
Unguja. Licha ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kupunguza asilimia 50 ya ada ya kuchukua fomu ya kugombea Urais, Uwakilishi na udiwani kwa wanawake, baadhi ya wadau wa uchaguzi wamesema ada iliyowekwa ni kubwa hivyo kuitaka iangaliwe upya.
Hayo yamebainika leo Mei 6, 2025 wakati wa kikao cha tathmini ya uandikishaji wa awamu ya pili ya daftari la mpiga kura kati ya Zec na wadau wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa ZEC, ada ya fomu ya Urais ni Sh2 milioni, uwakilishi Sh250,000, Ubunge Sh50,000 na udiwani Sh10,000.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Chama Cha AAFP Taifa, Said Sound Said amesema kiwango hicho ni kikubwa na kinalenga kuwakatisha tamaa wengi washindwe kumudu hivyo ni vyema Tume ikaangalia upya mpango huo.
Kwa mujibu wa Sound, hatua hiyo ni kama Zec inalenga kukusanya kodi.
“Tuwekeeni viwango vinavyoendana na hali halisi ya watu, lakini unamuwekea mtu Sh2 milioni anazipata wapi, hivi ni vikwazo kwa watu kujitokeza kugombea hizi nafasi,” amesema.
Amesema haiingii akilikini mwakilishi ambaye hata marupurupu yake ni madogo lakini anaambiwa alipe Sh250000 lakini mbunge anatozwa Sh50,000.
“Tupeni uhuru kwanini mnaweka kiwango kikubwa, angalau Rais iwe Sh300000 na mwakilishi Sh100000 lakini sio viwango hivi, kama mnaambiwa kukusanya kodi,” amesema.
Kauli hiyo imezungumzwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Ccha ADC Taifa, Mtumwa Faizi Sadiki licha ya kupongeza kwa punguzo la asilimia 50, bado kiasi hicho ni kikubwa hususani kwa wanawake ambao hawana rasilimali za kutosha.
Amesema kiwango cha Sh2 milioni kwa mwanamke ni kubwa, pamoja na kupunguza kwa asilimia 50 bado kiwango hicho ni kikubwa sana.
“Bado hiki kiwango ni kikubwa sana, wanawake wanatamani kuingia kushindana lakni ukiona hali kama hii hivi ndio vikwazo vikubwa kwetu, kwahiyo Tume iangalie upya viwango vyake,” amesema.
Naye Ofisa uchaguzi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Muhene Said Rashid amelalamikia kiwango cha kuweka pingamizi kutoka Sh5,000 hadi Sh50,000.
Amesema kiwango hicho ni kikubwa hukua akisema huenda kinalenga kuwaondoa watu kwenye msingi wa kuhakikisha utaratibu unafuatwa.
“Tukisema kuna watu mamluki wameandikwa kupiga kura ndio kama hivi, tunawekewa vikwazo ili pingamizi zisiwekwe kwa sababu ya kiwango kikubwa, hapa ni dhahiri wanawekewa kinga,” amelalamika kiongozi huyo.
ZEC yajibu
Akijibu hoja hizo, Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema kwa kuwa bado vikao vinaendelea kuhusu masuala ya uchaguzi, watazigatia maoni ya wadau hao na ndio maana wamepunguza asilimia 50 kwa wanawake ili wapate ushiriki mkubwa.
Akifafanua zaidi kuhusu madai hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Thabit Idarous Faina amesema viwango hivyo vinawekwa ili kuleta heshima katika uchukuaji fomu kwani kinapowekwa kiwango kidogo wakati mwingine watu huchukua tu fomu kwa ajili ya kupiga picha.
“Kwa hiyo hiki kiwango cha fedha hakina nia ya kuwakomoa, lakini ni katika utaratibu tu wa kuheshimu nafasi hizi na isiwepo viwango ambavyo watu wataona kama mchezo,” amesema.
Hata hivyo, amesema maoni hayo wanayazingatia na kuyafanyia kazi na watatolea mrejesho katika vikao vinavyofuata.
Katika hatua nyingine, Tume imepokea jumla ya maombi 4,211 kutoka kwa wapiga kura waliopoteza sifa kutaka kuandikishwa upya. Kufikia Mei 5 mwaka huu, kati ya maombi hayo, wapiga kura 2,992 wamethibitika rasmi kuwa wamepoteza sifa.
Kuhusu uandikishaji wa wapiga kura wapya, jumla ya watu 101,641 wamejiandikisha, ikilinganishwa na matarajio ya kuandikisha wapiga kura 78,922. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 128.79. Kati ya waliandikishwa, wanawake ni 56,333 na wanaume 45,308.