
Tangu vuguvugu la waasi la AFC-M23 wakisaidiwa na Kigali kuchukuwa udhibiti wa mji wa Goma nchini Kongo, wanajeshi wa Kongo na maafisa wa polisi walikimbilia katika kambi ya kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini DRC, MONUSCO. Miezi mitatu baadaye, zoezi la kuwahamisha wanajeshi hawa limeanza siku ya Jumatano, Aprili 30, zoezi ambalo limesimamiwa na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC). Lakini hii hufanyika katika hali ya kutoaminiana kati ya wahusika.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na RFI, karibu wanajeshi na maafisa wa polisi 1,400 wanahamishwa: wengi wao wakiwa wanajeshi, lakini pia maafisa wa polisi na familia zao. Hakuna wapiganaji wa Wazalendo katika msafara huu, makundi yanayounga mkono jeshi la Kongo.
Wote walikuwa wamekimbilia katika kambi ya tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini DRC (MONUSCO) kwenye uwanja wa ndege wa Goma, baada ya kuanguka kwa mji huo mikononi mwa waasi wa AFC-M23 mwishoni mwa mwezi wa Januari. Zaidi ya watu 3,000 walikimbilia katika kambi hiyo.
Uhamisho wa sasa ni wa hiari, salama, na unatawaliwa na makubaliano yaliyotiwa saini na pande nne: serikali ya Kongo, AFC/M23, MONUSCO na ICRC. Kwa mujibu wa taarifa zetu, operesheni hiyo inatarajiwa kudumu takribani siku kumi, huku kila moja ikiwa na misafara ya watu takriban 130. Uhamisho huo haupitii kwenye uwanja wa ndege wa Goma, ambao bado haufanyi kazi.
Misafara hiyo inaondoka Goma kwa njia ya barabara, kisha kusafirishwa kwa helikopta hadi uwanja wa ndege wa Mavivi, karibu na Beni, na kisha kupelekwa Kinshasa, kutokana na usaidizi wa vifaa kutoka ICRC.
Masharti yaliyowekwa na AFC/M23
Kuhamishwa kwa kundi hili hadi Kinshasa pia kunakidhi masharti yaliyowekwa na AFC/M23 kwa ajili ya kufungua tena uwanja wa ndege wa Goma: kuondoka kwa wanajeshi wa Kongo ambao bado wapo katika kambi ya Umoja wa Mataifa.
Operesheni hiyo inafanyika chini ya uangalizi wa hali ya juu, katika hali ya wasiwasi, lakini kwa idhini ya watu wote waliohamishwa, kwa mujibu wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu, pande zote zinaelezea.
Katika taarifa yake huko Goma, mkuu wa ujumbe wa ICRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Myriam Favier, amesema kuwa shirika lake liliombwa “kuwa kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote.”
ICRC iliombwa na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Wizara ya Ulinzi ya Kongo, MONUSCO na waasi wa AFC-M23, kufanya kazi kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote. ICRC haiweki masharti ya mazungumzo, lakini inatoa ofisi zake nzuri ili kuwezesha utekelezaji wa operesheni. Chini ya makubaliano yaliyohitimishwa na ICRC, pande zinazohusika zimejitolea kuhakikisha usalama wa watu katika misafara na kufanya kazi ili kufanikisha operesheni hiyo. ICRC pia imehakikisha kwamba watu wote walikubali kujumuishwa katika usafiri huu.