
Dar es Salaam. Wakati wadau wa masuala ya afya wakipendekeza kujumuishwa huduma za uzazi wa mpango kwenye bima ya afya, Serikali imesema imeyapokea na yatafanyiwa kazi.
Serikali imesema ipo kwenye mchakato wa kubadili sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), hivyo pendekezo la kujumuishwa huduma za uzazi wa mpango kwenye bima ya afya imelipokea.
Mkurugenzi wa Sera, Tafiti na Ubunifu wa Wizara ya Afya, Tumainiel Macha amesema hayo leo Alhamisi Mei 8, 2025 akichangia mjadala wa Mwananchi X Space, uliojadili mada isemayo: “Nini maoni yako kuhusu mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)? Umeandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na NHIF.
Amesema tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ambayo itahusisha mahitaji yote ya binadamu, ikiwamo uzazi wa mpango.
“Marekebisho madogo ya sheria ya NHIF tunayoyafanya yatajumuisha uzazi wa mpango. Lakini suala la uzazi wa mpango na mambo mengine yote Rais Samia ameridhia iwe kwenye kifurushi kimoja ambacho wananchi watakipata,” amesema na kuongeza:
“Hivyo tukianza kutangaza hicho kitita ambacho wananchi watanufaika nacho, hayo masuala ya uzazi wa mpango, malaria na ugonjwa wa Ukimwi yatajumuishwa.”
Amesema ili mwananchi awe na uhakika wa afya yake ni lazima awe na bima ya afya, akieleza Serikali inaendelea kukamilisha kifurushi kuwasaidia wananchi wa madaraja yote kuwa na bima ya afya.
Akichangia mjadala huo, Mkurugenzi wa taasisi ya TMEPiD, Cuthbert Maendaenda amesema uchangiaji wa bima ya afya si sawa na kuweka fedha kwenye akaunti ya benki.
Amesema mfuko wa bima unamwezesha mtu kupata matibabu ya gharama kubwa zaidi ya kile alichochangia.
“Mtu anayechangia mfuko wa bima ya afya si kama mtu anayechangia benki, unaweza usitibiwe lakini mtoto wako au jirani yako akatibiwa kwa gharama kubwa kuliko kiasi alichoweka, ndiyo maana tunasema tunachangia na si kuweka,” amesema.
Akizungumzia uzazi wa mpango kujumuishwa kwenye bima, amesema lengo si kuweka masharti kandamizi.
Amesema yapo maradhi mengi yanazuilika endapo mama atatumia uzazi wa mpango, hivyo njia hiyo huimarisha afya ya mtoto na mama.
“Afya ya mama na mtoto ikizorota wataingia kwenye maradhi, watahangaika kwenda kutibiwa na hawana bima,” amesema.
Mdau wa masuala ya afya, Abigael Sitishio amesema NHIF utakapoanza kutoa huduma ya afya ya uzazi, vituo vya afya binafsi vitawahudumia wananchi.
“Pendekezo langu huduma ya uzazi wa mpango iwekwe kwenye bima kama haki ya msingi ambayo mwanamke anaweza kupata,” amesema.
Amesema NHIF inapaswa pia kufanya uchunguzi kuangalia ni namna gani uzazi wa mpango umepunguza vifo vya mama na mtoto na kumwezesha mwanamke kupanga maisha yake vizuri.
Mchambuzi wa Sera na Bajeti, James Mlali amesema NHIF ukiingiza uzazi wa mpango kwenye vifurushi vyake itapata faida kubwa.
Mlali amesema hatua hiyo itapunguza mzigo wa gharama ambazo inagharimia wateja wake.
“Ukiwa na mteja ambaye anabeba ujauzito kila baada ya miaka miwili na mwingine baada ya miaka mitatu, baada ya miaka sita yule mteja wa miaka mitatumitatu utakuwa umemhudumia mara mbili lakini huyu anayejifungua kila baada ya miaka miwili utamuhudumia zaidi,” amesema.
Mlali amesema uzazi wa mpango huimarisha afya ya mama na mtoto, akieleza bima za sekta binafsi ziliona faida hiyo baada ya kufanya utafiti kuangalia gharama walizotumia katika kuhudumia mama na mtoto.
Ofisa wa masuala ya bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (Tira), Ayoub Mremi amesema hadi sasa kuna kampuni saba zinazotoa bidhaa za huduma za uzazi wa mpango kwa matakwa ya mteja.
Amesema iwapo kuna uhitaji wa Watanzania kutaka fao hilo, ametoa rai kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuangalia na kutathmini kwa kiasi gani likiwekwa mfuko utaweza kugharimia.
“Kwa upande wangu naona fao hilo ni zuri na tuhakikishe kampuni na skimu zinazotoa huduma za bima zitoe bidhaa kulingana na mahitaji ya wananchi,” amesema.
Bima kwa wote
Katika hatua nyingine, Matamus Fungo, Meneja wa Huduma za Kisheria kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), amesema Watanzania wote wanapaswa kuwa na bima ya afya, ndiyo maana yakafanyika marekebisho ya sheria.
Amesema marekebisho hayo ya sheria yamegusa hadi ndugu wa damu wa mwanachama ili kuongeza sehemu ya wategemezi.
“Ilionekana ni muhimu kufanya marekebisho ili kuwahusisha wote. Ikumbukwe sheria yetu ilikuwa inahusisha baadhi ya watumishi wa umma lakini tukataka wote wahusike bila kujali wanatoka umma au binafsi.
“Sheria ilikuwa haitambui baadhi ya wategemezi, mfano ndugu wa damu wa mwanachama lakini kupitia marekebisho haya tukayapeleka bungeni ili na ndugu wa damu wa mwanachama watambuliwe,” amesema.
Mtaalamu wa masuala ya bima, Anselm Anslem amesema marekebisho ya Sheria ya NHIF ili kuendana na sheria ya bima kwa wote ni jambo la msingi.
Amesema muundo wa NHIF kwa sheria iliyopo ulitengenezwa kwa ajili ya watu waliopo katika sekta rasmi pekee.
“Mwaka jana au mwaka juzi kulikuwa na changamoto ya NHIF kushindwa kuhimili mahitaji, hapo ulikuwa unahudumia watu wachache. Sasa unakwenda kuhudumia wengi zaidi, maana yake Watanzania wengi ndio watapata changamoto,” amesema.
Amesema mabadiliko ya kisheria ni lazima yazingatiwe, ikiwamo namna mfuko unavyoweka mafao katika utaratibu unaoeleweka kwenye utoaji wa huduma.
“Mfuko una makundi mawili ambayo yanachangia, wapo waajiriwa na mashirika binafsi, sasa tunakwenda kuongeza kundi lingine ni lazima tutafute mbinu ya kuwaweka katika eneo moja, hivyo ni muhimu kuhakikisha mfuko unasawazisha matumizi kwa manufaa ya uhai wake,” amesema
Mtaalamu wa masuala ya bima ya afya, Yusuph Mohamed amesema muswada wa sheria ya bima ya afya kwa wote una faida kwa wananchi.
Amesema muswada huo umelenga kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo wa kulipia gharama za matibabu.
”Ile kadi ya bima ambayo utachukua utalipa gharama kulingana na utaratibu uliowekwa, hivyo mimi naona bima ni nzuri na inalenga kumsaidia mwananchi wa kipato cha chini,” amesema.
Yusuph amesema kuna watu wanahoji wanapokata bima na endapo hajaugua hufikiri watarejeshewa fedha zao jambo ambalo si sahihi na wanapaswa kufahamu fedha hazirejeshwi.
Amesema mtu anapokuwa na bima hapaswi kusubiri kuumwa bali anachotakiwa ni kwenda kupima afya yake na si kusubiri kuumwa.
“Ni vizuri watu kupima afya zao, unaposubiri hadi uumwe unaingia kwenye hatari kubwa ya kupoteza uhai, sasa ukiangalia afya yake mapema tatizo litatibiwa mapema kabla ya tatizo kuanza mwilini,” amesema.
Mbunge wa Momba, Condester Sichalwe ameiomba Serikali wakati inaendelea na mchakato wa bima ya afya kwa wote irejeshe baadhi ya huduma zilizotolewa kwenye kifurushi.
Amesema wakati maboresho ya bima kwa afya kwa wote yanayosubiri kanuni kutoka kwa waziri mwenye dhamana, huduma zinapaswa kurejea ili kuepusha kulipia pesa nyingi.
“Wametoa vitu vingi kwenye vile vifurushi kiasi kwamba mtu anapokwenda kupata huduma anajikuta analipia pesa nyingi pamoja na kwamba amechangia,” amesema.
Kuhusu uzazi wa mpango kwenye bima za afya amesema ni muhimu kwa kuwa uzazi ni msingi wa jamii, hivyo unahitaji maandalizi mazuri na miongoni mwa maandalizi hayo ni kuwepo kwenye kifurushi.
Akichokoza mada hiyo, mwandishi mwandamizi wa habari za afya wa Mwananchi, Herieth Makwetta amesema lengo la Serikali kuwasilisha muswada wa marekebisho ya sheria ya NHIF ilikuwa kuoanisha shughuli za mfuko na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ambao tayari ilishakuwa sheria baada ya kusainiwa na Rais Samia, baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Desemba 1, 2023.
Saini ya Rais katika sheria hiyo, inaipa kazi Wizara ya Afya kuanza utungaji wa kanuni kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake, ambayo itawezesha kila Mtanzania kupata huduma za afya pasipo na kikwazo cha kiuchumi.