Mchengerwa ahitimisha sakata ujenzi jengo la utawala Arusha

Arusha. Baada ya kuwapo tuhuma za ubadhirifu kuhusu ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Jiji la Arusha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema yuko jijini humo kuhitimisha minong’ono, maneno yaliyowavuruga na kuwachanganya, hivyo kuvuruga ujenzi.

Mbali ya hayo, amemweleza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Dk Emmanuel Nchimbi, ameelekeza migogoro iliyopo mkoani humo isiwe chanzo cha kushusha hadhi ya Serikali, badala yake hatua zichukuliwe.

Amesema hayo leo Mei 2, 2025 alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo ambalo ujenzi wake ulikwama tangu mwaka 2019.

Aprili 23, 2025 Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo (CCM), aliliomba radhi Bunge kutokana na kauli yake dhidi ya Waziri Mchengerwa aliyemtuhumu kuwa alisema uongo alipotoa maelezo ya Serikali dhidi ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa jengo hilo.

Tuhuma hizo zilimlazimu Spika, Dk Tulia Ackson kuagiza suala hilo lichunguzwe na Kamati ya Kudumu ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kabla ya utekelezaji wa agizo la Spika, Gambo aliomba radhi na kufuta kauli yake.

Waziri Mchengerwa akizungumza wakati wa uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo unaoendelea amesema:

“Leo nimekuja kumaliza jambo hili, watumishi wa Jiji wamesota kwa muda mrefu, wananchi wamehangaika kwa muda mrefu leo nimekuja kumaliza suala hili. Uwekaji jiwe la msingi tunahitimisha minong’ono na maneno ambayo yalikuwa yanatuvuruga na kutuchanganya na mengi yamechangiwa na migogoro ya kisiasa iliyokuwapo.”

Amesema unakaribia mwaka wa sita tangu ujenzi wa jengo hilo kukwama kutokana na sintofahamu iliyochangiwa na migogoro ya wanasiasa.

“Miradi hii ya Jiji la Arusha ambayo mmoja nauweka jiwe la msingi leo ulikwama tangu mwaka 2019, inawezekana Arusha leo mngekuwa mnazungumzia miradi mingine. Mmefika hapa kwa sababu ya mivutano ya kisiasa na hii haikubaliki hata kidogo,” amesema.

Mbali ya hayo, Mchengerwa amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua, baadhi ya watumishi wasio waadilifu wanaovujisha nyaraka za siri za Serikali na kuzisambaza kwenye mitandao ambazo wakati mwingine zinazua sintofahamu kwa jamii.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema utiaji saini mikataba ya ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ya mkoa huo na masoko mawili kupitia mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya miji Tanzania (Tactic) ni historia mpya kwa mkoa huo.

Amesema Jiji la Arusha linatumia jengo lililojengwa tangu enzi za mkoloni na kwamba, wananchi wamekuwa wakifuata watumishi katika maeneo mengine, yakiwamo Sakina au Njiro kwa kuwa wamelazimika kugawanyika katika majengo mengine.

“Watumishi wanafanya kazi katika mazingira magumu ila mbaya zaidi mwananchi anapomfuata mtumishi aje amhudumie anaambiwa mtumishi yuko Sakina au Njiro matokeo yake anaingia gharama ya nauli kwenda huko,” amesema na kuongeza:

“Akifika huko baada ya kusikilizwa anaambiwa nyaraka zako ziko jiji, wananchi wanazunguka sana kwa miaka yote kutokana na kutokupata huduma katika eneo moja. Utiaji saini mikataba iliyokuwa visiki, ambayo kila aliyekuwa akisogelea anang’oka yeye au mkataba unang’oka leo tunashuhudia historia inaandikwa.”

Mchengerwa pia alishuhudia utiaji saini miradi ya Tactic yenye thamani ya Sh30.5 bilioni ambayo ni ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Mkoa wa Arusha (Bondeni City), Soko la Kilombero, Soko la Kwa Mrombo na Bustani ya Themi.

Wakati wa utiaji saini, Meya wa Jiji la Arusha, Maxmillian Iranghe ameshukuru Serikali kwa utekelezaji wa miradi hiyo iliyokwama kwa kipindi kirefu.

“Waziri Mchengerwa ni mwanasheria aliwahi kuwa hakimu, nimesema taaluma yake kwa sababu ile hukumu aliyoitoa alipokuwa bungeni wiki mbili zilizopita ilikuwa halali, ilikata mzizi wa fitina kukata ngebe za wale waliokuwa wanakwamisha stendi yetu,” amesema.

Katika utiaji saini, Mkoa wa Arusha umewatambua viongozi waliowezesha kupatikana eneo la bure lenye ukubwa wa ekari 30.

Miongoni mwa hao ni  aliyekuwa Meya wa jiji hilo, Calist Lazaro ambaye kwa niaba ya wenzake alishukuru uongozi wa mkoa kwa kutambua mchango wao. Alieleza ucheleweshaji wa ujenzi wa stendi, Serikali haipaswi kulaumiwa kwani waliochelewesha ni viongozi waliokuwapo.

“Tulikuwa tunashughulikiana wenyewe kwa wenyewe na aliyekuwa anatushughulikia ni huyu aliyeomba msamaha juzi,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *