
Mwanza. Katika hali ya kushangaza, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Nyakabungo wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza, Edward Bihemo (43) amepoteza Sh12.47 milioni katika jaribio la kusaka utajiri, baada ya kutapeliwa na mganga wa kienyeji aliyemuahidi kuzalisha fedha kwa njia ya miujiza.
Akitoa taarifa ya tukio hilo leo Jumatano Aprili 30,2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema jeshi hilo limemkamata Edward Kumalija (38) ambaye ni mganga wa tiba asili mkazi wa Nyamhongolo Wilaya ya Ilemela kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mwalimu huyo.
Mganga huyo ambaye pia ni mmiliki wa nyumba ya kulala wageni alikamatwa Aprili 18, 2025 saa 7:30 mchana katika Mtaa wa Shamaliwa Kata ya Igoma Wilaya ya Nyamagana, Mwanza pamoja na mshirika wake kwenye utapeli huo, Boniphace Antony (33).
Mutafungwa amesema chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kupata utajiri, ambapo mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kwa kumlaghai Edward Bihemo (mwalimu) kupitia kazi yake ya uganga wa tiba asili kuwa ana uwezo wa kuzalisha fedha kwa njia ya miujiza.
“Mtuhumiwa alikuwa akichukua fedha hizo na kuziweka katika begi lake na kumuamuru mwalimu huyo awe anazitolea sadaka mara kwa mara ili ziongezeke, aliendelea kutoa sadaka hizo kwa muda mrefu hadi kufikia hatua ya kukosa fedha ya kujikimu,” amesema Mutafungwa
Ameongeza kuwa; “Baada ya kuishiwa fedha za kujikimu aliamua kwenda kwa mtuhumiwa huyo kwa lengo la kuchukua fedha alizowekeza, ndipo alipogundua kuwa alikuwa ametapeliwa. “Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na watuhumiwa watachukuliwa hatua za kisheria.”
Katika tukio lingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kutengeneza pombe kali bandia na kuziweka kwenye vifungashio vya nembo ya biashara ya pombe kali maarufu, pamoja na kukutwa na vifaa mbalimbali walivyokuwa wakitumia kutengeneza pombe hiyo.
Watuhumiwa hao ni Johnson John (26) mjasiriamali na Chacha Geswa (28) mwendesha pikipiki (bodaboda) wote wakazi wa jijini Mwanza ambao walikamatwa Aprili 24, 2025 saa 7:30 mchana katika mtaa wa Ihangiro, Nyakato wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza.
Mutafungwa amesema baada ya watuhumiwa hao kukamatwa jeshi hilo lilifanya msako katika nyumba waliyokuwa wakitengenezea pombe hizo na kufanikiwa kukamata vifaa mbalimbali ikiwemo kimiminika, kinachodhaniwa ni dawa ya kuchanganya kwenye pombe hizo.
“Tulikamata stemp bandia 1,318 za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), madiaba mawili ya kuchanganyia pombe na chupa tatu pombe kali aina mbalimbali zikiwa kwenye magunia saba. Watuhumiwa wanahojiwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani,” amesema Mutafungwa
Mutafungwa ametoa wito kwa wananchi kuacha kufanya vitendo kinyume na sheria kwani kufanya hivyo ni kosa, huku akiwataka wananchi kuendelea kufichua taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria ziendelee kuchukuliwa kwa haraka dhidi yao.