Dar es Salaam. Misitu tisa kwenye mikoa mitano nchini itaboreshwa na mradi wa kuimarisha ustahimilivu wa Bioanuwai ya misitu ya mazingira asilia dhidi ya athari ya mabadiliko ya tabianchi.
Misitu hiyo Pugu – Kazimzumbwi (Pwani), mlima Hanang (Manyara), Pindiro na Rondo (Lindi), Uzigua (Pwani na Tanga), Mwambesi (Ruvuma), Essimingor (Arusha), Hassam Hills (Manyara) na Nou (Manyara).

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mali Asili na Utalii, Balozi Pindi Chana leo Jumatatu Mei 5, 2025 wakati akizindua mradi wa kuimarisha ustahimilivu wa bioanuwai ya misitu ya mazingira asilia Tanzania dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mbali na mradi huo, Waziri Chana pia amezindua mkakati wa kitaifa wa urejeshwaji wa mandhari ya misitu.
Mkakati huo ni wa miaka 10 kuanzia 2023-2033 na mradi ni wa miaka sita kuanzia 2023-2029 unaotekelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa udhamini wa Mfuko wa Mazingira Dunia (GEF) pamoja na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Akizungumzia mradi na mkakati huo, Waziri Chana amesema uwepo wake ni tumaini jipya kwa Watanzania la kurejesha mifumo ya ikolojia.
“Lengo ni kuimarisha uwezo wa misitu yetu kustahimili athari za mabadiliko tabianchi,” amesema waziri Chana akibainisha mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya dola 5, 837,000 ambayo ni zaidi ya Sh15 bilioni.
Amesema katika mradi huo, wataboresha miundombinu, kuimarisha utalii katika misitu na ujenzi wa vituo 13 vya ulinzi wa misitu sambamba na ujenzi wa mabanda ya kupumzika watalii katika misitu mitano.
Kuhusu mkakati, Waziri Chana amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 za Afrika ambazo zimeweka lengo la kurejesha mandhari ya misitu.

“Mkakati ni kurejesha hekta 5.2 milioni,” amesema.
Kamishna wa Uhifadhi, profesa Dos Santos Silayo amesema mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka mmoja uliopita.
“Leo (Mei 5) ni uzinduzi kiutendaji, lakini ulianza kutekelezwa mwaka mmoja uliopita,” amesema profesa Silayo.
Amesema nchi imedhamiria kurejesha mandhari takribani hekta 5.2 milioni ambazo kati ya hizo, hekta 25,000 zitarejeshwa upande wa Zanzibar.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Tito Magoti amesema kwenye eneo hilo misitu ipo salama, akitangaza kiama cha wakata mkaa ambao alidai wengi wao ni viongozi na si wananchi wa Kisarawe.
“Wamenunua pikipiki na kuwapa watu, hivyo niwaambie tu, yeyote atakayekata misitu tutakula naye sahani moja.”
Amesema kuna viongozi wapo wanakata mkaa wana pikipiki hadi 85, akidai amekuwa akipokea vimemo akitakiwa awaachie baadhi ya wakata mkaa waliokamatwa.
“Kama nilivyosema, si wananchi wa Kisarawe, na ni viongozi, hawa nitadili nao,” amesema Magoti.

Waziri Chana katika uzinduzi huo amesisitiza hatua kali dhidi ya wavamizi na wote wanaotumia rasilimali bila vibali zichukuliwe.
“Yapo maeneo watu wanaingiza ng’ombe, maeneo mengine wanakata mkaa, lazima tuyalinde kwa masilahi ya Watanzania wote,” amesema.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas, Waziri Chana ameikabidhi TFS magari matatu na pikipiki 20 kwa ajili ya kuimarisha doria na kusaidia vita dhidi ya ujangili.