Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wameeleza hatari zilizopo kutunza watoto waliozaliwa pacha zaidi ya wawili, na changamoto wanazokutana nazo tangu kugawanyika kwa yai tumboni mwa mama, wakati na baada ya kuzaliwa.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na mgawanyo wa chakula na damu wawapo tumboni, kuzaliwa kabla ya wakati, uzito mdogo, changamoto za mfumo wa upumuaji baada ya kuzaliwa na nimonia.
Wataalamu hao wameibuka baada ya familia ya Halima Cissé ya jiji la Bamako nchini Mali, kusherehekea siku ya kuzaliwa ya watoto tisa waliozaliwa kwa mpigo, maarufu nonuplets, wakitimiza miaka minne tangu kuzaliwa kwao mwaka 2021.
Watoto hao, Mohammed VI, Oumar, Elhadji, Bah, Kadidia, Fatouma, Hawa, Adama, na Oumou wametimiza miaka minne Jumapili Mei 4, 2025 na kuendelea kuvuta hisia za watu duniani tangu walipozaliwa kwa upasuaji wa dharura katika Hospitali ya Ain Borja mjini Casablanca, Morocco.
Watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito wa kati ya gramu 500 na 1,000 kila mmoja wakati wa kuzaliwa, walihitaji huduma ya karibu ya kitabibu kwa miezi 19 kabla ya kurudi nyumbani kwao Mali.
Katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na ndugu, majirani na maofisa wa afya waliowasaidia wakati wa safari yao ya afya, walionekana wenye afya njema, wakicheza, kuimba na kufurahia michezo mbalimbali pamoja na dada yao mkubwa, Souda mwenye umri wa miaka sita.
Ikiumbukwe Shirika la Guinness World Records lilithibitisha kuwa ‘nonuplets’ hawa ndio kundi pekee la watoto tisa kuzaliwa kwa mpigo na kuishi, rekodi ambayo haijawahi kuwepo kabla katika historia ya matibabu ya uzazi.
Wakati hayo yakijiri Januari 2017, Beatrice na mumewe Julius Ngonyani Shauritanga, wakazi wa Mbezi Msakuzi walibarikiwa kupata watoto pacha wanne waliozaliwa kabla ya wakati (njiti) wiki ya 28 ya ujauzito na miezi miwili baadaye alimpoteza mtoto mmoja.
Changamoto
Mtaalamu bingwa na bobezi wa magonjwa ya watoto wachanga, Profesa Karim Manji anasema hapa nchini watoto wengi pacha hupoteza maisha kutokana na uangalizi.
“Mama anashtuka ana watoto wanne wakati wa kujifungua na yupo mbali na kituo cha afya na hakuhudhuria kliniki. Wanashindwa kupumua wanapungukiwa na oksijeni, mwingine alikaa juu akapata damu kuliko wenzake, wanaozaliwa na damu hafifu sana.

“Kinamama hawa wakibaini mapema wana pacha zaidi ya mmoja, wangepewa uangalizi na kuokoa watoto wote,”anasema.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama, Isaya Mhando anasema watoto pacha wanaozaliwa wengi ni nadra kupona na kukua kutokana na hatari kadhaa zinazowakabili tangu kuumbwa kwao.
Anasema wanaokuwa kwenye plasenta moja, huwa na changamoto hasa katika mishipa ya damu kutofautiana na hiyo husababisha mmoja kupata damu nyingi kuliko mwenzake na anayepata damu kidogo kuwa dhaifu.
Hilo anasema, huenda sambamba na ugawanywaji wa chakula na kwamba wanaopata kiasi cha kuwatosheleza huzaliwa na uzito angalau mkubwa kuliko yule aliyepata kidogo.
“Changamoto nyingine ni kuzaliwa kabla ya wakati, mama anakuwa na tumbo kubwa ile misuli ya mimba ni rahisi kutengeneza uchungu, kadri misuli inavyotanuka ndivyo inavyoleta uchungu.
“Huchangia kuzaliwa kabla ya wakati, kuna hatari nyingi za kuzaliwa kabla hawajakomaa mapafu, yanashindwa kutanuka na kusinyaa kwa kawaida.
“Kuna changamoto kwenye matumbo pengine wanakuwa hawakukomaa vizuri hii pia huambatana na mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye ubongo,” anasema Dk Mhando.
Anasema mtoto anayezaliwa kabla ya wakati, chini ya uzito wa kilo mbili huwa na uwezekano mkubwa wa kutokukua vizuri.
Anafafanua kuwa kwenye nchi maskini kwa maana ya miundombinu ya hospitali, huenda mama uwezo wake wa kifedha ni mdogo kushindwa kumtunza mtoto hasa vifaa kwa kuwa kuna njia nyingi za kuwatunza watoto hao, hatari ya kukua salama inaongezeka.
“Watoto hawa wanaugua sana nimonia kwa hiyo huwa kwenye hatari. Kwenye mifumo yetu hapa nchini kidogo wanajitahidi kuna vifaa vya kulelea watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati kwenye hospitali za mikoa na wilaya.
“Mama anatakiwa kuwa na maziwa ya kuwalisha hao wote, kunyonya na kula vyakula vya kutengeneza maziwa ya kutosha kukidhi mahitaji na afya za watoto wote,” anasema.
Dk Mhando anasema miaka miwili ya mwanzo wakitunzwa vizuri na kunyonya maziwa ya mama huwaimarisha zaidi na wakifikisha miaka mitano huwa na nguvu na hatari kwao hupungua.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Jane Muzo anasema baada ya kuzaliwa watoto hao huhitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa wataalamu na madaktari wa watoto mpaka wanapofikisha umri wa miaka mitano.
Dk Francis Furia, bingwa wa watoto na figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili anasema pacha wengi hukabiliwa na changamoto nyingi zaidi kama watazaliwa kabla viungo vyao havijakomaa, “kama viungo vyao havijakomaa vizuri, watahitaji uangalizi wa karibu zaidi.”
Sababu kuzaa pacha wengi
Mtandao wa kimataifa wa Verywell Family, unaeleza kuwa nusu ya mapacha duniani kote huzaliwa mapema, kabla ya majuma 36 na wengi wao huzaliwa na miezi minane.
Pacha watatu, wanne na kuendelea wana nafasi kubwa ya kuzaliwa mapema, wakati utaalamu wa kidaktari hauwezi kuzuia hilo huku katika hatua nyingine mama huwa katika hatari kiafya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wamesema kwa kawaida pacha wapo wa aina mbili kupitia mayai mawili au zaidi yanaporutubishwa kwa pamoja na mbegu za kiume wasiofanana ‘hapa huzaliwa wawili, watatu au wanne na kuendelea’ na wale wa yai moja linalorutubishwa kisha kugawanyika mara mbili ‘pacha wanaofanana’.
Dk Mhando amesema mgawanyiko unapotokea, mayai mawili tofauti kuchevushwa na kutengeneza kila mtoto na plasenta yake, mgawanyiko wa yai moja hutokea kwa kuchevushwa baada ya saa 72 kila mtoto anakuwa na mfuko wake, “Baada ya sikutisa mpaka 11 wote wanakuwa kwenye mfuko mmoja.”
Imezoeleka wanawake wengi hupata pacha wawili, lakini miaka ya hivi karibuni nchini Tanzania tumeshuhudia kinamama wakipata pacha watatu mpaka wanne.
Hapa daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Muhimbili, Nathanael Mtinangi anatoa ufafanuzi sababu za mama kujifungua watoto pacha zaidi ya wawili.
Dk Mtinangi anasema kuna sababu kuu mbili za mama kupata pacha, moja ikiwa ni kurithi yaani kuwa na vinasaba vya pacha ambapo mayai hupevuka kwa wakati mmoja kutoka pande zote mbili.
“Wapo wanawake ambao hutoa mayai mawilimawili, kwa kawaida kila mwezi hutakiwa kutoa yai moja, kushoto na mwezi ujao kulia, lakini ikiwa mama anatoa pande zote kama ilivyo kwa baadhi ya koo zinatoa kila pande au matatu na wakati mwingine mawili kila pande matokeo ni watoto pacha kulingana na mayai yanayopevushwa,” anasema.
Dk Mtinangi amesema aina ya pili ni wanawake ambao mayai yao hupevushwa na kugawanyika mara mbili na hao ikiwa litashuka moja atapata pacha wawili wanaofanana yaani wa mfuko mmoja, “akishusha pande zote mbili mayai ambayo yatagawanyika mara mbili atapata pacha wanne wanaofanana ambao walikaa wawili katika kila mfuko.”