
Dodoma. Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gelard Mweli ameeleza faida nne muhimu zilizopatikana mara baada ya Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT) kupata cheti cha Ithibati ya Ubora wa Kimataifa kutoka Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO) kwa huduma ya uchunguzi wa udongo na mimea.
Mweli ameyasema hayo leo, Ijumaa Mei 9, 2025, wakati alipokuwa akipokea cheti hicho kwa niaba ya maabara hiyo.
Amesema kuwa maabara hiyo inakuwa miongoni mwa taasisi 108 nchini ambazo zimepata cheti cha ISO, na faida zake ni kubwa kwa wakulima na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Mweli amezitaja faida hizo ni kupunguza matumizi ya mbolea, kuongeza uzalishaji wa mazao, kuongeza ushindani katika soko la kimataifa na kusaidia katika utekelezaji wa sera na mikakati ya kitaifa.
Amesema maabara hiyo inakuwa miongoni mwa taasisi 108 nchini ambazo tayari zimeshapata cheti cha Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO). Mweli aliongeza kuwa faida kubwa kwa wakulima ni kwamba sasa wataweza kupata ushauri sahihi kuhusu matumizi ya mbolea kulingana na hali ya udongo, hivyo kuboresha matumizi yenye tija na kulinda mazingira.
Mweli amesema maabara hiyo inakuwa ni miongoni mwa taasisi 108 nchini ambazo zimeshapata cheti cha Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO).
Amesema faida za maabara kwa wakulima nchini ni wataweza sasa kupata ushauri sahihi wa mbolea kulingana na jinsi ya udongo na hivyo kuwa na matumizi yenye tija na yanayolinda mazingira.
“Pia, itapunguza gharama za matumizi ya mbolea kwa kutumia kiwango kinachotakiwa kwa mmea na itakuwa sehemu ya kurahisisha utekelezaji wa sera na mikakati mbalimbali kwa kilimo endelevu,” amesema.
Ametaja faida nyingine ni kuongeza ushindani wa mazao yanayozalishwa nchini katika soko la kimataifa kutokana na usahihi wa matokeo.
Kwa upande wa jamii, Mweli amesema jamii itanufaika kwa kuwa na ongezeko la mazao ya chakula na biashara na hivyo kuwezesha upatikanaji wa chakula cha kutosha na kuongeza lishe bora na maisha bora kwa wananchi.
“Maendeleo ya kilimo ni nguzo ya uchumi wetu na hivyo tunapaswa kuelewa msingi wa maendeleo hayo ni utafiti wa kisayansi unaoaminika na kuzingatia viwango vya kimataifa,” amesema.
Amesema maabara hiyo ni pekee nchini ambayo inauwezo wa kutoa huduma za kiuchunguzi, uchambuzi wa udongo na mmea kwa viwango vinavyotambulika kimataifa.
“Hii ina maana wakulima wetu wa chai na mazao mengine kama parachichi, mahindi, maharage, mbogamboga na hata miti ya mbao sasa watapata huduma bora na sahihi itakayowezesha kuongeza tija ya uzalishaji,”amesema.
Amesema huduma za upimaji wa udongo, hazitaongeza uzalishaji wa chai na mazao mengine pekee bali zitaongeza mapato ya wakulima, ajira, zitalinda mazingira kwa matumizi sahihi ya mbolea pamoja na kusaidia katika matumizi bora ya ardhi ambayo ni dhamana kubwa ya Wizara ya Kilimo.
“Nitoe wito kwa Watanzania kujitokeza na kutumia huduma za maabara yetu hii. Tuanze kujenga mazoea ya kulima kilimo cha kisasa kwa kuzingatia matokeo yatokanayo na uchunguzi wa kimaabara,”amesema Mweli.
Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wakulima Wakubwa wa Chai (TAT), Jones Sikira amesema utafiti wote wa zao la chai ulikuwa ukifanyika nchini Kenya kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Amesema baada ya kuvunjika kwa jumuiya hiyo masuala ya utafiti yalirejea katika nchi husika na kuwa hiyo ililazimu baadhi ya wakulima kupeleka uchunguzi wa zao hilo nchini Kenya.
“Mbolea katika uzalishaji wa chai ina gharama kubwa na ni ya pili kwa gharama kutoka kwenye uchumaji kwenye chai, hivyo ukianza kuweka kwa mashaka kwa kutojua kiasi kinachotakiwa, unajikuta unaingia gharama kubwa,”amesema.
Amesema kupatikana kwa ithabati hiyo, kutawezesha udongo kupimwa nchini na hivyo kuepuka gharama na muda wa kupeleka nje ya nchi.
Kuanzia Desemba 2024 hadi Machi mwaka 2025, Tanzania imeingiza Sh50.25 bilioni kutokana na vibali vya kusafirisha chain je ya nchi vinavyotolewa na Bodi ya Chai Tanzania (TBT).
Pia, Tanzania inatajwa kuwa na wakulima wadogo 32,000 huku wananchi wengine waliopata ajira zisizo za moja kwa moja katika sekta hiyo wakitajwa kuwa zaidi ya milioni mbili.