
Serengeti. Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, amewaagiza wananchi wa Kijiji cha Nyatwali, kilichopo Wilaya ya Bunda, kuondoka mara moja katika maeneo waliyokuwa wakiishi baada ya kulipwa fidia na Serikali, ili kupisha ushoroba wa wanyamapori wanaopita kuelekea Ziwa Victoria kutafuta maji.
Akizungumza leo, Jumanne, Mei 6, 2025, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Urithi wa Dunia Afrika, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mugumu, Wilaya ya Serengeti, Mtambi amesema Serikali imeshalipa fidia ya Sh53 bilioni kwa wakazi wa kijiji hicho kwa ajili ya fidia, hatua inayowezesha kuanzishwa rasmi kwa ushoroba huo unaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Amesisitiza kuwa eneo hilo limeshatangazwa kuwa hifadhi rasmi kupitia Tangazo la Serikali (GN) Na. 269 la mwaka 1974, hivyo haliruhusiwi kuwa na makazi ya binadamu.
“Serikali imelipa fidia. Wananchi wa Nyatwali ambao wamelipwa wanapaswa waanze kuondoka mara moja, kupisha ushoroba huu wa wanyamapori. Kufanya hivyo kutasaidia kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyama, hasa tembo wanaokwenda Ziwa Victoria kutafuta maji,” amesema mkuu huyo wa mkoa.
Amesema wananchi wanaishi katika hali ya hofu kutokana na uvamizi wa mara kwa mara wa wanyamapori katika makazi yao, hali inayohatarisha usalama wa maisha na mali zao.
Amesema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema, “Majanga na Migogoro ni Tishio kwa Urithi wa Dunia”, hivyo amesisitiza kuwa hatua ya Serikali ya kutoa fidia ni sehemu ya mkakati wa kupunguza migogoro hiyo.
Aidha, amewataka wananchi kutosikiliza watu wanaopotosha ukweli au kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu fidia na uhamishaji huo.
Amesema Serikali inaendelea kulipa fidia kwa awamu kwa wananchi wote wa kata hiyo, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Malikale kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Zuberi Mabiye, amesema vituo vya urithi vinapaswa kulindwa na kuendelezwa, huku akiitaja Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuwa ni moja ya tunu kubwa ya urithi wa Afrika.
“Tangazo la kuitambua Hifadhi ya Serengeti kuwa sehemu ya urithi wa dunia ni fahari kwa Watanzania. Naomba wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hii waiheshimu, wailinde na kuitunza kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema.
Naye Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Stephano Msumi, amesema mafanikio ya uhifadhi yametokana na ushirikiano mzuri kati ya hifadhi na jamii, na kwamba juhudi hizo zitaendelea kwa manufaa ya urithi endelevu.
“Tunahitaji kivutio hiki kiendelee kuwa alama ya urithi wa dunia. Ushirikiano na jamii ndio msingi wetu, na tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi wa hifadhi hii,” amesema.
Mwakilishi wa Tume ya Taifa ya Unesco, Ana Kalumuna, amesema taasisi hiyo itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam kuhusu utunzaji na usimamizi wa vivutio vya urithi wa dunia vilivyopo nchini, pamoja na kutafuta rasilimali kwa ajili ya uhifadhi endelevu.