
Dar es Salaam. Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimeshtushwa na taarifa za kushambuliwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima.
Kutokana na tukio hilo, CCM imetoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na haraka ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali wahusika wa tukio hilo.
Dk Kitima ambaye amelezwa Hospitali ya Aga Khan ameshambuliwa jana usiku Aprili 30, 2025 Kurasini Dar es Salaam, zilipo ofisi za Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Tanzania..
Tayari TEC imetoa taarifa kuhusu tukio hilo, huku ikilitaka Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama kuharakisha uchunguzi wa tukio hilo na kuwabaini pamoja na kuwakamata wahusika.
Jeshi la Polisi kupitia taarifa iliyoitoa kwa umma ikisainiwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, limesema tayari mtu mmoja amekamatwa na uchunguzi unaendelea kuwabaini wahusika.
“CCM imepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk Charles Kitima, tukio lililotokea usiku wa Aprili 30, 2025, katika eneo la Kurasini, Dar es Salaam,” imeeleza taarifa iliyotolewa leo ya CCM na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi.
CCM imesema inaungana na taarifa iliyotolewa awali na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira kulaani vikali kitendo hicho cha kikatili na kisicho na utu dhidi ya kiongozi wa dini ambaye amejitolea maisha yake kuhudumia jamii kwa upendo na uadilifu.
“Aidha, CCM inatoa pole kwa Padri Dk Charles Kitima, familia yake, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, na waumini wote wa Kanisa Katoliki kwa mshtuko na maumivu yaliyosababishwa na tukio hili.
Tunamuombea Padri Kitima uponaji wa haraka na kurejea katika majukumu yake ya kiroho na kijamii,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CCM itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini katika kujenga taifa lenye kulinda na kuendeleza misingi ya amani, umoja wa kitaifa, mshikamano, heshima na linaloheshimu haki za binadamu.