiwemo ya kiuchumi na afya ni rahisi kupata mtandaoni,” anasema Dk Olomi.
Hata hivyo, alitamani kuona kunakuwapo udhibiti wa matumizi ya namba za simu wa uhakika, hasa kwa wale wanaotumia katika kufanya utapeli.
“Kwa nini bado mtu anaweza kufanya utapeli na asikamatwe, hiki kitu kinaharibu sana, watu wanasajili namba za simu si kwa namba zao, wengine wanatumia vibaya kufanya utapeli na wengine kutishia watu,” anasema.
Anasema anatamani ifike kipindi ambacho mtu akipigiwa simu awe anajua simu hiyo imetoka kwa nani na ikiwa simu iliibiwa basi laini hiyo iweze kuzuiwa ndani ya muda mfupi kufanya matukio yanayoweza kumuweka mtu katika hatari.
“Watu wanakosa raha na inaifanya kuwa si dhana ya kuaminika kufanya biashara,” anasema.
Kuhusu utapeli aliouzungumzia, takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kuwa Tanzania imepoteza Sh5.345 bilioni kutokana na udanganyifu mwaka 2024.
Matukio hayo yanahusishwa na udanganyifu wa uhamishaji wa fedha kupitia simu za mkononi, benki, na utoaji wa fedha kwa ATM, kama inavyoonyeshwa na ripoti mpya ya Takwimu za Uhalifu na Ajali za Barabarani.
Kiasi hicho kinaashiria ongezeko kutoka Sh5.067 bilioni zilizoripotiwa mwaka uliopita, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa mienendo ya udanganyifu wa kifedha kwa njia ya mtandao.
Taarifa hiyo inakuja wakati ambapo Watanzania wamekuwa wakilalamikia kutapeliwa kwa njia ya mitandao ya simu, wakitumiwa ujumbe wa maandishi wakitakiwa kutuma ‘fedha kwa namba hii’.
Jumbe hizo, ambazo hutumwa kupitia namba ya simu, huomba fedha kwa ajili ya kodi ya nyumba, ada ya watoto, gharama za matibabu ya mgonjwa aliyepo hospitalini, au michango ya harusi.
Ripoti hiyo ya Jeshi la Polisi Tanzania, iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imetaja sababu za ongezeko la matukio hayo kuwa ni hali ngumu ya kiuchumi, ukosefu wa ajira kwa vijana, utandawazi, na tamaa ya kupata fedha kwa njia za haraka na zisizo halali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matukio 4,091 ya uhalifu unaohusiana na udanganyifu wa kifedha yaliripotiwa mwaka jana, ikilinganishwa na matukio 3,731 mwaka uliotangulia.
Hali hiyo inaonyesha ongezeko la matukio 360, sawa na asilimia 9.6. Hata hivyo, ni Sh254.1 milioni pekee ndizo zilizopatikana katika kipindi hicho.
Mtaalamu mwingine wa Uchumi, Oscar Mkude anasema ongezeko linaloshuhudiwa ni ngumu kujua kama ni watumiaji wapya ndio wameongezeka au ni wale wale ambao sasa wanamiliki laini zaidi ya moja.
“Kwa sababu, kinachosaidia kuchagiza uchumi ni watu, siyo laini. Tunatumia laini kama kielelezo tu. Sasa kama watu ni walewale ila wameongeza laini hakuna kinachobadilika katika wastani, matumizi yatabaki kuwa yaleyale,” anasema Mkude.
“Hivyo basi, kwa mfano tukisema hawa ni watumiaji wapya, yaani ndio wanamiliki laini za simu kwa mara ya kwanza na tukidhani pia kuwa wana simu, iwe za kawaida au za kisasa, tunatarajia kuwa wataongeza matumizi yao kwa namna mbalimbali, kama vile kununua vocha, kufanya miamala ya pesa kwa njia ya simu au kununua data na kutumia intaneti,”
Anasema mambo haya yote yatachangia kwa njia chanya katika mzunguko wa kiuchumi na hivyo kutafsiriwa kama mchango fulani wa kiuchumi, ikizingatiwa kuwa mambo mengine yote yako sawa.
“Zaidi ya hayo, huenda ikaashiria ongezeko la ujumuishaji wa kifedha, uwiano na ufanikishaji wa huduma. Yote haya yanaelekea kuwa na mchango chanya kwa uchumi, hivyo basi, inaweza kuwa ni habari njema, lakini unahitaji kupunguza au kuchuja takwimu hizo ili kubaini ongezeko halisi na si idadi tu.”
Mtaalamu wa uchumi, Profesa Aurelia Kamuzora anasema ongezeko la laini hizi huenda zikachangiwa na hulka ya mtu mmoja kuwa na simu tofauti.
Hata hivyo, anasema hali hiyo inaisaidia Tanzania kuendana na mabadiliko ya teknolojia ambapo matumizi ya akili mnemba yanashika hatamu, hivyo uwepo wa vifaa kama simu janja itasaidia katika mabadiliko haya.
Anasema matumizi ya akili mnemba yana faida kwa nchi na katika maeneo ambayo wameanza kutumia uzalishaji na ufanisi umeongezeka. “Tunapokuwa na vifaa inamaanisha kuwa tunakwenda kukua kidijitali zaidi,” anasema Profesa Kamuzora.
Anasema pia ongezeko hilo linasaidia katika mabadiliko ya tamaduni, huku akitolea mfano wakati wao wanazaliwa walikuwa hawatumii simu za mkononi, lakini sasa ni kawaida watu kuzitumia.
“Hii itakwenda kurahisisha mambo mengi, ikiwemo upatikanaji wa huduma mbalimbali, ikiwemo uwezeshaji watu katika matatizo mbalimbali. Pia inasaidia utunzaji wa fedha kwa kutumia simu kwa urahisi, tofauti na zamani,” anasema Profesa Kamuzora.
Anasema hali hii itasaidia kuongezeka kwa uchumi kwa sababu ya kuwapo kwa ubadilishanaji wa fedha, ikiwemo kununua bidhaa mbalimbali, malipo ya huduma, ikiwemo zile za afya.
“Zamani kulikuwa na shida sana katika kupata huduma, mtu anakuambia nipe shilingi mbili nikusaidie kwa haraka, lakini sasa kila kitu ni rahisi, mtu akiwa na simu unanunua tiketi na unasafiri,” anasema Profesa Kamuzora.
Hali hii inafanya hata biashara mbalimbali kupata faida ya kile wanachokifanya kutokana na kupunguza mwingiliano wa watu katika huduma za malipo ya huduma mbalimbali.
Lakini ili dhana hii ifanikiwe kwa asilimia 100, Profesa Kamuzora anashauri kufanyika utafiti wa kusoma vipato vya watu ili kujua uwezo wao wa kumudu simu janja.
“Na baada ya hiyo tunaweza kuangalia mbinu zinazoweza kutumika kama ni kuingia mkataba na kampuni za simu ambazo zinaweza kuwa zinatoa mikopo sawa, lakini wao pia waelezwe wanavyoweza kunufaika na kile wanachokifanya kama ambavyo nchi ya China inafanya,” anasema.