Dar es Salaam. Staa wa Konde Music Worldwide, Harmonize amerudiana na aliyekuwa mpenzi wake, Kajala Masanja ambaye tangu mwaka 2021 amekuwa akiingia na kutoka katika maisha ya mwanamuziki huyo mwenye albamu tano.
Hilo limemfanya Kajala kuwa na rekodi tatu za kipekee kwa Harmonize ukilinganisha na warembo wengine ambao wamewahi kuwa na mwimbaji huyo anayefanya vizuri na kibao chake kipya, Furaha (2025).

Harmonize ambaye alitua kwa muigizaji huyo baada ya kuachana na mkewe Sarah Michelotti kutokea Italia, hakuna uhusiano wake ambao umewahi kuwa na drama nyingi mtandaoni kama huu na Kajala.
Ni Kajala aliyetamba na filamu kama Kijiji Cha Tambua Haki (2012) akiwa na Steven Kanumba, licha ya kuipa kisogo tasnia hiyo bado anagonga vichwa vya habari kupitia uhusiano wake na Harmonize ambapo ana rekodi hizi tatu zifuatazo.
1. Kurudiana sio shida
Tangu ametoka kimuziki na wimbo wake, Aiyola (2015), Harmonize amekuwa na uhusiano na warembo kama Jacqueline Wolper, Sarah Michelotti, Briana na Poshy Queen lakini Kajala ndiye mwenye rekodi ya kuachana na kurudiana naye mara nyingi.

Uhusiano wao ulianza kuonekana hadharani Februari 2021 ila kufika Aprili ikiwa na mwezi mmoja tu wa penzi lao, wakaburuzana Polisi ambapo mmoja wapo alikuwa akimtuhumu mwenzake kusambaza picha zake chafu mtandaoni na ndio ikawa sababu ya kuachana.
Akiwa anaendelea na ziara yake ya muziki Marekani hapo Novemba 2021, Harminize akamtambulisha Briana kutokea Australia kama mpenzi wake mpya ila walikuja kuachana baada ya miezi mitano, yaani Machi 2022.
Baada ya hapo Harmonize alianza kutumia mitandao kumbembeleza Kajala warudiane na kweli alifanikiwa hadi kuja kumvisha pete ya uchumba, tukio kubwa lilofanyika Juni 25, 2022 katika hoteli ya Serena, na baadaye bibie alipewa zawadi ya gari.
Hata hivyo, bado hilo halikutosha kuwafanya waendelee kuwa pamoja adaima!, waliachana na kufikia Januari 2024 Harmonize akaweka wazi uhusiano wake na Poshy Queen ambaye walikuja kubwagana Agosti, na sasa Harmonize karejea kwa Kajala wake.

2. Mpenzi kawa Meneja
Hadi sasa Kajala ndiye mpenzi pekee wa Harmonize ambaye alimpa nafasi ya kuwa meneja wake kimuziki kwa kipindi fulani ingawa hatua ilizua minong’ono iwapo kweli anaweza kuitendea haki nafasi hiyo kutokana na uzoefu wake.
Lakini katika kipindi ambacho akiwa meneja, ndipo Cheed, Killy na Anjella mikataba yao ilivunjwa na Konde Music kwa sababu mbalimbali na kuifanya lebo hiyo kusalia na msanii mmoja kutoka saba waliokuwepo awali.
Anjella ambaye alikuwa msanii pekee wa kike Konde Music, kupitia video ya wimbo wake, Blessing (2023), ametumia lugha ya sanaa kueleza kuwa Kajala alikuwa kikwazo kwa yeye kupata huduma muhimu ndani ya lebo.
Wengine wanaona ni kama Harmonize alikurupuka kumpa Kajala nafasi hiyo muhimu ya kiutendaji, walienda mbali zaidi na kusema amemuiga staa wa Nigeria, Wizkid ambaye mpenzi wake na mama watoto wake Jada P ndiye meneja wake.
Lakini akasahau kuwa huyu sio kama Kajala, Jada P kabla ya kuwa meneja wa Wizkid, alishafanya kazi nyinyi sawa na hiyo hapo awali akisimamia chapa za mastaa kama Chris Brown, Pia Mia na Didier Drogba wakati akiichezea Chelsea pale Ligi Kuu England (EPL).
3. Katungiwa Nyimbo
Katika panda shuka zake na Kajala, Harmonize ametumia sana muziki wake kuweka mambo sawa baina yao na hata kueleza hisia zake pale alipoumizwa au kufurahishwa na mwenzake kwa lolote lile, na nyimbo hizo zimekuwa zikizingatiwa sana.

Basi hilo limemfanya Kajala kuwa mwanamke ambaye amelengwa sana na nyimbo nyingi za Harmonize, kwa mfano kipindi penzi lao limepamba moto, alimwimbia nyimbo kama Deka (2022) na Nitaubeba (2022) ambao katika video yake ametokea pia.
Vilevile pindi Kajala alipomuumiza Harmonize na kuachana naye, basi Konde Boy hakusita kuingia studio na kutoa nyimbo kama Mtaje (2021), Vibaya (2021) na You (2022).
“Anayelenga kwa rula siku zote ndiye apataye, mwambieni mwanangu Paula mimi nampenda mamae,” anaimba Harmonize katika wimbo wake ‘Mtaje’ kutoka katika albamu yake ya pili, High School (2021).
Na sasa wamerudiana, bila shaka tutarajie muziki mwingine kutoka kwa Harmonize akimwimbia Kajala Masanja, mama wa Paula ambaye ni mpenzi wa staa wa Bongofleva, Marioo aliyetoka na kibao chake, Dar Kugumu (2018) kilichotengenezwa na Abbah.