
Dodoma. Serikali iko mbioni kukamilisha mchakato wa kuanzisha baraza la afya ya akili na kwa sasa wanakamilisha vitu vichache.
Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 7, 2025 ambapo amesema awali walikuwa na ahadi ya kuanzisha baraza hilo Mei mwaka huu, lakini kuna mambo hayajawekwa sawa.
Dk Mollel amesema hayo alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu ambaye ameuliza kuhusu ahadi ya Serikali ya kuanzisha baraza hilo ifikapo Mei mwaka huu imefikia wapi.
Katika swali la Msingi Msambatavangu ameuliza lini NHIF itajumuisha huduma za afya ya akili kwenye vifurushi vya bima ya afya.
Dk Mollel amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa baraza hilo ambalo litasaidia katika masuala mazima ya afya ya akili.
Amesema huduma za matibabu ya afya ya akili, ushauri nasaha, na huduma nyingine za kibingwa ikiwemo huduma za utengamao, ni baadhi ya zilizoorodheshwa kama muhimu za afya kwenye mwongozo wa matibabu (Standard Treatment Guideline – STG).
“Mwongozo huo hutumika kama kigezo kikuu cha huduma za msingi zinazolipiwa na Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF),” amesema Dk Mollel.
Amesema katika utoaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wa akili, mfuko wa bima (NHIF) hugharamia dawa zote kwa kuzingatia aina ya dawa na ngazi ya huduma kwa mujibu wa Mwongozo wa Matibabu (STG).
Akijibu swali la kama ni sahihi kwa watu wanaotaka kujinyonga kufungwa kamba na kupelekwa hospitalini, amesema yako mambo mengi ambayo husababisha hali hiyo kutokea hivyo akaomba vyombo vingine viachwe kufanya uchunguzi.
Ripoti ya CAG
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2022/2023 ilibaini upungufu katika maeneo 12 ya utoaji huduma kwa jamii, ikiwamo ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya afya ya akili.
Hayo yamebainishwa na CAG Machi 2024 katika ripoti ya ukaguzi wa ufanisi kuhusu upatikanaji wa huduma za afya ya akili.
“Wagonjwa wanaongezeka kila mwaka na vifo pia. Vituo vingi havipati huduma za utengamo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa kupona. Kati ya mikoa 28, ni mitano pekee ndiyo ina vituo vya utengamo vya huduma za afya ya akili,” ilieleza ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa CAG, kuna ongezeko la idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na matatizo ya akili kulingana na utendaji wa kila mwaka wa Wizara ya Afya.
“Mwaka 2022 iliripotiwa katika Hospitali ya Taifa ya Akili ya Mirembe kulikuwa na ongezeko la idadi ya wagonjwa waliopatiwa matibabu ya magonjwa ya akili kutoka kwa wagonjwa 3,472 mwaka 2019 hadi 5,060 mwaka 2022, sawa na asilimia 31 ya wagonjwa,” inaeleza ripoti ya CAG.
Hali ya afya ya akili mwaka 2020 inakadiria mzigo wa maradhi ya akili umechangia kiwango cha vifo vya kujinyonga cha asilimia 8.15 kwa kila watu 100,000.
Vivyo hivyo, mwaka 2022 ripoti ya wizara hiyo ilikadiria mzigo wa maradhi ya akili umepanda kutoka wagonjwa 386,358 hadi 2,102,726 kuanzia mwaka 2012 hadi 2021 mtawalia, ambayo imeongezeka kwa asilimia 82.
Matokeo ya ukaguzi uliofanywa na CAG yanaonyesha upungufu katika utoaji wa huduma za afya ya akili katika jamii, miongoni mwa hayo ni kukosekana kwa sera ya afya ya akili.