Mizengwe ya uchaguzi yaanza CCM, wajumbe walalama kuwekwa kando

Bunda. ‘Mizengwe imeanza’ ndio neno unaloweza kutumia kwa kile kinachoendelea katika Chama cha Mapinduzi (CCM) katika matawi mbalimbali ya Kata ya Nyamuswa, wilayani Bunda, mkoani Mara.

Zaidi ya wajumbe 100 wa mabaraza ya mashina ya CCM kutoka matawi mbalimbali ya Kata ya Nyamuswa, wilayani Bunda, mkoani Mara, wameripoti kuondolewa kwenye nafasi zao.

Wajumbe hao wanahusisha hatua hiyo na maandalizi ya mchakato wa kura za maoni ndani ya chama, unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu kama sehemu ya kuelekea uchaguzi mkuu.

Hata hivyo, Mohamed Kizuri, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nyamuswa akizungumza na Mwananchi kuhusiana na hilo, amekiri kusikia madai hayo japo hayajawasilishwa rasmi ofisini kwake.

Baadhi ya mabalozi na waliokuwa wajumbe wa mashina ya CCM katika tawi la Bukama wakiwa kwenye ofisi ya CCM tawi la Bukama wilayani Bunda kabla ya kuongea na waandishi wa habari juu ya madai ya kuondolewa kwenye nagasi za ujumbe wa baraza kwenye mashina yao kinyume na utaratibu.  Picha na Beldina Nyakeke

Hivyo ametoa wito kwa wote walioathirika kufikisha malalamiko yao rasmi ili yafanyiwe kazi kwa utaratibu wa kichama.

“Masuala ya kichama yanazungumzwa kwenye vikao rasmi. Wakija mapema, tutayashughulikia kabla ya mchakato wa kura kuanza,” amesema Kizuri.

Naye Katibu wa CCM wa kata hiyo, Changwe Bita ameiambia Mwananchi kwa simu kuwa hajapokea pia malalamiko hayo rasmi. Amesema wote wenye malalamiko wayafikishe ngazi za juu ili yafanyiwe kazi.

Baadhi ya mabalozi na wajumbe wa mashina hayo ya CCM katika Kata ya Nyamuswa wanalalamikia uamuzi wa kuwaondoa kwenye nafasi zao bila kufahamishwa sababu rasmi. Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Aprili 30, 2025, wamesema uamuzi huo ulifanyika wiki mbili zilizopita kwa maelekezo ya uongozi wa kata bila kuzingatia taratibu za chama.

Wamedai kuwa walichaguliwa kihalali mwaka 2022 kupitia mchakato wa kidemokrasia katika mashina yao, hivyo wanashangazwa na hatua hiyo ambayo haikufuata utaratibu wowote rasmi wa chama.

Jackson Nyaburi, mmoja wa wajumbe walioondolewa, amesema anaamini kuwa hatua hiyo inalenga kuandaa safu ya uongozi kwa ajili ya nafasi za udiwani na ubunge, kwa kuwahusisha watu wanaotaka kujiimarisha kwa njia zisizo halali.

“Kwa sasa wajumbe wa mabaraza ya mashina ndio wapiga kura wa awali katika mchakato wa kupata wagombea wa ubunge na udiwani, hivyo huu ni mkakati wa baadhi ya watu kupanga safu mapema kwa maslahi yao binafsi. Hatukubaliani na mchezo huu,” amesema

Ameongeza kuwa kila mtu anayo haki ya kugombea na kuchaguliwa, hivyo si sahihi kwa baadhi ya wanachama kutumia mbinu zisizo halali kuwanyima wengine haki hiyo.

Kwa upande wake, Magesa Magesa, Balozi wa Shina namba 17 katika Tawi la Bukama, amesema alishtushwa na hatua ya uongozi wa kata kuleta majina ya wajumbe wapya wasiokuwa sehemu ya mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2022.

amesisitiza kuwa hakuna sababu ya msingi iliyowasilishwa kama vile kifo, kujiuzulu, au kuhama kwa wajumbe waliokuwepo.

“Ninashangazwa kuona majina mapya yakiwasilishwa ilhali mimi kama balozi sijaonyesha malalamiko yoyote kuhusu wajumbe wangu. Hili ni jambo la kushangaza na linapaswa kurekebishwa mara moja,” amesema Magesa.

Rehema Kizuri, Balozi wa Shina namba 6, amesema tangu waanze kazi mwaka 2022 wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na wajumbe wake bila matatizo yoyote.

Amesema mabadiliko hayo ya ghafla si ya kidemokrasia na yataleta migogoro isiyo ya lazima ndani ya chama.

“Majina mapya yaliyowasilishwa hata hayahusiani na maeneo yetu, kuna jina la mtu aliyehama kijijini zaidi ya miaka 20 iliyopita. Hii inatufanya tujiulize lengo la mabadiliko haya ni nini,” amedai Rehema.

Katibu Mwenezi wa CCM Tawi la Bukama, Terita Terita amesema aliombwa na kata kuwasilisha orodha ya wajumbe wa mashina wote ndani ya tawi lake miezi mitano iliyopita, jambo ambalo alilitekeleza kwa kushirikiana na mabalozi wa mashina yote.

Hata hivyo, anasema alishangazwa kuona kamati ya siasa ya kata ikimletea majina mapya ya wajumbe, kinyume na orodha halali iliyokubaliwa na mkutano wa tawi.

“Katika tawi langu pekee, majina 48 yameondolewa. Kata yetu ina matawi matano na yote yameguswa. Huu ni mkakati wa baadhi ya viongozi wanaotafuta kura za maoni mapema kwa kuweka watu wao kwenye mabaraza,” amesema Terita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *