Madiwani waonywa kuchafuana kuelekea uchaguzi mkuu

Mbeya. Ikiwa imesalia miezi kadhaa kuelekea uchaguzi Mkuu Oktoba 2025, madiwani jijini Mbeya wametahadharishwa kuepuka kuchafuana na badala yake washikamane na kushirikiana kutatua changamoto katika maeneo yao.

Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Dourmohamed Issa amesema hayo leo Jumatano Aprili 30, 2025 alipokuwa akifunga kikao cha Baraza la Madiwani cha kupitia taarifa za kamati mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Issa amesema kipindi hiki si  vyema kusemana vibaya bali wanapaswa kuwa wamoja na kama kuna changamoto washirikishane kuzitatua ili kwenda pamoja.

“Madiwani wenzangu ,tunapaswa kushirikiana na kurejea kwa wananchi kufanya mikutano ya hadhara kueleza nini Serikali imefanya kwa kipindi cha miaka mitano ,”amesema.

Amesema lengo ni kuwajulisha wananchi mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika miradi ya maendeleo na sio kusubiri wakati wa kuomba kura ndio tuwaeleze.

Kuhusu makusanyo ya mapato ya ndani , Issa amesema kwa kipindi cha mwaka 2024/25,wamevuka malengo ya ukusanyaji kutoka Sh20.6 bilioni mpaka Sh21.9 bilioni, akifafanua kuwa  mafanikio hayo ni kutokana na ushirikiano wa madiwani na watendaji wa Serikali.

Amesema mafanikio hayo yamewezesha Jiji hilo kutekeleza miradi mbalimbali ya sekta elimu, afya na uboreshaji wa miundombinu ya barabara pamoja na shule chakavu kwa kutumia mapato ya ndani.

Katika hatua nyingine amesema kuwa  wametumia zaidi ya Sh1.3 bilioni,  kujenga kiwanda cha mbogamboga, kufanya ukarabati wa shule kongwe 154 , ujenzi wa matundu ya vyo 400 kati ya 900 kwa thamani ya Sh1.1 bilioni.

Issa ametaja miradi mingine ni kujenga jengo la dharura la wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igawilo ikiwemo miundombinu ya ofisi za Serikali ngazi za kata ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa jamii.

“Yote yamefanikiwa kwa ushirikiano wetu madiwani , sasa tumebakiwa na muda mchache niwaombe kila mmoja arejee kwa wananchi kufanya mikutano ya hadhara kuyasema haya,”amesema.

Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Mbeya, Nyambaza Christopher amewataka madiwani kwenda kuboresha taarifa zao katika daftari la mpigakura ambapo kwa Jiji la Mbeya wanaanza kesho Mei Mosi mpaka saba mwaka huu.

Pia amewataka kutoa elimu hiyo kwa wananchi wao ili kila mmoja awe na kibali cha kushiriki uchaguzi.

Katibu Tawala Wilaya ya Mbeya, Devotha Chacha ameungana na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya , kuwataka madiwani kurejea kwa wananchi kufanya mikutano ya hadhara ili wajue mambo makubwa yaliyofanywa na Serikali.

Diwani Kata ya Mbalizi Road, Adam Simbaya amesema wamepokea maelekezo na kwamba suala la mikutano linaeleweka lengo ni kuwajulisha wananchi nini kimetekelezwa na Serikali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *