Polisi Mbeya yakanusha kuhusika tukio la kushambuliwa Mdude

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limekanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa askari wake wanahusika katika tukio la kuvamiwa na kupigwa kwa kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia ni mwanaharakati, Mdude Nyagali.

Kwa mujibu wa Jeshi hilo, taarifa hizo siyo za kweli na zinalenga kupotosha umma kuhusu uhalisia wa tukio hilo ambalo bado linaendelea kuchunguzwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, ametoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari leo, Ijumaa Mei 2, 2025.

Kauli hiyo ya Kamanda wa Polisi imetolewa saa chache baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii zikieleza kuwa watu waliodaiwa kuwa askari wa Jeshi la Polisi walivamia nyumba ya kada huyo, kuvunja mlango na kisha kumshambulia kwa kipigo.

Awali, akizungumzia tukio hilo leo Mei 2, 2025, Kamanda Kuzaga amesema kuwa Jeshi la Polisi limepokea taarifa kutoka kwa mwanamke aitwaye Sije Emmanuel (31), mkazi wa Iwambi, ambaye ni mke wa Mdude Nyagali.

Ilielezwa kuwa majira ya saa 8:00 usiku wa kuamkia leo, Mei 2, 2025, wakati wakiwa wamelala nyumbani kwao katika Mtaa wa Ivanga, Kata ya Iwambi, jijini Mbeya, watu wasiojulikana walivamia nyumba hiyo kwa kuvunja mlango, wakaingia ndani na kisha kumjeruhi Mdude Nyagali kwa kumshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake.

Amesema kuwa baada ya kufanya tukio hilo, watu hao walifanikiwa kutoweka pamoja na mumewe, wakimchukua na kumpeleka kusikojulikana.

Kufuatia maelezo hayo, Jeshi la Polisi limekanusha vikali taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa askari wa polisi wanahusishwa na tukio hilo.

Aidha, Kamanda Kuzaga amesema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na ufuatiliaji wa kina ili kuhakikisha Mdude anapatikana, pamoja na kuwabaini wote waliohusika katika tukio hilo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi na jamii kwa ujumla kushirikiana na jeshi hilo kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia kubaini mahali alipo Mdude  pamoja na watu waliotekeleza tukio hilo.

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Hamad Mbeyale amesema kuwa msimamo wa chama hicho ni kutaka kufahamu mahali alipo kada wao huyo pamoja na sababu za kuchukuliwa.

“Msimamo wetu ni kwamba tunahitaji kujua aliko kada na mwanaharakati Mdude, kwani mazingira ya purukushani zilizotokea nyumbani kwake yanatupa mashaka,” amesema Mbeyale.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa jiji hili wameeleza kushtushwa na tukio hilo, huku wakitoa wito kwa Serikali kulitazama kwa jicho la tatu na kuchukua hatua stahiki.

“Tunaelekea kwenye uchaguzi, na matukio ya aina hii yameanza kujitokeza. Kimsingi, sisi wananchi tunaingiwa na hofu na mashaka kuhusu matukio kama haya,” amesema Allen Fredy, mkazi wa Mbeya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *