Dar es Salaam. Dunia ya leo siyo ile ya jana, enzi za barua kutumwa posta kufika baada ya wiki mbili. Hii ya sasa kidijitali aliyepo Mwanza anatuma ujumbe unafika muda huohuo. Hapo ndipo ukali wa teknolojia unapoonekana.
Ndiyo ni teknolojia hiyo hiyo iliyosambaza habari kuwa Dogo Paten ni mkali wa muziki wa singeli. Yaani ukali wa teknolojia ukakutana na nguvu ya ushawishi kutoka kwa Zuchu ambaye anamiliki wafuasi zaidi ya milioni sita kwenye ukurasa wake wa Instagram na zaidi ya milioni nne kwenye ukurasa wake wa TikTok.

Ogopa sana vitu hivi viwili, yaani nguvu ya ushawishi na teknolojia. Kama hauamini fuatilia mchezo ulivyochezwa, baada ya Zuchu kuonesha kuukubali wimbo wa Dogo Paten ‘Afande’ ambao aliona kipande chake kwenye mtandao wa TikTok na kupelekea kufanya kazi na msanii huyo.
Kupitia komenti moja tu ya Zuchu upepo ukabadilika kila mtu akaanza kusifia uwezo wa msanii huyo mchanga wa singeli. Mwisho wa siku wawili hao wakavutana studio na kufanya remix ya ‘Afande’. Haikuishia hapo Zuchu akaonesha shauku ya kumkuza na kumtambulisha Paten kwa jamii. Akampandisha kwenye jukwaa la tamasha la Samia Serengeti Music Festival.
Unaweza kusema lengo la Zuchu likatimia kwani baada ya hapo habari ikawa moja tu kwenye mitandao ya kijamii, siyo peji za udaku wala za viongozi wote walinyoosha mikono kwa kuukubali uwezo wa Paten hayo mahojiano kwenye vyombo va habari ndiyo usipime leo utamsikia redio mbao, kesho utamuona kwenye TV ya chogo.
Lakini wakati yote hayo yakiendelea, swali ni je? Paten atadumu kwenye masikio ya watu au atapitiwa na upepo wa kisulisuli uliowasomba baadhi ya waliovuma na kupotea kwa muda mfupi. Wako wapi hawa?.

Hamisi BSS
Huyu aligonga sana vichwa vya habari katika shindano la kusaka vipaji vya uimbaji la Bongo Star Search (BSS) 2019, kutokana na uwezo wake wa kuimba nyimbo za zamani pamoja na kupiga gitaa kwa umahiri mkubwa.
Akiwa katika kilele cha umaarufu wake, Harmonize alijitokeza na kuahidi kuwa atamsaini katika rekodi lebo yake, Konde Music Worldwide lakini hajatimiza ahadi hiyo hadi sasa na Hamisi BSS hasikiki tena.
BSS ni kipindi cha televisheni ambacho majaji wake wa muda mrefu ni Madam Rita Paulsen, Master J na Salama Jabir, huku kikitoa wasanii wakubwa kama Kala Jeremiah, Peter Msechu, Walter Chilambo, Kayumba, Frida Amani, Phina n.k.
Kinata MC
Mkali huyu wa Singeli, alikuwa akipiga freestyle katika kituo kimoja cha redio Pwani, video hiyo ikapata mapokezi makubwa mtandaoni, wengi walifurahi jinsi alivyokuwa akiimba Kiswahili na Kiingereza katika Singeli.

Ndani ya siku chache tu, akaingia studio na msanii wa Konde Music, Ibraah kisha wakatoa wimbo wao, Do Lemi Go (2021) uliofanya vizuri hadi Kinata MC kuchaguliwa kuwania vipengele vitatu katika Tuzo za Muziki Tanzania (TMA).
Hata hivyo, baada ya kolabo hiyo, Kinata MC amekuwa na wakati mgumu kimuziki maana ameshindwa kuja na wimbo mwingine uliofanya vizuri kama huo, huku akiwa hana tena uhusiano mzuri na Konde Music.
Mwimbaji huyo alirekodi wimbo, Please Don’t Go Away (2016), akiwa na Akon na hii ni baada ya Mayunga kushinda katika shindano la Airtel Trace Music Star Africa ndipo akapata nafasi ya kufanya kazi na staa huyo ikiwa ni sehemu ya zawadi ya shindano hilo.

Mayunga aliachia wimbo huo Mei 2016, lakini tayari ulikuwa umerekodiwa tangu mwaka 2015, aliposhinda shindano hilo lilojumuisha nchi 12, fainali zake zilifanyika Nairobi Kenya Machi 2015, huku Akon akiwa ni sehemu ya majaji pia.
Baada ya mradi huu na Akon, mwanamuziki wa Senegal mwenye makazi yake Marekani, wengi walitarajia Mayunga atafika mbali kimuziki lakini haijawa hivyo licha ya kuachia kazi nzuri kwa kipindi chote ambacho amekuwepo katika muziki.
Brian Simba
Kijana huyu alimkosha sana Vanessa Mdee hadi kufikia hatua ya kumsaini katika rekodi lebo yake, Mdee Music akiwa ni msanii wa pili baada ya Mimi Mars aliyetoka na wimbo wake, Sugar (2017).
Licha ya kuja kutoa wimbo na Vanessa, Silence (2018), bado Brian Simba hakuweza kutengeneza jina kubwa katika Bongofleva kama wenzake wengi akiwemo Marioo waliokuwa wanachipukia wakati huo.
Na baada ya Vanessa kuachana na muziki mwaka 2020, mdogo wake Mimi Mars alisema kuwa Brian Simba hayupo tena Mdee Music maana lebo haina fedha za kujiendesha kwa sababu mwanzilishi wake ameshakaa pembeni.
Ally Nipishe
Mwimbaji huyo alitoka chini ya Tanzania House of Talent (THT) na kushinda tuzo ya TMA kama Msanii Bora Chipukizi 2013, lakini baada ya hapo alipotea kabisa.
Wengi watamkumbuka Ally Nipishe kupitia wimbo wake, My (2013), pia kolabo yake na Mwasiti, Mapito (2012) ambayo iliandikwa na Amini, mwanamuziki mwingine aliyetolewa na THT.
Kwenye moja ya mahojiano yake mwaka 2015, Ally Nipishe alisema sababu ya kupotea kwake kimuziki ni kwamba aliuziwa gari la wizi hivyo kesi hiyo kwa sehemu kubwa ilimtoa katika mchezo kwa kuchukua muda na fedha zake.
Lody Music
Mbali na hao yuko wapi Lody Music aliyewakosha na kuwatoa machozi wanaoteswa na mapenzi kwa wimbo wake ‘Kubali’. Uliotoka miaka mitatu iliyopita, na kuwafanya baadhi ya watu, waamini mwanzo wake wa kishindo unatafsiri namna atavyoliteka soko la muziki Bongo. Lakini leo yuko wapi.

Si hao tu wapo wengi waliotoweka kwa haraka. Hiyo ni tafsiri tosha kuwa mashabiki siyo watu wa kuelekewa kuna wakati hupelekwa na upepo unavyotaka na wakati mwingine huchoshwa na kelele za aina moja. Hivyo ni jukumu la msanii kuhakikisha anabaki na kijiji alichojizolea mwanzo.
Mbinu ya kudumu kwenye gemu
Akizungumza na Mwananchi, Docta Ulimwengu ambaye anasimamia chapa za mastaa kama Hamisa Mobetto, Jux na Idris Sultan na hapo awali alimsimamia Jay Mondy amesema kinachowaponza wasanii wanaovuma na upotea ni kutokuwa na akiba ya kazi za kutosha.
“Changamoto inayokuja ni kwamba ‘industry’ imebadilika sasa hivi sanaa ni biashara kubwa sana. Siku zote watu wanaweka pesa sehemu ambayo wanauhakika itakuwepo. Wasanii wengi wachanga unakuta ana wimbo mmoja alafu huohuo unategemewa.
“Unakuta hana mwingine hiyo inatengeneza stress ya kupata wimbo mwingine mkubwa zaidi ya ule. Hit song haitengenezwi kwa kusema, kwa sababu muziki ni hisia lazima ujipe muda, panga mipango yako vizuri na ndiyo maana wasanii ambao wapo kwenye label kubwa, wanadumu kwa sababu mbali na wimbo ulioachiwa mwanzoni zipo nyingine nyingi zinasubiri tu wakati,”amesema.
Amesema ili kuepuka majanga ya kupotea kwenye gemu lazima kuwe na mipango endelevu.
“Mtu akitoka na wimbo mmoja anaanza tena kuhangaika studio kutafuta wimbo mzuri zaidi ya huo. Tayari unakuwa umekosea, mipango ya biashara ni lazima kabla msanii hujaachia wimbo jipange usiharakishe kwa sababu utaishia kupata umaarufu lakini huna hela.
“Kaa chini andaa miradi yako kama unataka kufika mbali na kupata malengo ya kudumu kwenye gemu lazima ujipe muda wa kujiandaa. Tafuta watu sahihi wa kukusaidia.’’
Hata wasanii wakubwa wana nyimbo nyingi sana, kila siku wanarekodi na unaweza kukuta kwa mwaka ametoa nyimbo sita lakini anazo nyingine zaidi ya 30. Hicho ndicho kinawasaidia zaidi,”amesema