
Sudani imevunja uhusiano wa kidiplomasia na Falme za Kiarabu siku ya Jumanne, Mei 6, baada ya kuishutumu UAE kwa kuvipa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) silaha na ndege zisizo na rubani ambazo zimelenga Port Sudan, makao makuu ya muda ya serikali, kwa siku tatu zilizopita.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Dunia nzima imekuwa ikifuatilia kwa zaidi ya miaka miwili uhalifu wa uvamizi dhidi ya mamlaka ya Sudani, uadilifu wa ardhi yake na usalama wa raia wake, unaofanywa na Falme za Kiarabu kupitia afisa wake wa ndani,” Waziri wa Ulinzi Yassin Ibrahim amesema kwenye televisheni ya taifa. Ameishutumu Imarati kwa kusambaza “silaha za kimkakati za kisasa” kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF), wakiongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Daglo, ambaye aliingia katika uhasama na mkuu wa jeshi Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan mnamo mwezi Aprili 2023. “Wakati Falme za Kiarabu ulipoona kushindwa kwa kibaraka wao dhidi ya vikosi vyetu vya majeshi (…) waliongeza uungwaji mkono wao” Waziri wa Ulinzi ameshtumu. Sudani “itajibu uchokozi huu kwa njia zote muhimu ili kuhifadhi uhuru wa nchi,” ameongeza.
Tangazo hilo linakuja baada ya siku tatu za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika mji wa Port Sudan, makao makuu ya mud ya serikali. Mashambulizi haya, yanayohusishwa na jeshi la serikali kwa RSF, lakini ambayo hayakudaiwa na wanamgambo hao, yameharibu miundombinu ya kimkakati katika mji wa Port Sudan, bandari kuu ya Sudan. Uwanja wa ndege, kambi ya jeshi, kituo cha umeme na ghala za mafuta zilishambuliwa, kulingana na vyanzo vya habari ambavyo havikuripoti majeruhi yoyote.
Tangazo la serikali ya Sudani pia linakuja siku moja baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki, mahakama ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa, kutoa uamuzi dhidi ya Sudani inayoishutumu Abu Dhabi kwa kuhusika na mauaji ya halaiki kwa uungaji mkono wake kwa RSF. Kwa kukosa ndege za kivita, RSF inategemea ndege zisizo na rubani – kuanzia vilipuzi vilivyotengenezwa kienyeji hadi ndege za kisasa – kuendesha shughuli zao za anga, vifaa ambavyo serikali ya Sudani inashutumu Falme za Kiarabu kwa kuzisambaza. ICJ ilitangaza kuwa “hainauwezo” wa kutoa uamuzi katika kesi hiyo na Imarati, ambayo mara zote imekana kuhusika katika mzozo huo, imekaribisha uamuzi huu.