
Moshi. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa ameelekeza kuanza kwa mchakato wa kugawanywa kwa kata ya Mabogini, yenye watu zaidi ya 60,000 iliyopo wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kugawanywa kwa kata hiyo, kunatokana na idadi kubwa ya watu wanaoishi eneo hilo, ambapo pamoja na mambo mengine amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo, Yusuf Nzowa kupeleka taarifa rasmi ofisi za Tamisemi leo, Mei 5.
Maagizo hayo ameyatoa leo Jumatatu Mei 4, 2025 akiwa kwenye ziara yake ya kikazi katika Kata ya Mabogini, mkoani humo.
“Nimefarijika sana kumwona diwani anayesimamia kata yenye watu zaidi ya 60,000 hii sasa ndio tafsiri ya akina mama wanaweza, kata yenye watu zaidi 60,000 ni sawa na jimbo.
“Kata hii igawanywe mara moja, sasa kwa takwimu na idadi ya watu nimeridhika kabisa kata hii inapaswa kugawanywa, namwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro aniletee taarifa haraka kesho (leo) nizipate Tamisemi,” amesema Mchengerwa
Pamoja na mambo mengine amemwagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), Victor Seff kufanya tathmini ya haraka kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mabogini- Kahe- Chekereni yenye urefu wa kilomita 31.2 kwa ajili ya matengenezo ya dharura.
“Moja ya changamoto kuu inayowakabili wananchi Moshi vijijini najua ni barabara, namwelekeza Mtendaji Mkuu wa Tarura alete hapa Kahe- Mabogini Sh7 bilioni kukarabati barabara hii iweze kupitika wakati wote,” amesema Mchengerwa.
Amesema “Mchakato huu nataka uanze mara moja sio mwaka wa fedha ujao ni mwaka huu, nikiondoka hapa wataalamu waje wafanye tathmini na tuanze mara moja kujenga barabara hii iweze kupitika wakati wote.”
“Awamu ya pili nimeshamwelekeza Mtendaji wa Tarura kwamba barabara hii tuingize katika programu ya maboresho ya Jiji ili kusudi tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami ambacho wananchi wanataka,” amesema Mchengerwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema barabara hiyo imekuwa na changamoto na maji yamekuwa yakiingia kwenye makazi ya wananchi.
“Wananchi hawa wote tatizo lao kubwa ni barabara na wakati wa mvua kubwa, maji yanaingia kwenye nyumba zao na baada ya mvua za juzi kuna kaya 62 hazina mahali pa kukaa,” amesema RC Babu.
Akizungumzia barabara hiyo, Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, Mercy Mollel amesema kutokana na ubovu wa barabara hiyo, wananchi wanashindwa kusafirisha mazao, wagonjwa na mvua zinavyozidi wanashindwa kutoka nyumbani.