MZEE WA FACT: Tuangalie upya mafunzo ya waamuzi wetu

Niko kwenye TV nasubiri kuangalia mechi ya ligi kuu, kati ya wanafainali wa Kombe la Shirikisho la CAF, Simba SC, dhidi ya Mashujaa.

Nilitarajia kuona bonge moja la mechi kama kawaida ya timu hizo mbili zinapokutana.

Tangu wakutane mara ya kwanza mwaka 2018, Simba wakiwa wana robo fainali wa ligi ya mabingwa Afrika, na Mashujaa wakiwa daraja la kwanza.

Ilikuwa mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB, kwenye Uwanja wa Taifa, pale kwa Mkapa ambapo Simba waliapa kwamba hatoki mtu.

Mashujaa walishinda mechi hiyo 3-2 na kuwatoa Simba waliokuwa mabingwa watetezi.

Hata Mashujaa walipopanda daraja kwa gharama za Mbeya City, bado mechi zao dhidi ya Simba hazikuwa za kubeza walitoa mechi hasa.

Kwa hiyo nikaruhusu watoto waende wakacheze nje ili nione Mashujaa wakipambana na wana fainali wa Afrika.

Wakati uchambuzi wa kwenye TV unaendelea, nikawa naperuzi peruzi mtandaoni, nikaona chapisho la mchambuzi wa Wasafi FM, Anwary Binde, akiutabiria mabaya mchezo huu.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Binde aliweka chapisho linalotabiri kuwepo kwa kadi nyekundu na penalti kwenye mchezo huo.

Nikagonga ‘like’ na kupita, nikichukulia hilo kama utani wa mitandaoni.

Mara timu zinaingia uwanjani na namuona Kefa Kayombo kama mwamuzi wa kati. Kumbukumbu zangu zikaja kwa mechi kadhaa ambazo mwamuzi huyu alikuwa kati na namna alivyoharibu mambo.

Lakini nikajipa moyo kwamba labda leo atakuwa na siku nzuri ofisini.

Ghafla Mashujaa wakapa bao, hali ya hewa ikabadilika. Nikaanza kumuona Kayombo akiyumba katika maamuzi yake, pamoja na wasaidizi wake, hasa mwanadada Neema Wilson Mwambashi, aliyekuwa msaidizi namba moja.

Mara Simba wakapata penalti, utabiri wa kwanza wa Binde ukatimia na yeye mwenye akarudi kuthibitisha.

Hapo sasa akili ikaanza kunikaa sawa na kurejea matukio ya mechi zingine ambazo mwamuzi Kayombo alizichezesha.

Hivi ndivyo walivyo waamuzi wetu. Unaweza ukawatabiri, hadi muda wa matukio, na ukapatia.

Watu wengi wameizungumzia mechi hii kwa hisia za kifitna…kwamba Kayombo hakufanya makossa ya kibindamu bali ya kupangwa.

Mimi sitaki kujikita huko, nataka tuyaangalie maamuzi ya Kayombo na wenzake kwa jicho lingine kabisa, litakaloweza kutusaidia kupata picha nyingine tofauti.

1.NJANO YA KWANZA YA MUNTHALI

Kipa wa Mashujaa, Patrick `Munthali, aliumia na kumwambia mwamuzi, Kayombo, ambaye aliwaita madaktari.

Wakati wakiwa njiani kumtibu kipa, Kayombo akatoa kadi ya njano kwa kipa huyo akimtuhumu kupoteza muda.

Inawezekanaje hilo likafanyika kabla madaktari hawajafika? Kama alibaini kipa anapoteza muda, kwanini aliita madaktari?

Hii kadi ndiyo iliyokuja kuzaa nyekundu baadaye baada ya kupatikana njano nyingine.

Ilitakiwa Kayombo awaite madaktari, wamuangalie kipa alipoumia, wamtibu…kama ilikuwa upotezaji muda, basi hapo ndiyo amuadhibu…lakini siyo unaita madaktari, kabla hawajafika, tayari umetoa kadi.

Haya ni makosa ya kukosa maarifa siyo ya kibinadamu wala ya kupanga.

2.NJANO YA PILI KWA MUNTHALI

Mpira ulitoka, ikaingizwa miwili, Ellie Mpanzu wa Simba akaupiga mmoja kuutoa nje, ukaenda kugonga bango la matangazo na kurudi uwanjani, lakini ukasimama juu ya mstari.

Beki wa Mashujaa akaupiga kuuingiza ndani ukaenda kwa kipa, akaugusa kupeleka uwanjani, refa akampa njano. Kimsingi aliyestahili njano ni yule beki aliyeupiga ule mpira kwenda kwa kipa, siyo kipa aliyeusogeza mbele kidogo.

3.MACHELA KUMTOA KIPA

Baada ya kadi nyekundu kwa Munthali, akaingia kipa mwingine dakika chache baadaye naye akaumia.

Kayombo akaita machela imtoe kipa akatibiwe nje ili mechi iendelee. Hili kosa ni kipimo kikubwa zaidi kwa uwezo wa Kayombo.

Kipa anatakiwa kutibiwa palepale alipoumia na mpira unatakiwa usimame kusubiri matibabu.

Zikifika dakika tano hajapona, ndipo anatakiwa kutolewa nje na aingie kipa mwingine…lakini siyo eti machela ije imtoe.

4.PENALTI YA PILI

Simba walipata penalti ya pili dakika za mwisho kabisa. Penalti hii ilitolewa na mwamuzi msaidizi namba moja, Neema Wilson Mwambashi.

Kitu cha ajabu ni kwamba, alipoona madhambi na kuinua kibendera, alitakiwa aende hadi mwisho na kuzunguka kibendera cha kona kuashiria kwamba hii ni penalti.

Lakini yeye alisimama pale pale akiwa hajui afanye nini.

Hii inaonesha kabisa kwamba waamuzi hawa hawajui watendacho uwanjani, hawajaiva kuwa waamuzi wa ligi kuu.

Haya makosa yote tunayoyaona, ni kwa sababu ya uwezo wao.

Mtu anaweza kuhoji kwamba kwanini ifaidike timu moja, jibu ni rahisi, upande upi unampa presha zaidi.

Kidole chenye kidonda ndiyo rahisi zaidi kujikwaa, kwa sababu ndicho kinachokupa presha zaidi.

Mashabiki wa Simba walikuwa wengi zaidi ya Mashujaa, kelele zao zilipeleka presha kwa waamuzi.

Kwa hiyo wakati tukiwalalamikia waamuzi hawa kwamba wametumika vibaya, tuangalie na upande huo.

Refa anayetaka kuipendelea timu, hawezi kuita machela imtoe kipa wa timu nyingine ili mpira uendelee, bali refa asiyejua afanyalo, kama Kayombo.

Hawa waamuzi warudi darasani kujifunza…wana maarifa madogo sana ya uamuzi, tutawalaumu bure tu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *