Shujaa wa Kiswahili, Profesa Martha Qorro, afariki dunia

Dar es Salaam. Pigo limeikumba tasnia ya lugha ya Kiswahili kufuatia kifo cha mwanazuoni, Profesa Martha Qorro, kilichotokea leo Jumatano, Aprili 30, 2025.

Profesa Martha amewahi kuhudumu kama Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita), Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la HakiElimu na anatajwa miongoni mwa wanazuoni waliopigania Kiswahili kutumika kama lugha ya kufundishia.

Uthibitisho wa kifo cha mwanazuoni huyo umetolewa na mmoja wa wanafamilia, Edward Qorro, ambaye ameeleza kuwa Profesa Martha amefariki alfajiri ya leo, Aprili 30.

“Ni kweli amefariki alfajiri ya leo baada ya kuugua kwa takribani miaka mitatu. Tunamshukuru Mungu kwa maisha yake,” amesema Edward.

Akizungumza na Mwananchi, mwalimu na mwandishi wa vitabu, Richard Mabala, amesema kifo cha Profesa Martha ni pengo kubwa, hasa katika harakati za kupambania Kiswahili kiwe lugha ya kujifunzia.

Amesema enzi za uhai wake, alifanya kazi kubwa kama mwanazuoni na mtafiti aliyeonesha kwa ushahidi kwa nini wanafunzi wajifunze kwa lugha ya Kiswahili.

“Si kwamba alikuwa mtetezi mkubwa wa lugha ya Kiswahili tu, lakini alitumia muda wake kufanya tafiti na kuandika makala kuonesha kwa nini mtoto ajifunze kwa lugha yake. Martha aliumwa kwa muda mrefu, lakini hiyo haikuwa kikwazo kwake. Kila alipohitajika kwa ajili ya Kiswahili, alitoa mchango wake.”

Mabala amesema njia pekee ya kumuenzi Profesa Martha ni kuendelea kupigania alichokiamini siku zote, kwamba upo umuhimu mkubwa wa mtu kujifunza kwa lugha yake.

“Historia haizuiliki. Inaweza kucheleweshwa, na ndiyo maana nasema tutaendelea kupambania hili – watoto wafundishwe kwa lugha yao kwa kuwa ndiyo msingi mkuu wa elimu. Msingi wa elimu ni kujifunza kwa lugha ile unayoielewa,” amesema Mabala.

Kwa upande wake, Rasi wa Ndaki ya Isimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Mpale Silkiluwasha, amemtaja Profesa Martha kama mwanazuoni mchapakazi aliyetumia muda wake mwingi katika kufundisha, kufanya utafiti na kuandika machapisho kwenye eneo la lugha.

“Ni miongoni mwa wanazuoni mahiri waliotumika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Amekuwa Idara ya Lugha za Kigeni na alikuwa Mtanzania wa kwanza kuongoza Taasisi ya Confucius. Kabla ya hapo, wakurugenzi walikuwa Wachina.

“Martha aliamini lugha ndiyo nyenzo inayotumika kuwezesha mawasiliano, ndiyo sababu alikuwa kinara wa kutaka lugha ya Kiswahili itumike katika kufundishia, kwa sababu ndiyo Watanzania wanayotumia kwenye mawasiliano,” amesema Dk Mpale.

Katika mahojiano aliyofanya na gazeti hili mwaka 2021, Profesa Martha alionesha kutoridhishwa na hoja kuwa hakuna walimu wa kutosha kufundisha kwa kutumia lugha ya Kiswahili.

“Inawezekana wasiwepo. Kukosa walimu wa Kiswahili wakati hii ndiyo nchi inayojulikana ulimwengu mzima kuwa ni ya Waswahili, ni aibu. Hatupaswi kulalamika. Ni lazima tubadilike, tuwaandae wataalamu wa Kiswahili wa kutosha hapa nchini na kupeleka nchi nyingine.

“Tukubali kuwekeza katika elimu ambayo ina tija kwa taifa, siyo tija kwa wengine. Kwetu kwanza. Elimu iliyopo bado inamtumikia mkoloni hadi leo. Ipo kama tulivyoirithi, hatujabadilisha mambo ya msingi. Tunawaandaa watu wa kuwatumikia Waingereza; haimuandai Mtanzania kwenda kufanya kazi ya asili yake.”

Historia yake kitaaluma

Alipata shahada yake ya udaktari mwaka 1999 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa nadharia ya utafiti wa ubora wa ufundishaji na ujifunzaji wa uandishi wa Kiingereza katika shule ya sekondari Tanzania kuhusiana na mahitaji ya uandishi wa elimu ya juu.

Kabla ya kufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu 1983, Profesa Qorro alikuwa mwalimu wa sekondari akifundisha Kiswahili na Kiingereza.

Aliwahi pia kuhudumu kama mkuu na mhadhiri mwandamizi katika Idara ya Lugha za Kigeni, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Martha alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Shirika la HakiElimu sambamba na Jenerali Ulimwengu, Elizabeth Missokia, Rakesh Rajani, Wilbert Kapinga, Demere Kitunga, Elieshi Lema, Richard Mabala, Japhet Makongo, Marjorie Mbilinyi, Illuminata Tukai, Mary Rusimbi, Joseph Semboja, John Ulanga na Helen Kijo-Bisimba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *