Dar es Salaam. Uzembe wa madereva wa vyombo vya moto nchini umetajwa kuwa sababu iliyobeba asilimia 44.1 ya ajali zote zilizotokea mwaka 2024, hali iliyochangia kuongezeka kwa idadi ya waliopoteza maisha.
Wakati wao wakinyoshewa kidole, madereva wamesema hawapaswi kulaumiwa moja kwa moja, kwani hadi ajali inapotokea huwa kuna sehemu tatu zinazosababisha, ikiwamo upande wa dereva mwenyewe na chombo husika.
Pia, madereva hao wamenyoshea kidole miundombinu ya barabara iliyopo, huku wakitaka maboresho kufanyika.
Hilo limesemwa wakati takwimu za ajali za barabarani zilizotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania zikionyesha kuwa idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na ajali mwaka 2024 imeongezeka hadi kufikia watu 1,715 kutoka watu 1,647 waliokuwapo mwaka uliotangulia.
Ongezeko hilo, kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni, linatokana na ongezeko la ajali zilizotokea, ambapo kubwa zilifikia 1,735 na matukio madogo yalikuwa 3,104,501, ikilinganishwa na matukio makubwa 1,733 na madogo 3,170,073 ya mwaka 2023.
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadwu), Ally Kimaro, amesema hakuna mtu anayependa ajali kwa sababu huleta matatizo inapotokea.
Amesema badala ya kunyooshea vidole madereva, watu wanapaswa kutambua kuwa hadi ajali inapotokea maeneo matatu huangaliwa, ikiwemo miundombinu, chombo chenyewe na dereva.
“Unaposikia chombo kimesababisha ajali, kuna mengi huangaliwa kitaalamu. Barabara nayo inaweza kuchangia mazingira ya ajali, lakini anatupiwa lawama dereva kuwa ndiye msababishaji bila kujali kilichotokea. Tusimpe asilimia 90 ya lawama,” amesema.

Amesema moja ya njia zinazoweza kukomesha suala hilo ni kuboresha maisha ya madereva na kuwashirikisha katika kanuni zinazotungwa na mamlaka mbalimbali, ili watambue kinachoendelea badala ya kukutana na baadhi ya vitu ghafla, ikiwamo faini barabarani.
Wakati Kimaro akisema hayo, mmoja wa madereva wa mabasi ambaye hakutaka kutajwa jina, amesema Serikali inapaswa kuangalia upya suala la uboreshaji wa miundombinu kabla ya kuwanyooshea wao kidole.
“Umewahi kwenda Mtwara? Umeona ile barabara ilivyo mbaya, ilivyo finyu? Mnatulaumu sawa, lakini nini mmefanya kwetu? Boresha kwanza kwenu ndipo mtupe lawama,” amesema.
Amesema si barabara hiyo ya Kusini pekee inayohitaji maboresho, bali hata za mikoa mingine hali yake hairidhishi na zinahitaji hatua za haraka.
Hatua kwa madereva
Katika kukabiliana na hali hiyo, Jeshi la Polisi katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024 lilifungia leseni za madereva 713 baada ya kubainika kuwa ni sugu kwa kufanya makosa hatarishi barabarani.
Pia madereva 1,204 walifikishwa mahakamani, madereva 2,973,982 walilipishwa faini za papo kwa papo, na madereva 128,774 walipewa onyo.

“Katika kipindi hicho, Kikosi cha Usalama Barabarani kilikamata jumla ya makosa madogo 3,104,501 ya usalama barabarani, ikilinganishwa na makosa 3,170,073 ya mwaka 2023. Upungufu huu unatokana na ongezeko la operesheni za usalama barabarani pamoja na usimamizi wa sheria na taratibu mbalimbali,” limesema Jeshi la Polisi.
Katika hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu, Habari na Mawasiliano kutoka Chama cha Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), Ramadhan Msangi, amesema ili kumaliza tatizo hilo ni vyema kuongeza usimamizi wa sheria zilizopo, ili kila mtu azitii.
Hilo linapaswa kwenda sambamba na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kwa watumiaji wa barabara, ili wawe tayari kuhakikisha kuwa sheria zinazotumika wanazifuata na kuzitekeleza ipasavyo.
“Kama barabara ni mbovu, dereva anajua kuwa barabara ni mbovu, kwa nini haendeshi vizuri? Kama gari ni mbovu, nani ameruhusu gari hiyo kuingia barabarani? Ni lazima mtumiaji wa barabara ajue kuwa barabara salama ni wajibu wake,” amesema Msangi.
Amesema wakati mwingine askari wa usalama barabarani wanaweza kuwa wachache, changamoto ambayo haipo kwa Tanzania peke yake, lakini wananchi wana wajibu wa kushirikiana na vyombo hivyo na wadau wengine kuibua changamoto zinazojitokeza barabarani.
Mikoa vinara
Kwa Tanzania Bara, mikoa iliyoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya makosa madogo ya usalama barabarani kwa mwaka 2024 ni Ilala (382,613), Kinondoni (329,951), Temeke (209,755), Morogoro (174,895) na Pwani (163,752).
Mikoa iliyokuwa na idadi ndogo ya makosa ya usalama barabarani ni Katavi (26,115), Tarime Rorya (29,497), Simiyu (30,848), Rufiji (32,059) na Mara (37,970).

Kwa upande wa Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi uliongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya makosa madogo ya usalama barabarani (19,565), ukifuatiwa na Kusini Unguja (12,365). Mikoa iliyokuwa na idadi ndogo ya makosa ilikuwa ni Kaskazini Pemba (1,912) na Kusini Pemba (4,565).
Hatua zilizochukuliwa
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, ili kukabiliana na hali hiyo wanaendelea kudhibiti mwendokasi kwa kutumia mifumo mbalimbali iliyopo ndani ya jeshi hilo.
Pia wanaendelea kuimarisha doria na ukaguzi barabarani, kutoa adhabu stahiki kwa wakosaji kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168.
“Pia tunaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kwa watumiaji wa barabara, kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wanaajiri watu wenye ujuzi, weledi na maadili ili kupunguza ajali zinazoepukika,” imesema taarifa ya Jeshi la Polisi.
Haya yote yanafanyika wakati ukaguzi wa mara kwa mara wa vyombo vya usafiri ukiendelea sambamba na kuwajengea uwezo askari wa usalama barabarani ili wafanye kazi kwa maadili na weledi, kwa kuwapatia vifaa vya kisasa.
Wizara ya Ujenzi
Wakati barabara zikinyooshewa kidole kuwa chanzo cha ajali, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alipowasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/2026, alisema kuwa mradi wa kujenga uwezo wa taasisi katika masuala ya usalama barabarani na mazingira umetengewa Sh55.81 milioni kwa ajili ya kuwezesha huduma za ukaguzi wa barabara.
Mradi huo utafanyika katika baadhi ya barabara za mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Manyara, Singida, Arusha na Tanga.
Pia, Ulega alisema kuwa kupitia fedha za Mfuko wa Barabara zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2025/26, Sh688.75 bilioni zimetengwa. Tanroads imetengewa Sh608.46 bilioni kwa ajili ya kazi za matengenezo na ukarabati wa barabara kuu na za mikoa.
“Kwa upande wa Wizara ya Ujenzi, imetengewa Sh67.6 bilioni kwa ajili ya kazi za ukarabati wa barabara za mikoa, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara, ukarabati na ununuzi wa vivuko, usalama barabarani pamoja na usimamizi na ufuatiliaji wa miradi hiyo,” alisema Ulega.
Baadhi ya wabunge, walipochangia bajeti hiyo, walilalamikia ubovu wa barabara pamoja na kukithiri kwa vilabu vya pombe kandokando ya barabara vinavyosababisha ajali.
Alichokisema Rais Samia
Desemba 31, 2024, akitoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuwa mwaka 2024 Tanzania ilikumbwa na jinamizi la ajali za barabarani, na aliitaka Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.
“Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kuwa kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715.
“Hii ni idadi kubwa. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa ni uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi – ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” alisema.
Naye Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, alipowasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025, alisema kuwa katika kipindi cha miaka mitano kati ya mwaka 2019 hadi Mei 2024 ajali za barabarani zilikuwa 10,093, ambapo vifo vilikuwa 7,639 na majeruhi 12,663.

“Idadi hii kubwa ya majeruhi na vifo vya watu kutokana na ajali, utadhani nchi iko kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Askari barabarani msiwe na huruma hata kidogo kwa wazembe wote wanaokiuka sheria, hata kama gari lina usajili wa namba za Serikali,” alisema Dk Mwigulu.
Ili kukomesha hilo, Dk Mwigulu alipendekeza kama sheria ni rafiki, makosa yote ya ajali barabarani yaondolewe kwenye ‘traffic case’ na yapelekwe kwenye makosa makubwa zaidi.
“Ikiwezekana huu uwe ni uuaji kama uuaji mwingine, kwa maana kwamba mtu anayekufyatulia risasi kwa makusudi ana uhakika wa kukujeruhi au kukuua na hata anayefanya uzembe na vyombo vya moto ana uhakika wa kukujeruhi au kukuua kwa makusudi kabisa,” alisema.