
Nairobi. Polisi nchini Kenya wamesema wamefanikiwa kupata bastola inayoshukiwa kutumika katika mauaji ya Mbunge wa Kasipul, Charles Ong’ondo Were, kufuatia msako mkali uliofanyika katika eneo la Chokaa, Nairobi.
Mbunge Were aliuawa Aprili 30, 2025 kwa kupigwa risasi na mtu aliyekuwa kwenye pikipiki katika Barabara ya Ngong Jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa tovuti ya KBC, gari ya mbunge huyo aina ya Toyota Crown ilisimama baada ya taa nyekundu za barabarani kuwaka kabla ya mtu huyo kushuka kwenye pikipiki kisha kusogelea gari, kutoa bastola na kufyatua risasi.
Baada ya kufanya hivyo mtu huyo alirudi haraka kwenye pikipiki ambayo dereva wake alikuwa akimsubiri kisha wakatokomea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 8, 2025 Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja amesema ripoti ya uchunguzi wa risasi imeonesha wazi kuwa bastola ya aina ya Sarsilmaz, iliyopatikana kwa mshukiwa ndiyo iliyotumika kumuua mbunge Were.
Bastola hiyo imepatikana mikononi mwa washukiwa wawili waliokamatwa wakiwa na silaha mbili aina ya Retay Falcon na Sarsilmaz, pamoja na begi na jozi ya viatu vinavyolingana na maelezo ya mavazi ya mshukiwa aliyeripotiwa kuwa katika eneo la tukio.
“Ripoti ya uchunguzi wa risasi imebaini kuwa bastola aina ya Sarsilmaz inahusishwa moja kwa moja na risasi zilizomuua mbunge Were,” alisema Kanja aliponukuliwa na gazeti la Taifa Leo.
Aidha, uchunguzi wa mwili wa mbunge huyo uliofanywa Mei 2, na Mpasuaji Mkuu wa Serikali, Dk Johansen Oduor, ulibaini kuwa Mbunge Were alipigwa risasi tano upande wa kushoto wa mwili wake.
Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeripoti kwamba Edwin Odhiambo, anayejulikana pia kama Abdul Rashid, pamoja na Dennis Munyasi walikamatwa Jumatano, na kuwaongoza maofisa hadi nyumbani kwa Odhiambo ambako silaha hizo zilipatikana.
Wakati huohuo, washukiwa wanne waliohusishwa moja kwa moja na tukio hilo wanashikiliwa na polisi huku wawili wengine pia walikamatwa Jumatano na kufanya jumla ya washukiwa walioko kizuizini kufikia 10.
Katika hatua nyingine polisi pia wanachunguza simu aliyopigiwa msaidizi wa mbunge Were siku aliyouawa. Msaidizi aliyekuwa katika majengo ya Bunge wakati huo, alizungumza na mpigaji simu kwa muda wa dakika moja na sekunde 10.
Taarifa zinadai kwamba ingawa hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa mpigaji huyo kuzungumza na msaidizi wa Mbunge Were, siku mbili kabla ya tukio, msaidizi huyo alipokea simu kutoka kwa namba hiyohiyo.
Wachunguzi wanaamini kwamba simu hiyo iliyopigwa saa tano tu kabla ya mbunge kupigwa risasi, inaweza kusaidia kufichua siri ya mauaji hayo.
Taifa Leo imesema kwa mujibu wa vyanzo vyake namba hiyo ilisajiliwa siku tatu tu kabla ya mbunge kuuawa na ilimpigia msaidizi huyo wa mbunge.
Chanzo hicho kilisema kwamba uchunguzi zaidi wa laini hiyo ulibaini kuwa ilisajiliwa kwa jina la mwanamke ambaye, wapelelezi walibaini, alishafariki na kitambulisho chake kilitumiwa kusajili laini hiyo.