Uingereza nayo yaanza kuwashambulia Wahouthi, waungana na Marekani

Sana’a. Jeshi la Uingereza, kwa kushirikiana na Jeshi la Marekani, limefanya mashambulizi ya anga dhidi ya wapiganaji wa Houthi nchini Yemen.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na tovuti ya Al Jazeera, maofisa wamesema mashambulizi hayo ya anga yamefanyika mapema leo, Jumatano, Aprili 30, 2025.

Mashambulizi hayo yanaashiria kushiriki kwa mara ya kwanza kwa Uingereza katika kampeni mpya ya mashambulizi makali inayoendeshwa na Marekani dhidi ya kundi la waasi wa Kihouthi, linalodaiwa kupata msaada kutoka Iran.

Tofauti na Marekani, ambayo hadi sasa imefanya zaidi ya mashambulizi 800 tangu kuanza kwa kampeni hiyo Machi 15 mwaka huu bila kutoa maelezo ya kina, Uingereza imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu sababu za kushambulia maeneo yanayoaminika kuwa ngome za wapiganaji wa Houthi nchini Yemen.

Kampeni hiyo, inayofahamika kwa jina la “Operesheni Rough Rider,” inalenga wapiganaji wa Kihouthi wakati Serikali ya Rais Donald Trump ikiendelea na mazungumzo na Iran, mfadhili mkuu wa kundi hilo  kuhusu mpango wa nyuklia wa taifa hilo, ambao unaendelea kusonga kwa kasi.

Shambulizi la Uingereza

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imeeleza kuwa shambulio hilo lililenga kundi la majengo yanayotumiwa na waasi wa Kihouthi kutengeneza ndege zisizo na rubani (drones) zinazotumika kushambulia meli katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden.

Majengo hayo yapo takriban maili 15 (sawa na kilomita 25) kusini mwa mji mkuu wa Yemen, Sana’a.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza imeeleza kuwa mashambulizi hayo yalitefanywa na ndege za kivita aina ya Royal Air Force Typhoon FGR4, zilizotumia mabomu yaliyoongozwa kwa teknolojia ya Paveway IV.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shambulizi lilifanyika baada ya giza kuingia, kipindi ambacho uwezekano wa kuwepo kwa raia katika eneo hilo ulikadiriwa kuwa mdogo.

Hata hivyo, Uingereza haikutoa taarifa kuhusu madhara ya mashambulizi hayo, ikiwemo iwapo kuna vifo au majeruhi. Kwa upande mwingine, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika Mashariki ya Kati (CENTCOM) haikutolea kabisa kauli kuhusu tukio hilo.

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza, John Healey, amesema kuwa hatua ya Uingereza kufanya mashambulizi hayo inalenga kujibu tishio la mara kwa mara kutoka kwa waasi wa Kihouthi dhidi ya uhuru wa usafiri baharini.

“Kupungua kwa usafirishaji kwa asilimia 55 kupitia Bahari Nyekundu tayari kumesababisha hasara ya mabilioni ya dola, kuchochea hali ya ukosefu wa utulivu katika eneo, na kuhatarisha usalama wa kiuchumi kwa familia za Uingereza,” amesema Healey.

Kwa upande wao, wapiganaji wa Kihouthi wameripoti mashambulizi kadhaa karibu na mji mkuu wa Yemen, Sana’a, ambao uko chini ya udhibiti wao tangu mwaka 2014. Mashambulizi mengine yalifanyika katika maeneo ya karibu na mji wa Saada, ngome nyingine ya kundi hilo kaskazini mwa nchi.

Uingereza imekuwa ikishiriki katika mashambulizi ya anga pamoja na Marekani tangu utawala wa Rais Joe Biden ulipoanzisha kampeni dhidi ya waasi wa Kihouthi mnamo Januari 2024.

Hata hivyo, shambulizi hili ni la kwanza kushirikisha Uingereza chini ya utawala mpya wa Rais Donald Trump, aliyeingia madarakani Januari 20, 2025.

Marekani kushambulia Gereza

Shambulizi la pamoja kati ya Uingereza na Marekani limefanyika leo, ikiwa imepita siku moja tangu CENTCOM idaiwe kufanya shambulizi la anga Jumatatu lililolenga gereza lililokuwa linahifadhi wahamiaji wa kutoka barani Afrika, na kuua watu wasiopungua 68 na kuwajeruhi wengine 47.

Jeshi la Marekani limesema linafanya uchunguzi wa madai hayo.

Aprili 18, shambulizi la Marekani katika bandari ya mafuta ya Ras Isa liliua watu wasiopungua 74 na kuwajeruhi wengine 171 likiwa shambulizi lenye vifo vingi zaidi katika kampeni ya Marekani.

Marekani inaendesha mashambulizi dhidi ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen kupitia meli zake mbili za kubeba ndege za kivita zilizoko katika eneo hilo: USS Harry S. Truman, iliyoko katika Bahari Nyekundu, na USS Carl Vinson, iliyoko katika Bahari ya Arabia.

Katika mashambulizi yake, Marekani imesema inalenga kuzuia mashambulizi ya Kihouthi dhidi ya meli zinazopita Bahari Nyekundu, njia muhimu ya kimataifa ya biashara, pamoja na mashambulizi dhidi ya Israel.

Wahouthi ni kundi la mwisho la wapiganaji ndani ya kile kinachoitwa na Iran Muungano wa Upinzani lenye uwezo wa mara kwa mara kushambulia Israel.

Mashambulizi hayo pia yameibua mzozo nchini Marekani baada ya Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth kudaiwa kutumia programu ya ujumbe isiyo na usalama ya ‘Signal’ ambayo ilidaiwa kusambaza taarifa nyeti kuhusu operesheni hiyo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *