
Huduma za mikopo ya kidijitali zimeleta mapinduzi katika upatikanaji wa mikopo, kwa kurahisisha mchakato hadi kufikia hatua ambapo mkopaji anaweza kupata fedha ndani ya sekunde kupitia simu ya mkononi bila kujaza fomu, kusimama kwenye foleni, wala kutoa dhamana.
Hali hii huwapa watumiaji ahueni ya haraka, hasa wanapokuwa na mahitaji ya dharura. Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuongeza uwazi kuhusu gharama halisi za ukopaji katika huduma hizi, ili kuwawezesha watumiaji wa huduma za kifedha kufanya maamuzi sahihi, yenye taarifa kamili, na kwa umakini unaostahili.
Mikopo ya mtandaoni ni mikopo inayotolewa na kulipwa kupitia majukwaa ya kidijitali, hususan kwa kutumia huduma za kifedha zinazotolewa na kampuni za mawasiliano ya simu au watoa huduma wengine kama vile makampuni ya malipo na majukwaa ya simu janja (aplikesheni).
Mikopo hii haitaki dhamana za kawaida; mara nyingi hutolewa kwa kuzingatia rekodi za miamala ya mtumiaji, muda wa maongezi, au hata kitambulisho cha taifa (NIDA) kinaweza kutosha kukudhamini.
Mfumo huu umepata umaarufu mkubwa nchini, hasa kwa kuwa idadi ya watumiaji wa simu za mkononi ni kubwa. Unaweza kusema, huduma hizi zimekuwa suluhisho la kifedha kwa makundi yaliyo nje ya mfumo rasmi wa kifedha.
Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania kuhusu Mifumo ya Malipo ya Taifa kwa mwaka 2024 inaonesha kuwa thamani ya miamala ya mikopo ya kidijitali iliongezeka kufikia Sh4.2 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 91.49 ikilinganishwa na mwaka 2023.
Takwimu hizi zinaashiria kuwa idadi ya Watanzania wanaotumia majukwaa ya kidijitali kupata mikopo inaendelea kuongezeka. Sababu kubwa ya ongezeko hili huenda ni urahisi wa upatikanaji wa mikopo hiyo, hasa ikilinganishwa na taratibu za mikopo katika taasisi za fedha za kawaida.
Hata hivyo, kwa kadiri sekta inavyokua ndio changamoto hujitokeza, na katika hili changamoto inajitokeza kwanza, kwa baadhi ya watoa mikopo wanaoendesha shughuli zao nje ya mfumo rasmi wa usimamizi wa huduma za kifedha, kwa mtazamo wa kulinda haki za mtumiaji huduma za kifedha, jambo hili linatia mashaka katika uzingatiaji wa haki za mtumiaji wa huduma hizo.
Kwa mfano, watoa mikopo wanaodhibitiwa na mamlaka husika hulazimika kufuata miongozo inayohakikisha uwazi wa bei, kama vile kuweka kiwango cha riba kisichozidi kiasi fulani.
Hata hivyo, inapokuwa mtoa huduma wa mikopo ya mtandaoni ambaye hajulikani au anayetambulika kama vile makampuni ya huduma za mawasiliano yanayotoa mikopo, hana mwongozo wa kisheria wa kufuata. Hali hii inampa uwezo wa kujipangia gharama yoyote atakayoona inafaa, jambo ambalo linaweza kusababisha kutoza riba kubwa na kuathiri watumiaji wa huduma hizo.
Ukosefu wa uwazi kuhusu masharti ya utoaji na urejeshaji wa mikopo ni changamoto nyingine katika huduma hizi. Ni muhimu masharti ya urejeshaji yawekwe wazi ili mteja ajue ni lini anatakiwa kulipa, ni gharama zipi za ziada atakazobeba endapo atachelewesha, na iwapo kiasi atakachopokea au salio lake kwenye simu kitakatwa moja kwa moja kufidia mkopo.
Wakati mwingine watumiaji huichukulia huduma hii kama huduma ya kawaida ya kifedha, bila kutambua kuwa ni mkopo unaobeba wajibu na makubaliano. Hivyo, ni lazima masharti yote yawekwe wazi kwa mteja kabla ya kukopa, mkopo inabidi iwe ni ridhaa yenye taarifa (informed consent).
Jambo lingine la wasiwasi ni mbinu zisizo na staha za ukusanyaji madeni zinazotumiwa na baadhi ya watoa mikopo mtandaoni na hii imeenea zaidi kwenye majukwaa yanayotoa mikopo kupitia programu za simu aplikeshini za mikopo. Utumaji wa ujumbe wa mara kwa mara, vitisho au kuvunja heshima ya mkopaji, pia kusambaza taarifa binafsi; jina, namba ya NIDA, huyu tunamdai, na mengine, linalokiuka hata haki ya ulinzi wa taarifa binafsi za mkopaji.
Kutokana na hayo, naona kuna umuhimu wa kuweka kanuni maalumu zitakazowaongoza watoa huduma zote za mikopo ya mtandaoni chini ya mfumo wa usimamizi rasmi, bila kuathiri urahisi na kasi ya upatikanaji wa huduma hizo.
Pia usajili wa watoa huduma wote wa mikopo ya kidijitali unapaswa kuwa wa lazima, kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watumiaji wa huduma za kifedha. Wakopaji wapewe taarifa kamili na kwa uwazi kuhusu viwango vya riba, ada mbalimbali, ratiba za marejesho, pamoja na athari zitokanazo na ucheleweshaji wa malipo.