Makalla: Simba, Yanga ni zaidi ya mpira, watu wasipangiwe

Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema Simba na Yanga ndizo klabu zinazopendwa zaidi nchini, hivyo asitokee mtu wala chama kinachotaka kuwabana Watanzania kuhusu wanachokipenda au kufikiria.

Makalla amesema mbali na kutoa burudani, amani, mshikamano na furaha, klabu hizo pia zinachangia kukuza na kutangaza utalii kupitia mashindano mbalimbali ya kimataifa kama Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kauli yake imekuja kana kwamba ni majibu kwa hoja ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche aliyedai kuwa Watanzania wamekuwa wakishabikia mpira, hasa klabu za Simba na Yanga  badala ya kujihusisha na siasa, ambayo ndiyo msingi wa kuboresha maisha yao.

Heche alitoa kauli hiyo Aprili 17, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Chamazi, wilayani Temeke.

Alisema; “Msipuuze siasa, ndiyo maisha yenu. Tumekuja kuwaomba mtuunge mkono kwenye kampeni ya No Reforms, No Election. Mko tayari kufa na kupona kwa ajili ya Simba na Yanga, lakini siyo kwa ajili ya siasa.”

Leo Jumatano, Aprili 30, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mandege, Temeke, Makalla amesema wapinzani kwa sasa hawana hoja, akidai kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya kazi nzuri ambayo inajieleza yenyewe.

“Wamekuja huku Temeke na hasira; badala ya kufanya kazi, wanabeza na kubeza upendo wa watu kwa Simba na Yanga. Hizo ni hasira na kejeli za kukosa watu katika mikutano yao ya hadhara,” amesema Makalla na kuongeza;

“Simba na Yanga ni timu zetu pendwa. Hakuna atakayetupangia tutakachokipenda. Rais Samia Suluhu Hassan amechangia mafanikio mengi kwenye michezo na kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba na Yanga.”

Makalla pia ameipongeza klabu ya Simba kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Stellenbosch FC katika mchezo uliochezwa Aprili 27, 2025, kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Afrika Kusini.

Amesema hata klabu ya Yanga Mei 2023 jana ilishaifikia hatua ingawa ilishindwa kutwaa kombe mbele ya USM Alger ya Algeria.

Katika mkutano huo, Makalla amesema;
“Tanzania ya leo imejaa furaha, Simba imetufikisha fainali. Hii ni fahari, siyo tu kwa mashabiki bali kwa taifa. Hizi timu hupunguza msongo wa mawazo na zinatupa furaha ya kitaifa. Wanasema tumekalia Simba na Yanga; hizi timu zinaitangaza Tanzania nje ya mipaka yetu.”

Amesema wapinzani wamefilisika hoja na amewaomba wananchi wa Dar es Salaam wasichukulie kwa uzito kauli zao za kejeli dhidi ya CCM.

Hoja ya CCM kudumu madarakani

Akizungumzia madai ya CCM kung’ang’ania madaraka, Makalla amesema kuwa chama hicho hakijiweki chenyewe madarakani, bali kinapewa ridhaa na wananchi kutokana na ufanisi wa Serikali yake.

“Ndiyo maana kila mwaka wa uchaguzi mnatuunga mkono kwa kura nyingi. Hongereni kwa imani hiyo,” amesema Makalla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Temeke, Dorothy Kilave amesema miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali imesaidia kutatua changamoto nyingi za wananchi, hivyo watampa tena kura nyingi Rais Samia Suluhu Hassan.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *