
Wanariadha wa Tanzania wamekuwa na mwamko mkubwa kwa siku za hivi karibuni kutokana na jinsi ambavyo wamekuwa wakipeperusha bendera kwenye mashindano mbalimbali.
Ni kawaida kwa wanariadha wetu kufanya vizuri kuanzia kizazi cha kina Filbert Bayi hadi sasa ambapo tunatamba na Alphonce Simbu na Gabriel Geay.
Hiki ni kizazi ambacho kimeendelea kuliletea taifa hili heshima kubwa na wanariadha wake wameonekana kuwa na kasi nzuri kuliko kipindi kifupi hapo nyuma.
Huu umekuwa mwaka mzuri kwa wanariadha hao maarufu wa mbio ndefu nchini baada ya awali Geay kufanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mashindano maarufu ya Daegu Marathon yaliyofanikiwa nchini Korea ya Kusini.
Geay ambaye makazi yake ni Arusha alifanikiwa kuibuka mshindi wa kwanza kwenye mashindano hayo akimaliza kwa kutumia saa 2:05:59 katika mashindano hayo ambayo yalishirikisha wanariadha mbalimbali wakubwa akiwemo Addissu Gobena na Dejene Magersa.
Hizi zilikuwa mbio maarufu ambazo mwanaridha huyo ambaye alishindwa kumaliza kwenye mashindano ya Olimpiki mwaka jana alipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Geay ambaye ana rekodi ya kushika nafasi ya pili kwenye mashindano ya Boston Marathon ni kati ya wanariadha ambao wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vyema kwenye mashindano yoyote ya ngumi.
Awali kabla ya mbio hizo za Daegue, Geay alifanya vizuri pia kwenye mbio za Huston Marathon ambazo zilifanyika nchini Marekani baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwa kutumia dakika 59:18.
Mbali na Geay, staa mwingine kwenye riadha ambaye ameonekana kuunza mwaka vizuri ni Simbu ambaye hivi karibuni alishika nafasi ya pili kwenye mbio maarufu za Boston Marathon.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanaridha huyo maarufu kufanya mambo makubwa kwenye mbio hizo na unaonekana kuwa mwanzo mzuri kwake.
Simbu ambaye ni mwanariadha mwenye heshima kubwa nchini alifanikiwa kumaliza mbio hizo kwa kutumia saa 2:05:04 ukiwa ni muda wa pili kwa kasi zaidi katika historia ya mbio hizo akitanguliwa kwa sekunde chache na Mkenya John Korir ambaye alimaliza mshindi wa kwanza.
Hizi ni mbio nyingine ambazo zilihusisha wanariadha wakubwa Afrika na duniani kote, akiwemo Korir, Conner Mantiz raia wa Marekani, pamoja na Mkenya Cybrian Kontut lakini Mtanzania huyo akafanya vizuri na kuileta heshima nchi.
Haya ni mashindano ya pili Simbu naye anafanya vizuri kwa kipindi kifupi baada ya mwaka jana kufanya vizuri kwenye mbio za Valencia kwa kuweka rekodi binafsi ya yakumaliza kwa saa 2:04:38.
Haya ni mashindano ambayo yamekuwa yakiwaneemesha zaidi wanariadha kutokana na kuwa na udhamini mkubwa, hivyo ni wakati wao sasa kuhakikisha kuwa wanajiandaa vizuri pia kwenye yale ya kitaifa kama Olimpiki.
Heshima kubwa ambayo wameiweka huku, ndiyo kiwango hicho ambacho Watanzania wanakisubiri kwenye mashindano mengine makubwa ambayo yanahushisha riadha.