Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimetangaza kuwa kesho, Mei 3, 2025, kitaanzisha kamati maalumu itakayoratibu maombi yao ya kutaka kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya kisheria, haki na utawala bora.
Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, amesema kwamba uundwaji wa kamati hiyo ni hatua ya kistaarabu katika kutafuta majibu ya changamoto zinazolalamikiwa nchini.
Akizungumza leo Ijumaa, Mei 2, 2025, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya TLS jijini Dar es Salaam, Mwabukusi amesema kamati itakayoundwa itajumuisha viongozi waandamizi wastaafu wa Serikali, wakiwemo mawaziri na wazee mashuhuri waliowahi kulitumikia Taifa katika nafasi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, uamuzi wa kuhusisha wazee hao ndani ya kamati maalumu unalenga kuongeza uzito na msukumo wa kupokelewa haraka na Rais Samia Suluhu Hassan, ili wakutane naye na kujadili kwa kina changamoto mbalimbali, kwa lengo la kufikia suluhu mapema.
Hata hivyo, kabla ya kufikia hatua ya kuonana na Rais, Mwabukusi amesema kamati hiyo itaanza kupitia na kuchambua kwa kina masuala yote yanayohusu utawala bora na haki za binadamu nchini.

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Mei 2, 2025. Picha na Sunday George
Aidha, ametumia jukwaa hilo kulaani tukio la kushambuliwa kwa wafuasi wa Chadema na askari wa Jeshi la Polisi, waliokwenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Aprili 24, 2025, kwa ajili ya kusikiliza kesi ya Mwenyekiti wao, Tundu Lissu.
Amesema kitendo cha kupigwa kwa wafuasi hao ni ukiukaji wa haki za msingi zilizoainishwa na kulindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kudhalilisha hadhi ya taasisi za mahakama nchini.
Kwa mujibu wa Mwabukusi, tukio hilo limevunja haki ya usawa mbele ya sheria, uhuru wa mtu binafsi, uhuru wa kutembea na kwenda atakako, pamoja na kuwa kinyume na masharti ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Kutokana na hali hiyo, amesema TLS itasimamia na kuratibu hatua za kisheria dhidi ya wote waliohusika au kuonekana kushiriki katika uvunjaji huo wa haki, ili kuhakikisha wahanga wote wanapata haki yao kwa mujibu wa sheria.
“Tunawasihi wahanga wote waliopo Dar es Salaam kujitokeza na kufika TLS ili tufanye tathmini ya hatua stahiki za kuchukuliwa, pamoja na kutafuta njia bora za kuwawajibisha askari na wote waliohusika au kuratibu tukio hilo batili,” amesema Mwabukusi.
Pia, ameongeza kuwa chama hicho kitaandaa kongamano la kitaifa litakalowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia, mahakama, Jeshi la Polisi na vyama vya siasa, kwa lengo la kujadili na kuhimiza uwajibikaji wa vyombo vya dola na mamlaka za Serikali katika kulinda haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
Kuhusu tukio la kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, Mwabukusi amelitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka dhidi ya waliohusika, ili wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, ubalozi wa Marekani umetoa tamko kuhusu kushambuliwa kwa Padri Kitima ukisema, “tunaungana na Watanzania na kutoka kila upande wa kisiasa kumuombea apone kabisa.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Mei 2, 2025. Kulia ni Wakili Ipilinga Panya na (kushoto) Wakili Reginald Shirima. Picha na Sunday George
Ubalozi huo umelaani tukio hilo na vitendo vyote vya ukatili, hasa vinavyolenga kunyamazisha wito wa haki, maridhiano, na haki za binadamu.
“Tunatumaini kuwa Tanzania itautumia wakati huu kutafuta haki kupitia uchunguzi wa haraka na wa wazi. Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia, Katibu wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Eliud Mvela, naye ameungana na wadau mbalimbali kulaani tukio la kushambuliwa kwa Kitima, akieleza kuwa kitendo hicho ni tishio kwa amani ya Taifa.
“Watu wanaojihusisha na vitendo vya aina hii ni maadui wa maendeleo na wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema Diwani Mvela.
Ameongeza kuwa ni jukumu la kila mwananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa muhimu zitakazowezesha kuwakamata na kuwawajibisha wahusika wa tukio hilo haraka.
“Tunaomba wananchi wawe waangalifu na waendelee kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuhakikisha wahalifu wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” amesisitiza Diwani Eliud Mvela.
Aidha, Mvela ametumia nafasi hiyo kutoa pole kwa familia ya Padri Kitima na TEC, kutokana na tukio la kushambuliwa kwa kiongozi wao.
“Watu wanaojihusisha na vitendo vya namna hii ni maadui wa amani na maendeleo ya nchi, hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria bila kuonewa huruma,” ameongeza.