Arteta: Tupo Hapa Kuandika Historia

Paris, Ufaransa. Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema kikosi chake kimejiandaa vizuri kwa mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG), licha ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani kwa bao 1-0.

Arsenal watashuka dimbani leo Jumatano Mei 7, saa 4 usiku kwenye Uwanja wa Parc des Princes, wakiwa na matumaini ya kufuzu kwenye fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006.

Arteta amesema licha ya kipigo cha mwisho wa wiki dhidi ya Bournemouth kwenye Ligi Kuu ya England, wachezaji wake wapo tayari kwa vita ya kusaka tiketi ya fainali.

“Tuko na lengo moja tu, kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa. Hili ni tukio kubwa sana. Tupo hapa kuandika historia,” amesema Arteta.

Arteta ameongeza kuwa kikosi chake kimetambua mapungufu ya mchezo wa awali na kinajua nini kinapaswa kufanywa ili kupata ushindi.

“Kuna tofauti ndogo sana kati ya timu hizi mbili. Nafasi ipo. Hii ni fursa ya kuthibitisha tunachostahili na kufuzu,” amesema Mikel Arteta.

Katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa Emirates, PSG walifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 kupitia kwa Ousmane Dembele ambaye alifunga katika dakika za mwanzoni mwa mchezo. Hata hivyo, kiungo wa Arsenal, Declan Rice amesema mabadiliko ya kimkakati yaliyofanywa na kocha, Mikel Arteta yamewapa matumaini makubwa ya kupindua matokeo Jijini Paris.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa England aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi katika mikikimikiki dhidi ya Real Madrid kwenye hatua ya robo fainali, amesema kikosi hicho kinaamini kinaweza kupata matokeo mazuri dhidi ya PSG.

“Tunaamini tunaweza kufanya jambo kubwa kwa klabu yetu. Tupo tayari kwa mchezo, kila mchezaji yupo tayari kupambana kuhakikisha tunaenda fainali,” amesema Declan Rice.

Arsenal sasa wanalazimika kushinda kwa tofauti ya mabao ili kufuzu moja kwa moja au angalau kusawazisha na kulazimisha dakika za nyongeza. Mshindi wa jumla atakutana na Inter Milan katika fainali itakayochezwa kwenye Uwanja wa Allianz Arena, Ujerumani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *