Wauaji wa dereva bajaji waliokamatwa wakitafuta mteja, wahukumiwa kunyongwa

Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, imewahukumu adhabu ya kifo, watu wawili waliomuua dereva wa bajaji, Omary Yahaya na kisha kukamatwa na Polisi wakiwa katika harakati za kuiuza bajaji hiyo.

Waliohukumiwa adhabu ya kifo katika hukumu iliyotolewa Aprili 30, 2025 na Jaji Hamidu Mwanga iliyowekwa katika tovuti ya mahakama leo Mei 2, 2025 ni Samwel Daudi na Brayan Yakobo, huku mshitakiwa wa pili, Juma Juma akiachiwa huru.

Akitoa adhabu hiyo baada ya kuwatia hatiani washitakiwa hao, Jaji Mwanga alisema mikono yake imefungwa na kiapo alichokula cha kulinda Katiba na sheria za nchi na kwamba adhabu pekee kwa kosa la kuua kwa kukusudia ni kifo.

Mwili wa dereva bajaji huyo ulipatikana Julai 2, 2019 ukiwa katika eneo la Malindi Mbweni Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati huo bajaji aliyokuwa akiiendesha ikiwa haijulikani ilipo.

Kulingana na shahidi wa sita wa Jamhuri, Ezekiel Kiogo, baada ya kupatikana kwa mwili huo, ulipelekwa katika hospitali ya Mwananyamala na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Uchunguzi huo ulifanywa na shahidi wa saba wa Jamhuri, Dk Atuganile Malango ambaye alibaini mwili huo ukiwa na majeraha kifuani, mgongoni na tumboni, lakini pia kulikuwa na alama maeneo ya shingoni na mifupa ya shingo ilikuwa imevunjika.

Halikadhalika kucha zilikuwa na rangi ya bluu huku wengu likiwa limepasuka, tumbo likiwa limejeruhiwa na mapafu yalikuwa na maji na Dk Malango akahitimisha sababu za kifo ni kutokana na majeraha na kukosa hewa ya oksijeni.

Kwa maoni yake, shingo ya marehemu ilifungwa kwa kamba au kitambaa kilichokazwa na kwamba kifo chake kilisababishwa na majeraha mbalimbali mwilini, kukosa hewa ya oksijeni na mshtuko wa kupasuka kwa wengu.

Namna mwili ulivyogundulika

Kulingana na ushahidi, Julai 2, 2019, mwili wa marehemu uligunduliwa na mtu aliyetajwa kuwa ni John Edward, ukiwa pembeni ya barabara eneo la Malindi Wilaya ya Kinondoni na tukio hilo kutolewa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Polisi walifika na kuuchukua mwili na kuupeleka hospitali ya Mwananyamala na baadaye kuhamishiwa MNH kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiini cha kifo.

Kabla ya umauti kumkuta, Omary Yahaya (marehemu) alikuwa amekodiwa na Victoria Nyoni lakini ghafla akiwa kwenye majukumu yake ya biashara, alitoweka hadi mwili wake ulivyopatikana.

Baada ya kutoweka, madereva wenzake, mmiliki wa bajaji hiyo na familia ilisambaza taarifa maeneo mbalimbali pamoja na kutoa taarifa polisi ambao waliwakamata washitakiwa Julai 2, 2019 siku mwili ulipogundulika.

Washitakiwa hao walikamatwa ‘red handed’ wakitafuta mteja wa pikipiki ambayo walikuwa wameipora kutoka kwa marehemu na baada ya polisi kukamilisha upelelezi, waliwafikisha mahakamani wakikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia.

Ushahidi wa Jamhuri

Jaji Mwanga alisema katika kesi hiyo, ushahidi wa Jamhuri uliegemea ushahidi wa kukutwa na mali ya marehemu kwa kuwa hakuna shahidi aliyeshuhudia washitakiwa wakimuua marehemu na kuondoka na bajaji aliyokuwa akiiendesha.

Lakini, katika kesi hiyo, shahidi wa kwanza, wa tatu na wa tia waliithibitishia mahakama kuwa Julai 2, 2019 walikutana na washitakiwa eneo la Big Brother kwa lengo la mauziano ya bajaji yenye namba MC 847 BWE iliyokuwa ya marehemu.

Shahidi wa tisa alitoa ushauri kuwa waende eneo la Kilimani, ambalo ni umbali wa kilometa mbili kutoka Big Brother kwa ajili ya kufanya biashara hiyo na huko Kilimani ndiko ambapo washitakiwa katika kesi hiyo walikuwa wamejificha.

Kulingana na shahidi huyo, yeye na wenzake walifanikiwa kuwakamata washitakiwa na katika mahojiano ya mdomo walikiri pikipiki hiyo ni ya wizi ambapo washitakiwa walitia saini hati ya ukamataji wa bajaji hiyo.

Shahidi wa pili, Victoria Nyoni, alieleza kuwa yeye ndio mmiliki wa pikipiki hiyo na kwamba Juni 26,2019 alimkabidhi Omary Yahaya (marehemu) ili kuiendesha, lakini baada ya wiki moja alitoweka na taarifa za kutoweka kwake aliletewa na mke wa marehemu.

Mbali na ushahidi huo, lakini shahidi wa sita, alieleza kuwa Julai 2,2019 alipokea taarifa ya uwepo wa mwili wa marehemu wa mtu eneo la Malindi na baada ya upelelezi ilibainika ni wa Omary Yahaya ambaye ni dereva wa bajaji hiyo.

Jaji alisema utetezi wa washitakiwa kuwa wao walikuwa abiria tu umezidiwa nguvu na ushahidi wa shahidi wa tisa wa Jamhuri, ambaye alitoa wazo kwao kuwa waendele eneo la Kilometa mbili kutoka Big Brother ili wakafanye biashara.

Je, walikuwa na nia ovu

Jaji Mwanga alisema hoja ya mwisho ambayo mahakama yake inapaswa kuamua ni kama washitakiwa walisababisha kifo cha marehemu wakiwa na nia ovu.

Kuliamua hilo, Jaji alisema hakuna ubishi washitakiwa walikutwa na bajaji iliyokuwa ikiendeshwa na marehemu saa chache baada ya kifo chake na walishindwa kutoa maelezo yenye mashiko ya kwanini iko mikononi mwao.

Badala yake, Jaji akasema marehemu alikutwa ameuawa akiwa na majeraha mengi mwilini, jambo ambalo ni uthibitisho wa dhahiri kuwa washitakiwa walinuia ama kumsababishia umauti au kumpa majeraha mabaya mwilini.

“Hakuna uhalali wowote wa kumfanyia hivyo marehemu. Tabia kama hizo haziwezi kuvumilika katika Jamii iliyostaarabika. Kwa hayo niliyoyaeleza ni wazi washitakiwa walimuua marehemu wakiwa na nia ovu,” alieleza Jaji Mwanga.

Kutokana na uchambuzi huo wa ushahidi, Jaji alisema ameridhika kuwa upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha shitaka hilo pasipo kuacha mashaka kuwa washitakiwa hao ndio waliofanya mauaji hayo na hakuna mtu mwingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *