Berkane yatuma mashushushu Dar kuisoma Simba

Mambo yameanza kuchangamka baada ya RS Berkane ya Morocco itakayocheza na Simba katika mechi mbili za fainali za Kombe la Shirikisho Afrika kudaiwa kutuma watu wanne ili kuja kuwasoma Wekundu ikila viporo vya Ligi Kuu Bara, ambapo leo jioni itaumana na Pamba Jiji Uwanja wa KMC.

Simba itaanzia ugenini kuvaana na Berkane Mei 17 kabla ya kurudiana nao Kwa Mkapa Mei 25 kombe likiwa uwanjani, huku taarifa zikisema tayari Wamorocco wametuma mashushushu wanne ili kuipeleleza vya kutosha Simba katika mechi za ligi kabla ya kuwasubiri kwa fainali ya kwanza ugenini.

Simba imetinga fainali kwa kuing’oa Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 wakati wapinzani wao waliitoa CS Constantine ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 na katika kuhakikisha wanaisoma kwa undani Berkane imetuma mashushushu hao wanne akiwemo mtathmini wa mechi kupitia video (video analyst).

Hii inaweza isiwe taarifa nzuri kwa Simba, kuwa ikae chonjo leo itakapovaana na Pamba Jiji katika mechi ya Ligi Kuu kwani ufundi wowote itakaoufanya KMC itawapa akili mashushushu hao ambao hata hivyo hawakutajwa majina.

Mbali na video analyst wengine, waliokuja kuisoma Simba ni pamoja na mmoja ni kiongozi wa klabu hiyo iliyopo Ligi Kuu ya Morocco (Batola Pro) na kigogo mmoja wa Wizara ya Michezo wa Morocco.

“Wawili wataondoka baada ya siku chache, lakini wengine wawili wataondoka Mei 12, baada ya mechi dhidi ya KMC,” chanzo makini kiliidokeza Mwananchi na kuongeza;

“Wanataka kuisoma Simba hadi katika mechi dhidi ya KMC kabla ya kwenda kukutana na Waarabu Mei 17, lakini watatumia nafasi hiyo kuweka sawa kabla ya kikosi kuja nchini kwa fainali ya Mei 25.”

Simba leo inashuka uwanjani kuvaana na Pamba Jiji ikiwa ni baada ya kutoka kushinda dhidi ya Mashujaa na JKT Tanzania, ikiwa ni viporo ilivyonayo wakati ikiwajibika katika michuano ya CAF.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *