Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, ameibua wasiwasi kuhusu hali ya uwanja utakaotumika katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Europa Conference League dhidi ya wapinzani wao Djurgarden.

Chelsea itakuwa kwenye Uwanja wa 3Arena, jijini Stockholm usiku wa leo kuivaa Djurgarden ambapo Enzo Maresca, ameeleza hofu yake kuhusu uwezekano wa wachezaji wake kuumia kutokana na kucheza kwenye uwanja huo uliotengenezwa na nyasi bandia.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mechi, Maresca amesema amefuatilia mechi sita za wapinzani wao na kugundua kuwa hata baadhi ya wachezaji wa Djurgarden hawaridhishwi na ubora wa uwanja huo.
“Ni hali tofauti kabisa. Najua kwamba wiki zilizopita baadhi ya wachezaji wao walikuwa wakilalamikia ubora wa uwanja huu. Hii si hali tuliyozoea,” amesema Maresca.

Kocha huyo mzawa wa Italia amesema licha ya wasiwasi wake juu ya uwezekano wa wachezaji wake kuumia, hana mpango wa kuwapumzisha nyota wake kwa ajili ya mechi ya EPL dhidi ya Liverpool.
“Bila shaka, kuna hofu ya majeruhi. Lakini hii ni nusu fainali ya mashindano ya Ulaya. Hatuna nafasi ya kupumzisha wachezaji. Lengo letu ni kufika fainali,” amesema kocha huyo.
Chelsea, ambayo inawania kumaliza ndani ya nafasi tano bora za Ligi Kuu England, inakabiliwa na ratiba ngumu huku pia ikiweka macho kwenye mchezo mkubwa dhidi ya Liverpool utakaofanyika siku ya Jumapili kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Kwa upande wa Djurgarden wao wanakabiliwa na changamoto ya wimbi la mafua kwa baadhi ya wachezaji wao huku mwenyekiti wao, Lars-Erik Sjoberg akijiuzulu kufuatiwa na tuhuma za kauli za kibaguzi mitandaoni.
Chelsea inahitaji matokeo chanya kwenye mchezo huu wa ugenini kabla ya kurudi nyumbani wiki ijayo, ikiwa na matarajio ya kuandika historia mpya kwenye michuano hii ya Conference League.