Baraza la Wawakilishi kufunga pazia, SUK na uchumi wa buluu vyatajwa

Unguja. Mkutano wa 19 wa Baraza la Wawakilishi, ambao ni wa mwisho katika kipindi cha Baraza la 10 chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, unatarajiwa kujikita katika kujadili bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Pia, mkutano huo utakaoanza kesho, Mei 7, 2025 utajadili bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 yenye makadirio ya Sh6.8 trilioni, ambayo ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na bajeti ya Sh5.1 trilioni ya mwaka 2024/25, na tofauti kubwa zaidi kutoka bajeti ya Sh2.8 trilioni ya mwaka 2023/24.

Mbali na kujadili bajeti, Baraza la Wawakilishi linamaliza muda wake wa uhai likiwa limefanya kazi chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), mfumo wa utawala unaojumuisha vyama vikuu vya siasa vya CCM na ACT-Wazalendo.

SUK ilianzishwa kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa kitaifa, kudumisha amani, na kuhakikisha utulivu wa kisiasa baada ya historia ya migogoro ya uchaguzi visiwani.

Muundo wa uongozi wa SUK unajumuisha Makamu wa Kwanza wa Rais anayetoka chama cha upinzani na Baraza la Mawaziri linalojumuisha wanasiasa wa upinzani.

Pia, Baraza la Wawakilishi linakwenda kumaliza uhai wake wa kipindi cha miaka mitano, huku Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ikiwa imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza uchumi wa buluu, kama sehemu ya mkakati wake wa kukuza uchumi wa visiwa kwa njia endelevu.

Mkakati huo, ambao umeanzishwa na Dk Mwinyi, umelenga uchumi wa buluu unaohusisha matumizi ya rasilimali za bahari na pwani, kama vile uvuvi, utalii wa baharini, usafirishaji wa majini, nishati ya baharini, na utafiti wa viumbe vya baharini kwa lengo la kukuza pato la taifa, kuongeza ajira, na kulinda mazingira ya bahari.

Dk Mwinyi, katika kutekeleza uchumi wa buluu, ameanzisha Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, ikiwa ni hatua ya kwanza ya kisera kuonyesha dhamira ya kuiendesha Zanzibar kwa msingi wa uchumi wa bahari.

Pia, Serikali ya Dk Mwinyi, katika kutekeleza hilo, imeandaa sera ya uchumi wa buluu na kuingiza kipengele hicho katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021–2026).

Baraza linakwenda ukingoni wakati SMZ ikiwa imeboresha Bandari ya Malindi na inaendeleza bandari ndogo katika maeneo kama Mkokotoni na Wete, ili kurahisisha uvuvi, usafirishaji wa samaki, na biashara ndogo.

Pia, SMZ inahamasisha uwekezaji katika utalii wa fukwe, diving (kupiga mbizi), utalii wa viumbe vya baharini, na hifadhi za baharini kama Chumbe na Mnemba.

Kwa mujibu wa Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Raya Issa Msellem, mkutano huo utahusisha uwasilishaji wa bajeti kutoka wizara 17, maswali 311 ya msingi kutoka kwa wajumbe, pamoja na miswada miwili: wa sheria ya fedha na matumizi kwa mwaka 2025/26.

Amesema hayo ni mambo yanayoonekana kuwa na uzito mkubwa, hasa kwa kuwa ni kikao cha mwisho katika kipindi hiki cha uongozi.

Kauli ya wadau kuhusu Baraza

Mtumwa Faizi Sadiki, Naibu Katibu Mkuu wa chama cha ADC, amesema Baraza limepoteza mvuto wa awali na mijadala ilikuwa ya moto na yenye kuleta tija.

Amesisitiza kuwapo haja ya kuongeza uwakilishi wa wanawake na kujadili kwa kina masuala yanayowahusu, hasa kuhusu huduma za maji na changamoto nyingine za kijamii.

Aisha Haji Ali, mkazi wa Melitano, Unguja, amesema bado huduma za maji ni tatizo kubwa katika maeneo mengi, na wanatarajia suala hilo kushughulikiwa ipasavyo.

Kwa mujibu wa Aisha, matatizo ya maji yanawagusa watu wengi, hata wawakilishi wenyewe, hivyo haikubaliki kuona baraza likiyapuuza.

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar, Maulid Juma Mwadini, ameonesha wasiwasi kuhusu jinsi kundi hilo linavyopuuziwa katika mijadala ya baraza.

Amesema bado kuna changamoto nyingi, ikiwemo ukosefu wa pensheni jamii, mazingira duni ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kwenye uongozi, pamoja na kutoshirikishwa katika kupanga bajeti.

Ameshauri watu wenye ulemavu wapewe elimu kuhusu umuhimu wa muhimili wa baraza, ili washiriki kikamilifu na kusimamia masuala yanayowahusu.

Naima Salum Hawadh, Naibu Katibu Mkuu wa ADC, amehimiza kuwepo kwa bajeti kubwa zinazolenga makundi maalumu kama wanawake, kwani bajeti za awali zimekuwa hazikidhi mahitaji halisi ya jamii.

Kwa upande wa kilimo, Salum Ali Haji, mdau wa sekta hiyo, amependekeza Serikali kuweka mkazo kwenye kilimo cha umwagiliaji, ili kujitosheleza kwa chakula, badala ya kutegemea uagizaji kutoka nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *