Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimetaja maeneo 10 inayojivunia nayo kinaposherekea miaka 11 tangu kuanzishwa kwake huku kikisisitiza Serikali kutopuuza dai la Watanzania la uhitaji wa haki.
Mbali na dai hilo, baadhi ya maeneo ambayo ACT Wazalendo imetaja kama mafanikio yake kwa miaka 11 ni kuongoza katika siasa za hoja, kujenga jukwaa mbadala kwa wanasiasa waliokosa demokrasia kwenye vyama vyao pamoja na uwepo wa jukwaa la kuaminika kwa vijana.

Wakati ACT Wazalendo ikitaja mambo inayojivunia kwa miaka 11, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wametafsiri ukuaji wa chama hicho bado kina safari ya kujiimarisha kwani ni kichanga.
Katika dai la haki, chama hicho kimesema viongozi wa kisiasa, dini, wanaharakati na wadau mbalimbali wamekuwa wakilalamika juu ya mshikamano wa Taifa kuyumba na haki za binadamu kukiukwa, hivyo Serikali inapaswa kusikiliza sauti hizo.
Mambo hayo yametajwa jana Jumatatu Mei 5, 2025 na kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu wakati wa maadhimisho ya miaka 11 ya chama hicho kilichoanzishwa Mei 5, 2014.
Jambo la kwanza alilotaja Dorothy wanajivunia kwa miaka 11, ni chama hicho kuongoza kwa siasa za hoja dhidi ya siasa za vituko na uchawa.
“ACT Wazalendo tumetangulia mbele kusemea changamoto za wananchi na kupendekeza majawabu yake kupitia sera zetu makini, pili tumejenga jukwaa mbadala kwa wanasiasa wote wanaopenda siasa safi na ambao hawaridhishwi na demokrasia kwenye vyama vyao,” amesema.
Dorothy amesema kielelezo cha mafanikio hayo ni kupokelewa kwa hayati Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake mwaka 2019.
Kingine alichotaja Dorothy, ni ACT Wazalendo kujenga jukwaa la kuaminika kwa vijana na wanawapa nafasi kuonyesha vipaji vyao vya uongozi, akidokeza vijana waamini chama hicho ndio jukwaa lao.
“Pia tumejenga jukwaa la ukombozi wa wanawake na tumevunja minyororo ya kukandamiza demokrasia na tunaishi kwa vitendo dhana ya usawa wa kijinsia, kwa kuhakikisha kunakuwa na usawa kwenye vyombo vyote vya maamuzi,” amesema.
Uwepo wa ulingano kwenye nafasi za uongozi ndani ya nafasi za maamuzi ndani ya ACT Wazalendo, Dorothy amesema ni kielelezo ya mapinduzi makubwa ya kisiasa nchini.
Jambo lingine analotaja wanajivunia nalo, ni ujenzi wa jukwaa la Wazanzibari kujivunia nchi yao moja yenye mamlaka kamili, kwani ACT Wazalendo inakwenda kuongoza wakazi wa nchi hiyo kulikomboa Taifa lao.
Pia Dorothy amesema kwa miaka 11 tangu kuanzishwa kwa chama hicho wamejenga jukwaa la kupigania haki kwa wote kwa kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kuwakomboa Watanzania.
“Tumesimama na makundi yote kwenye jamii na ACT Wazalendo inatazamwa kama sauti ya matumaini, tumejenga chombo madhubuti ya kupigania haki ndani na nje ya nchi,” amesema.
“Pia tumeonyesha demokrasia kwa vitendo ndani ya chama na uamuzi wa chama chetu wa kuzingatia ukomo wa madaraka wa miaka 10 ni mfano wa kuigwa ambao umewashinda wengi kwenye vyama vya siasa,”amesema.
Vilevile Dorothy amesema wamejenga chama kinachokua kwa kasi na chenye ushawishi ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia ukuaji wa chama hicho, Mchambuzi wa Masuala ya Siasa, Dk Revocatus Kabobe amesema bado chama hicho kinajijenga na kusaka ushawishi.

“Bado ACT Wazalendo hakijaleta ushindani upande wa Tanzania Bara na imefanikiwa upande wa Zanzibar, sasa bado nguvu zake ni ndogo kulinganisha na CCM na Chadema kwa upande wa Bara, kwa hiyo bado kina safari ndefu ya kujijenga,” amesema.
Kwa upande wake, Mwalimu Samson Sombi, mchambuzi wa masuala ya siasa amesema chama hicho kinapaswa kujiimarisha kwa wananchi kwa kutangaza sera zake.
“Bado sera zake hazijakubalika zaidi, kwa miaka 11 safari ndefu inahitajika kupata watu wengi zaidi ili kiwe na nguvu ya kuunda Serikali,”amesema
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Isihaka Mchinjita akizungumzia hali ya demokrasia nchini amesema vyama vya siasa vinaishi katika mazingira ambayo demokrasia inaminywa.