
Dar es Salaam. Ingawa simu za mkononi na mitandao ya kijamii ni nyenzo muhimu za kupata taarifa, kwa upande mwingine, zinakuweka katika hatari ya kupata msongo wa mawazo, upweke, matatizo ya umakini na hatimaye changamoto ya afya ya akili.
Kwa taarifa yako, kadri unavyohisi raha ya kuperuzi katika mitandao ya kijamii kupindukia, ndivyo unavyojiweka karibu na hatari ya ustawi wa kisaikolojia, kama inavyoelezwa na wabobezi wa afya ya akili.
Ukiacha mtazamo wa wanazuoni, hoja hiyo inathibitishwa na ripoti ya uraibu wa matumizi ya simu janja iliyotolewa na Kampuni ya SlickText, Machi 6, 2025, ikionyesha mtu wa kawaida hufungua simu yake wastani wa mara 150 kwa siku.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, matumizi huongezeka zaidi kwa wafanyakazi ambao kila siku wanatumia kati ya programu na tovuti mara 1,200, hali inayoufanya ubongo kuwa katika msongo wa mara kwa mara.
Ripoti hiyo pia imebainisha asilimia 60 ya watumiaji wa mitandao ya kijamii na simu janja wana dalili za ‘nomophobia’, hali ya kiakili inayojitokeza kwa hofu ya kukosa simu ya mkononi.
Katika kipindi hiki ambacho dunia inaadhimisha mwezi wa uhamasishaji wa afya ya akili, wanataaluma wa kada hiyo wamesisitiza kuwa kitendo hicho kinasababisha msongo wa mawazo, upweke, matatizo ya umakini na utegemezi wa kidijitali.
Tabia hizo za kidijitali zimehusishwa na kuongezeka kwa msongo wa mawazo na wasiwasi, huku wengi wakijikuta wakitumbukia katika ulimwengu wa kulinganisha maisha yao na ya wengine, kupoteza muda na kujitenga kijamii.
“Tabia hii ya kuhamahama kila mara kati ya maudhui ya kidijitali inaumiza sana afya zetu za akili na kupunguza tija kazini,” amesema Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Mental Health Africa, Glory Livingstone.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 30, 2025, Glory amesema ni rahisi mtu kujikuta akitumbukia katika ufuatiliaji wa maisha ya wengine kwenye mitandao, huku akipuuzia afya yake ya akili.
Dalili kama hofu ya kukosa taarifa mtandaoni na tabia ya kuangalia simu kila mara, amesema zinaweza kuwa ishara ya changamoto za kisaikolojia.
“Katika dunia ya sasa ya kidijitali, wengi wanahisi shinikizo la kuwa mtandaoni muda wote. Wako watu wanaokosa hata mlo, ili mradi tu waendelee kuwa na data, wengine huchukua mikopo ya vifurushi ili waendelee kuunganishwa,” amesema.
Hatari nyingine inayotokana na matumizi ya mitandao hiyo kupitiliza, kwa mujibu wa Glory, ni watu kulinganisha maisha yao na wengine, hasa wakiona wale wanaochapisha mafanikio na furaha pekee huku wakificha changamoto.
“Mitandao hutupa fursa ya kupata taarifa, elimu na hata ajira, lakini kama ilivyo kwa kila kitu chenye faida, teknolojia pia ina hasara zake, hasa upande wa afya ya akili na mahusiano ya kijamii,” amesisitiza.
Vijana wengi hujikuta wakiingia kwenye utegemezi wa simu au baadhi ya programu, kiasi cha kushindwa kuacha kuzitumia, kwa kuwa mitandao mingi hutumia mfumo wa algorithm ambao huwapa watumiaji maudhui wanayoangalia mara kwa mara, hivyo kuwafanya washindwe kuacha.
Kwa kadri unavyotumia mitandao hiyo kupita kiasi, Glory amesema, ndivyo unavyoathiri uwezo wa kuzingatia mambo, kupunguza umakini na uwezo wa kutatua matatizo ya kijamii kama kusikiliza kwa makini, huruma na kushughulikia migogoro.
Mbali na mtazamo wa Glory, mwanaharakati wa afya ya akili, Sunday Kapesi, amefananisha utegemezi wa simu na uraibu wa dawa za kulevya, akieleza kuwa mtu anaweza kuonyesha dalili kama kukosa usingizi, kushuka kwa hali ya kujiamini, kuepuka watu na hata kushindwa kudhibiti maisha yake.
“Kutazama skrini kwa muda mrefu ni hatari kwa afya ya akili. Tunahitaji kuanza kufuatilia muda wetu wa mtandaoni, kujiwekea mipaka na kuchagua kufanya shughuli za ubunifu au kijamii,” ameeleza.
Mkurugenzi Mtendaji wa TechForward Tanzania, Elias Patrick, amesisitiza haja ya hatua za kitaasisi na binafsi ili kukabiliana na hali hiyo.
Ametoa wito wa kuanzishwa kwa sheria zitakazolinda ustawi wa kidijitali, hasa kwa watumiaji walio chini ya miaka 18.
“Ni muhimu kuweka kikomo cha muda wa kutumia skrini kwa watoto na kuhakikisha kuna uthibitisho wa umri. Serikali inaweza kufadhili tafiti za kitaifa kuhusu athari za mitandao ya kijamii kwa afya ya akili,” amesema.
Amehimiza familia kuanzisha utaratibu wa kupunguza matumizi ya simu, hasa kabla ya kulala, na kuhimiza mazungumzo ya ana kwa ana, kuelimishana kuhusu thamani binafsi na ustahimilivu wa kihisia.
Kwa upande wa mtu binafsi, ameshauri watu kufuata kurasa za kuelimisha na kujipa moyo, na kuacha kurasa zinazoamsha hisia za kulinganisha au hofu.