
Morogoro. Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amesema kwa kipindi cha miezi minane, amewaachia huru jumla ya wafungwa 68 waliobainika kutenda makosa hayo wakiwa na changamoto ya afya ya akili.
Waziri huyo ameyazungumza hayo leo Jumatatu Mei 5, 2025 wakati akifungua mafunzo maalumu ya siku tano kwa maofisa sheria wa Jeshi la Magereza, yenye lengo la kuongeza maarifa na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Amesema kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025, ametoa amri ya kuwaachilia huru jumla ya wakosaji 68 waliotenda makosa wakiwa na changamoto za afya ya akili, baada ya kuthibitishwa kuwa wamepona na wako tayari kurejea uraiani.
Kwa mujibu wa Dk Ndumbaro, amri hiyo imetolewa kwa Kifungu cha 219(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kinachompa waziri mwenye dhamana mamlaka ya kutoa msamaha huo kwa wahalifu waliokuwa wakihifadhiwa kwa uangalizi maalumu katika Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe na Isanga, mkoani Dodoma.
“Kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Aprili 2025, wakosaji 68 wameachiwa huru baada ya kuthibitishwa afya zao kuwa zimeimarika,” amesema Dk Ndumbaro.
Akiendelea kufafanua hatua nyingine zinazochukuliwa na wizara yake, Dk Ndumbaro amesema kuwa inaendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa kuimarisha ulinzi kwa watoa taarifa za uhalifu pamoja na mashahidi.
Amebainisha kuwa rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Ulinzi wa Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi (Sura ya 446) ipo katika hatua za mwisho baada ya wadau mbalimbali kutoa maoni yao.
Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza (CGP), Jeremiah Katungu, amesema kuwa mafunzo hayo yanayoshirikisha maofisa sheria 120 kutoka mikoa mbalimbali, ni sehemu ya mkakati mpana wa kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa jeshi hilo.
Amesema kuwa licha ya kuwa na zaidi ya maofisa sheria 264 nchi nzima, ni muhimu kuwawezesha kisheria kwa kuwa wao ndio kiungo kikuu katika utekelezaji wa haki kwa wafungwa na mahabusu.
“Matarajio yetu ni kwamba washiriki wa mafunzo haya watakuwa mabalozi wa mabadiliko, kwa kuwafundisha wenzao ambao hawakupata nafasi ya kushiriki, hivyo kuongeza tija na weledi katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku,” amesema Katungu.
Aidha, amebainisha kuwa mpaka sasa Serikali imefanikiwa kujenga vyumba vya Mahakama Mtandao katika magereza 66 nchini, ikiwa ni juhudi za kurahisisha usikilizwaji wa mashauri kiteknolojia. Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto bado ipo katika wilaya 50 ambazo hazina magereza, hivyo watuhumiwa hulazimika kushikiliwa katika wilaya jirani.
“Kwa sasa, ujenzi wa magereza 12 unaendelea katika hatua mbalimbali ili kupunguza msongamano na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa haki,” ameongeza.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi amesema kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Magereza, yakilenga kuwajengea uwezo maofisa sheria katika kushughulikia masuala ya kisheria kwa umahiri, kutokana na mabadiliko ya sheria na teknolojia.