
Dar/Mikoani. Katika kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi), 2025, wafanyakazi wamepaza sauti wakihitaji mishahara bora, ulinzi wa kisheria na ufuatiliaji wa haki kazini, kupambana na rushwa na kuwapo udhibiti katika sekta binafsi.
Maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa yatafanyika mkoani Singida yakiwa na kaulimbiu isemayo: ‘Uchaguzi Mkuu 2025: Utuletee viongozi wanaojali haki na masilahi ya wafanyakazi, sote tushiriki.’
Wakati wafanyakazi wakieleza hayo, mjumbe mwandamizi wa Umoja wa Maofisa Waajiri, Peter Mapigano amesema katika ajira, kila upande una wajibu wake wa kutekeleza.
Amesema mwajiri anawajibika kumpa kazi mwajiriwa, kumheshimu, kumsikiliza na kumlipa kutokana na anachozalisha. Pia, kumuhusisha kwenye uamuzi wa taasisi.
Mwajiriwa anawajibika kutumia uwezo alionao kuzalisha, akieleza kuwa katika hali ya sasa mfanyakazi anajilipa kutokana na anachozalisha.
Katika maadhimisho ya Mei Mosi, amesema wafanyakazi wanapopaza sauti kudai haki, wakumbuke pia wajibu wao wawapo kazini.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Aprili 30, 2025, baadhi ya watumishi wa umma na binafsi wamelalamikia mishahara midogo isiyoendana na gharama halisi za maisha, hivyo wanatarajia kupata nyongeza.
Mtumishi katika sekta ya afya mkoani Shinyanga, ofisa muuguzi msaidizi Mwanzenu Mbaluku amesema masilahi ya watumishi yaongezwe.
Baadhi ya watumishi wa umma, wakiwamo walimu, wameibua kilio cha kurejeshewa posho ya kufundishia wakidai ni haki yao, wengine wakilalamikia kodi inayokatwa kwenye mishahara, wakieleza kuwa inawaumiza, kwani inachangia ugumu wa maisha.
Mwalimu Edward Lutabu amependekeza Serikali irejeshe malipo ya ziada kwa walimu (posho ya kufundishia) iliyofutwa katika uongozi wa awamu ya nne.
Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Mbeya, Judith Mengi amesema kwa miaka mingi walimu kilio chao ni mishahara na mazingira bora ya utumishi, kwani miundombinu ya sekta ya elimu haina changamoto.
Mbali na hayo, waajiri wanalalamikiwa kwa kushindwa kuwasilisha michango ya hifadhi ya jamii, licha ya kufanya makato kwenye mishahara ya wafanyakazi.
Angelina Chikoko anayefanya kazi katika kampuni ya vifaa vya ujenzi iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam, amesema ni wakati sasa sekta binafsi itupiwe jicho la ziada, akidai watumishi wanaumia kwa sababu baadhi ya maofisa wa mamlaka husika wameendekeza rushwa na kuacha kutetea masilahi ya wafanyakazi.
“Katika sekta hizo, ukiacha kulipwa mishahara kwa wakati, wengi wa wafanyakazi hawapelekewi michango yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kwa miaka mingi. Licha ya changamoto hiyo kujulikana, bado haifanyiwi kazi. Mwishowe wanaoumia ni wafanyakazi,” amesema.
Yapo pia malalamiko ya rushwa katika taasisi zinazopaswa kutetea wafanyakazi, ikidaiwa kuwa baadhi ya maofisa huzungumza na waajiri pekee badala ya kusikiliza malalamiko ya pande zote panapotokea mgogoro kazini.
Emmanuel Geofrey, mfanyakazi wa kiwanda cha nguo Gongo la Mboto, Dar es Salaam, amesema mishahara yao ni midogo ya kima cha chini cha Sh150,000 ambacho hakiendani na uhalisia wa maisha mtaani.
Naye Eugene Andrew, mfanyakazi katika kiwanda cha unga Ubungo, Dar es Salaam, ametaka kuwe na ufuatiliaji katika sekta binafsi na hasa kuhusu mikataba ya ajira ambayo, ilivyo sasa, baadhi ni ya kinyonyaji.
Costantine Mathias, mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi kwenye vyombo vya habari (Jowuta), amesema wanahabari wengi hawana mikataba ya ajira wala bima ya afya, hivyo mamlaka husika zisimamie masilahi yao.
Samuel Mlemba, ofisa biashara katika duka la kuuza vyombo Kariakoo, na Shaban Mtoro, anayefanya kazi hoteli ya Serena, wamependekeza kuundwa tume maalumu ya Rais itakayoshughulikia changamoto za sekta binafsi, ambazo baadhi wamedai huwanyonya wafanyakazi kwa kufanya kazi nyingi na kwa muda mrefu, huku malipo yakiwa duni.
Wengine wameonyesha matumaini kwamba hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya Mei Mosi itagusa masuala ya msingi ya wafanyakazi, hususan katika mwaka huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Wamesema Mei Mosi inapaswa kuwa fursa ya kusikia ahadi na mwelekeo mpya katika kuboresha masilahi ya wafanyakazi, hususan wale wa ngazi ya chini.
Nyanga Elias, ofisa maendeleo ya jamii katika Kata ya Gidas, wilayani Babati Mkoa wa Manyara, amesema anatarajia masilahi ya watumishi yataboreshwa zaidi katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025.