Singida. Shirika la Kazi Duniani (ILO) limetaja mageuzi ya kiteknolojia, ujio wa Akili Mnemba (AI), mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la idadi ya watu kuwa ni miongoni mwa changamoto zinazotishia ustawi wa ajira, uchumi na nishati duniani.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei Mosi, 2025, katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, na Mkurugenzi wa ILO nchini Tanzania, Caroline Mugalla, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert Houngbo.
Mugalla ametaja athari za changamoto hizo kuwa ni pamoja na kubadilishwa sekta nyingi duniani, kuhitaji ujuzi mpya ili kuendana na soko la ajira, kuongezeka migogoro ya kisiasa, kuvuruga mnyororo wa usambazaji na kupungua rasilimali za kimataifa kwa ajili ya msaada wa maendeleo endelevu.

“Katika kukabiliana na changamoto hizo, ILO imeanzisha mikakati ikiwemo ‘Muungano wa kimataifa wa haki za kijamii’ na ‘kichocheo cha dunia cha ajira na ulinzi wa mpito wa kijamii’ yenye lengo la kuendeleza mshikamano, ubunifu na mustakabali wa kazi utakaohimili changamoto hizo,” amesema.
Amesema kupitia mikakati hiyo, ILO imewawezesha wanawake na vijana kiuchumi kupitia ushirikiano na taasisi za fedha kama vile Benki ya NMB, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na zisizo za kifedha hususan kwenye biashara.
“Kupitia mpango wa pamoja wa umoja wa mataifa (UN) na ushirikiano na Serikali mkoani Kigoma na Baraza la Taifa la Uwezeshaji, maelfu ya wanawake na vijana wajasiriamali (bila kutaja idadi) wamepata fursa mpya,” amesema Mugalla.
Pia amesema imehitimisha utafiti kuhusu sekta isiyo rasmi na kuzindua programu ya simu na mwongozo wa usajili wa biashara unaowaunganisha wajasiriamali na mifumo ya Serikali ya usajili wa biashara itakayowawezesha kuingia kwenye mfumo wa kiuchumi nchini.

Katika hatua nyingine, Mugalla amesema ILO pia imetoa msaada wa kitaalamu kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ikiwa ni pamoja na tathmini za hesabu za kifedha ili kuimarisha dhamira ya Tanzania katika kufanikisha bima ya afya kwa wote.
“Tumeendelea kushirikiana na taasisi za kitaifa kama Mahakama ya Kazi ya Tanzania na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ili kuboresha uwezo wao wa kutatua migogoro ya kazi kwa kufuata viwango vya kazi vya kimataifa na kuendeleza mazingira bora ya kazi yenye mshikamano na tija,” amesema.
Mbali na hilo, Mugalla uimarishaji wa mifumo ya afya na usalama kazini ikiwemo uundaji wa mifumo bora ya taarifa kuhusu ajali na matukio ya kazi kuwa ni miongoni mwa mikakati ya kulinda maisha ya wafanyakazi na biashara zenye uwezo wa kustahimili changamoto.
“Wafanyakazi, waajiri, Serikali na wadau wanapaswa kushikamana ili kuhakikisha kuwa haki ya kijamii haibaki kuwa ndoto bali inakuwa hali halisi ya maisha kwa kila mfanyakazi nchini Tanzania na kwingineko. ILO itaiunga mkono Tanzania katika safari hii ya maendeleo, heshima na matumaini,” amesema Mugalla.
Chimbuko la Mei Mosi
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), ‘Siku ya Wafanyakazi’ huazimishwa kote duniani ikilenga kukumbuka mapambano ya kihistoria na maendeleo yaliyofanywa na wafanyakazi kwa lengo la kudai mazingira bora ya kazi na nguvu ya muungano.
Awali, siku hii iliadhimishwa na mashirika mbalimbali ya Kikomunisti na vikundi vya wafanyakazi ambapo mwaka 1886, vyama vya wafanyakazi nchini Marekani vilianzisha mgomo wa watu wengi kudai kufanya kazi saa nane tu kwa siku, kwa kuzingatia wazo la mwanamageuzi wa kijamii wa Uingereza, Robert Owen.

Robert Owen
Owen aliandaa lengo la siku ya kazi ya saa nane na kauli mbiu “saa nane za kazi, saa nane za kucheza, saa nane za kupumzika.”
Maandamano hayo makubwa yalifanyika mjini Chicago Mei 1, 1886 na kuhudhuriwa na wafanyakazi zaidi ya 40,000.
Wakati huo, ilikuwa kawaida kufanya kazi nzito katika viwanda, bila kujali saa ngapi za kazi ama siku za kupumzika.
Katika siku zilizofuatia, maandamano hayo ambayo hayakutazamwa vyema na wachumi na wanasiasa yaliungwa mkono na maandamano mengine ya maelfu ya wafanyakazi wengine wasio na uwezo na watawala.
Hali ngumu ya kufanya kazi, mshahara mdogo na Saa ndefu za kufanya kazi haraka yalisababisha wafanyakazi nchini Serbia nao kuandaa mkutano wa Siku ya Mei 1, 1893. Tangu hapo siku hii imekuwa ikisherehekewa kote duniani.